MFANYABIASHARA WA KUUZA SUFURIA ASHIKILIWA NA TAKUKURU KWA KUMWEKA KINYUMBA MWANAFUNZI WA KIDATO CHA PILI
Na Jumbe Ismailly IKUNGI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida imefanikiwa kumkamata,Mfanyabiashara wa kuuza sufuria,Ashirafali Ibrahimu Mohamed (51) mkazi wa Mtaa wa Upanga,jijini Dar-es-Salaam kwa tuhuma za kumweka kinyumba mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Dadu iliyopo Kata ya Dung’unyi,wilayani Ikungi.
Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Ikungi,Erick Nyoni alisema kwamba tukio hilo limetokea,Juni,14,mwaka huu ambapo mtuhumiwa alimshawishi mwanafunzi huyo wakati akiwa katika likizo ya lazima ya ugonjwa wa COVID 19,unaosababishwa na virusi vya CORONA na kisha kwenda kuishi naye jijini Dar-es-Salaam.
Aidha Nyoni alisisitiza kwamba mtuhumiwa huyo mwenye asili ya kiasia ametiwa mbaroni baada ya kumkuta akiwa na mwanafunzi huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni Kijiji cha Puma,ambako ndiko walikofikia wakati akiwa njiani kwenda nyumbani kwa mwanafunzi huyo kutekeleza ahadi yake ya kumjengea nyumba ambayo alikwisha peleka jumla ya bati 32.
“Tulipata taarifa zake toka tarehe 14/06/2020 kwamba alimshawishi binti huyo wakati wakiwa kwenye sherehe pale nyumbani kwao akamdanganya kwamba waende naye kununua soda kwa ajili ya wageni,lakini alipoondokana naye kwenye pikipiki yake aliendanaye mpaka Kijiji cha Puma hadi kwenye nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Makuru na alimfungia ndani ya moja ya vyumba vya nyumba hiyo”alifafanua Nyoni.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa TAKUKURU baada ya mwanafunzi huyo kutoweka katika mazingira ya kutatanisha ndipo wazazi walitoa taarifa TAKUKURU na ndipo kwa siku hiyo kwa kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi walijitahidi kumtafuta bila mafanikio.
“Kwa kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi walijitahidi sana kumtafuta kwa siku hiyo kwa kutumia simu lakini wakati akitoa maelekezo ya mahali walipokuwa hakuwa mkweli kwamba mara yupo Singida mjini,mara yupo kwenye maeneo ya starehe kumbe uongo”aliweka bayana Mkuu huyo wa TAKUKURU.
Hata hivyo Nyoni aliweka bayana kwamba ndipo siku iliyofuata juni,15,mtuhumiwa alipoondoka na mwanafunzi huyo na kwenda naye hadi jijini Dar-es-Salaam na kumfanya binti huyo kusitisha masomo yake na kwa kuwa mtuhumiwa ni mfanyabiashara anayeuza sufuria,hivyo akawa anazunguka naye katika mikoa mbali mbali kama vile Lindi,Iringa,Mwanza,Shinyanga na Mkoa wa Tabora.
Mkuu huyo wa TAKUKURU hata hivyo alisisitiza kuwa kutokana na mitego waliyoweka,walifanikiwa kupata taarifa za kiintelijinsia kwamba sept,21,mwaka huu mtuhumiwa Ashrafali atakwenda Ikungi kutekeleza ahadi ya kulipia gharama za kiwanja kitakachojengwa nyumba ya mwanafunzi huyo na ndipo walipofanikiwa kumtia mbaroni.
“Mtu huyu ni mharibifu,kwani kabla ya kumshawishi mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Dadu,awali alimshawahi kumchukua binti mwingine na kumpeleka Dar-es-Salaam na baada ya kumtumia,alimtelekeza na aliporudi alikwenda kumchukua tena binti mwingine naye vile vile alimtelekeza na ndipo aliporudi,alimchukua mwanafunzi huyo”.alisisitiza Nyoni.
Hata hivyo Nyoni alisisitiza kwa wananchi wa Ikungi kwamba wilaya ya Ikungi imepiga marufuku vitendo hivyo wasingependa kusikia tena vitendo kama hivyo vikiendelea kutokea na kuonya kwamba mtu yeyote atakayebainika kukatisha wanafunzi masomo na kuwapa mimba,suala hilo katika wilaya hiyo halitapewa nafasi kabisa kuendelea kutokea kwani Rais ametoa nafasi ya wanafunzi kusoma bila malipo.
“Lakini niwajulishe waandishi wa Habari na wananchi wa Ikungi kwa ujumla kwamba vitendo hivi katika wilaya ya Ikungi tumepiga marufuku na tusingependa tena kusikia vitu kama hivi,matatizo ya watoto wa shule kukatishwa masomo.kupewa mimba suala hilo katika wilaya ya Ikungi tusingependa tena tulione”alibainisha Nyoni.
“Rais wetu anatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wanasoma bure,lakini baadhi ya watu wachache wenye nia mbovu na serikali hii wamekuwa wakiwapotosha watoto wetu,wakitoa fedha kwenye familia ili wachukue watoto wetu na huyu bwana katika kuwashawishi wazazi wa familia ile,amewajengea na nyumba lakini vile vile alimuahidi huyu binti kwamba atamnunulia kiwanja na atamsomesha masomo ya kompyuta kwa hivyo binti akashawishika akaacha shule,hata hivyo alimwachisha shule kwa lazima”.alisisitiza Mkuu huyo wa Takukuru.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’inyi,Yahaya Juma Njiku hakusita kumshukuru kipekee Rais Dlt John Pombe Magufuli kwa kuwapatia Mkuu wa Takukuru mwenye uadilifu wakati wa kutekeleza amajaukumu yake.
“Kipekee sisi tuendelee kumshukuru Mh Rais kama viongozi wake na wasaidizi wake wa ngazi ya chini tunahakikisha kwamba ile dhana yake inatimia kikamilifu kwa maana ya elimu bila malipo watoto wetu wanasoma na pale ambapo inapotokea mtu analeta sintofahamu kuhakikisha watoto hawapati elimu tunamshughulikia kikamilifu kwa kuhakikisha sheria zinachukuliwa”alisema.
Hata hivyo walimu wa shule ya sekondari Dadu anakosoma mwanafunzi huyo wameahidi kumpokea,kuingia darasani ili aweze kuendelea na masomo baada ya kukutana naye ana kwa ana na mwanafunzi huyo kuonyesha dhamira ya kuendelea na masomo.
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi,Erick Nyoni (wa kwanza kutoka kushoto) akimhoji mfanyabiashara,Ashrafali Ibrahimu Mohamed(wa tatu kutoka kulia) baada ya kutoka kituo kidogo cha polisi Ikungi.
Mtuhumiwa,Ashrafali Ibrahimu Mohamed akiwa chini ya ulinzi katika ofisi za TAKUKURU wilaya ya Ikungi.
Mtuhumiwa Ashrafali Ibrahimnu Mohamed akitoa sufuria anazouza kuwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuhojiwa katika ofisi za TAKUKURU wilaya ya Ikungi.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
No comments: