SEPTEMBA 11, SIKU ILIYOACHA KUMBUKUMBU KUBWA KWA MAREKANI
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
NI miaka 19 sasa tangu litokee shambulio kubwa kuwahi kutokea duniani, ilikua ni mwendelezo wa mashambulio manne ya kigaidi na shambulio hilo lilitekelezwa na kikundi cha kigaidi cha al-Qaeda chini ya kiongozi wao Osama bin Laden dhidi ya Marekani.
Taarifa kutoka kwa mamlaka husika zilieleza kuwa kundi hilo la kigaidi liliteka nyara ndege nne na kuzitumia kama silaha kwa kuzigongesha kwa makusudi katika majengo mawili ya Washington DC, na Newyork yaliyokuwa yakitizamana, maarufu kama "Twin Towers" yenye jumla ya ghorofa 210 yaani ghorofa 110 kwa kila jengo.
Tukio lilianza hivi, Kati ya ndege nne zilizotekwa nyara, ndege ya Shirika la ndege la Marekani "Flight 11" iliyobeba abiria 92 ilikua ndege ya kwanza kugonga mnara wa Kaskazini mwa jengo la kibiashara la kimataifa la "World Trade Center" la mjini Newyork majira ya saa 2:46:30 asubuhi.
Ndege ya Shirika la United Airlines "Flight 175" ilitumiwa kugonga upande wa kusini wa mnara wa jengo hilo la biashara la kimataifa majira ya saa 3:02:59 asubuhi.
Pia ndege ya Shirika la American Airlines "Flight 77" ilitumiwa kugonga jengo la Pentagon la mjini Arlington,Virginia karibu kabisa na Washington DC majira ya saa 3:37:46 asubuhi.
Ndege ya shirika la United Airlines, "Flight 93" haikubahatika kugonga mahala popote, iliangushwa majira ya saa 4:03:11 asubuhi, inasemekana kuwa magaidi hao walitaka kuigongesha ndege hiyo katika jengo la mji mkuu wa Marekani, haikufanikiwa ikaishia kuanguka karibu na mji wa Shankville, Pennsylvania.
Shambulio la Septemba 11, liliacha vifo zaidi ya elfu tatu, majeruhi zaidi ya elfu ishirini, matatizo endelevu ya kiafya pamoja na uharibifu na hasara kwa miundombinu yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 10 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 22 za kitanzania.
Pia taarifa kutoka jeshi la polisi zilieleza kuwa askari 78 walipoteza maisha na miili yao haikupatikana na askari 200 wa jeshi la zima moto walipoteza maisha.
Licha ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Barack Obama kutangaza kuuawa kwa kiongozi wa kundi hilo Osama bin -Laden bado siku ya Septemba 11 imebaki kuwa kumbukumbu kwa raia wa Marekani na ulimwengu kwa ujumla.
No comments: