SERIKALI YAHAIDI KUKAMILISHA MIRADI YOTE WALIYOIANZA NA KUAHIDI
Baadhi ya viongozi waliojitokeza katika viwanja vya Mji Mwema Kigamboni, jijini Dar es Salaam kushuhudia kampeni za CCM ambapo Makamu wa Rais na mgombea mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya CCM Samia Suluhu Hassan amenadi sera ya chama hicho pamoja na kuomba kura za mgombea Urais Dkt. John Joseph Magufuli, Wabunge na Madiwani wa Chama hicho, leo jijini Dar es Salaam.
*Mpango wa MEMKWA kuimarishwa
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MAKAMU Wa Rais na Mgombea mwenza wa kiti cha urais Samia Suluhu Hassan amesema, hadi serikali ya awamu ya tano itakapomaliza mhula wake miradi yote waliyoianza na kuahidi itakuwa imekamilika na kila mwananchi atakua amefikiwa na huduma zote muhimu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 na zoezi kuomba kura katika Wilaya ya Kigamboni jijini humo Mama Samia amesema kuwa Wana Dar es Salaam wanapenda maendeleo na hiyo imedhihirika katika ziara alizofanya katika Wilaya tatu, ambazo mamia wakazi wa jimbo hilo walijitokeza kusikiliza sera za chama pendwa cha CCM, na kusema kuwa mkakati uliopo ni kukamilisha miradi yote iliyoanza na ile iliyotolewa ahadi.
"Hadi kumaliza mhula wetu, miradi yote tuliyoianza na kuitolea ahadi itakua imekamilika na kila mwananchi atakuakua amefikiwa na huduma muhimu za Afya, Maji, Elimu na Umeme na ninawaomba tufanye kampeni za amani na utulivu, na ikifika Oktoba 28 mwaka huu, tukapige kura kwa CCM, Mkamchague Rais Dkt.John Joseph Magufuli na mimi mgombea mwenza, pamoja na wabunge na madiwani wa CCM na ninawahimiza wale wa vyama pinzani nao wakapige kura" ameeleza.
Amesema kuwa, mfumo wa elimu bure umeendelea kuwanufaisha watoto wengi nchini wakiwemo wa jiji hilo, na kusema kuwa wataendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya elimu, kuendelea kutoa mikopo ya elimu ya juu pamoja na kutoa walimu wa sayansi.
"Pia tutaboresha mpango wa MEMKWA ili watoto wetu waweze kusoma na kuandika, tutahakikisha kila mtoto anapata elimu bora ......" Ameeleza.
Vilevile amesema kuwa kero ya Maji Kigamboni inaenda kuwa historia, kila mwananchi jimboni humo atafikiwa na huduma ya maji ya bomba.
Kuhusiana na miundombinu, Samia amesema kuwa ujenzi wa barabara na uboreshaji wa barabara ndani ya jiji la Dar es Salaam zitajengwa na kuimarishwa na hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, Miundombinu ya Maji ambapo kwa jimbo la Kigamboni kero ya maji inakaribia kuisha na kila mwananchi atafikiwa na huduma hiyo ifikapo mwezi Aprili.
"Daraja la Gerezani, mmeona kuna ujenzi unaendelea ni daraja kubwa sana ambalo serikali inajenga, tunajipanga kujenga treni kwa jiji la Dar es Salaam na kufufua njia zilizosimama....pia tunajipanga kuwekeza ndege za masafa marefu za abiria pamoja na ndege za mizigo" ameeleza.
"Katika sekta za afya tumejipanga vyema mwendo ni ule ule.. hapa Kigamboni kuna hospitali mbili za Wilaya, afya ni kipaumbele chetu...kila mwananchi lazima afikiwe na huduma ya Afya" amesema Samia.
Vilevile amesema kuwa wanampango wa kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kufikia malengo ya kupokea watalii milioni tano kwa mwaka kutoka watalii milioni mbili wanaofika nchini kutalii kwa mwaka.
Kwa upande wake Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wanakigamboni kupiga kura za ndio kwa Rais Magufuli ili kumalizia kazi za kimaendeleo ziliyobaki na kuhaidi kuwa katika miaka mitano ijayo mitaa yote itapata umeme na kero ya Maji wa jimbo hilo itakua historia.
"Nguzo zimeshatandazwa umeme ni uhakika....Kigamboni itakuwa uwanja wa uwekezaji...asilimia 75 ya wavuvi wanatoka Kigamboni na tayari soko la samaki limejengwa kwa shilingi milioni 75 ambazo ni mapato ya ndani huko Pemba Mnazi..Tuchague CCM kazi iendelee" amesema Ndugulile.
Aidha Ndugulile ameiomba Serikali kudaidia kutatua changamoto ya wavuvi waliozuiwa kuvua nyakati za mchana ili kuongeza kasi ya maendeleo.
No comments: