Bolt yazindua huduma mpya ya usafiri kwa bei nafuu katika majiji ya Arusha, Mwanza na Dodoma
Na Mwandishi wetu
Kampuni inayoongoza kwa utoaji huduma ya usafiri barani Ulaya na Afrika (BOLT), imezindua huduma mpya, nafuu ya usafiri inayofahamika kwa jina la ‘Bolt Lite’.
Huduma hiyo ambayo inalenga kuwapatia abiria huduma bora za usafiri kwa bei nafuu, itapatikana katika mikoa Arusha, Mwanza na Dodoma.
Akizungumzia ujio wa huduma hiyo mpya ya usafiri, Meneja wa Bolt nchini Tanzania, Remmy Eseka alisema huduma ya ‘Bolt Lite’ inalenga kufanya huduma za usafiri katika maeneo ya mijini kupatikana kwa bei nafuu zaidi ili wateja wetu wafaidike na huduma za Bolt.
Alisema pia lengo ni kuongeza idadi ya safari na mapato kwa madereva ambao ndio washirika wakubwa wa Bolt.
“Lengo la Bolt ni kufanya huduma ya usafiri katika maeneo yote ya mijini kupatikana kwa bei nafuu ili watu kada mbalimbali waweze kumudu gharama za safari. Kwa sababu kadiri safari zinavyoongezeka kwa madereva ndivyo kipato cha madereva hao kinavyozidi kuongezeka.
“Madereva wetu ndio kiini cha shughuli zetu, hivyo kutokana na ujio wa huduma hii tunaamini kwamba madereva watafanya kazi kwa furaha kwa kuwa wanatoa huduma bora na rafiki kwa mteja. Hii inathibitisha kwanini tumekuwa marekebisho na ubunifu wa kila mara katika utoaji wa huduma zetu.
“Yote haya tunafanya kwa lengo la kuwawezesha madereva ambao ndio washirika wetu wakubwa kupata mapato bora na kuifanya Bolt kubaki kuwa kampuni inayopendwa zaidi katika huduma za usafiri nchini, "alisema Bw Eseka.
Aidha, alifafanua kuwa Bolt Lite ni huduma ya hiari kwa madereva ya Bolt ambayo inawaruhusu kusimamia mapato yao wakati wanakubaliana malipo na wateja wao ili kuendana na hali halisi ya janga la maambukizi ya Virusi vya COVID-19.
“Ni huduma ambayo inatoa fursa kwa wateja kulipa gharama ndogo kwa safari zao huku wakiwa na uhakika wa kupata huduma bora, salama na za uhakika.
“Kitengo cha Lite kitakuwa na magari ya injini zenye uwezo wa 1,500cc na yale yaliyo chini ya hapo. Kundi hilo pia litaruhusu madereva walio na magari yenye injini zenye uwezo mkubwa zaidi ya huo kubadili kati ya kitengo cha Lite na vitengo vingine vya kawaida kwenye huduma za Bolt,” alisema.
Alisema Bolt ina watumiaji zaidi ya milioni 30 katika nchi zaidi ya 35 barani Ulaya na Afrika. Huduma zake zilitokana na mashindano ya kupanda milima na huduma za usambazaji vyakula au vifurushi kwa kutumia baiskeli za umeme,” alisema.
No comments: