KASI YA TANESCO DODOMA INARIDHISHA- DKT. KYARUZI

Na Mwandishi Wetu

BODI ya Wakurugenzi TANESCO ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Alexander Kyaruzi wameipongeza TANESCO kwa kasi kubwa ya utekelezaji na uendelezaji wa huduma za umeme wa uhakika kuendana na kasi kubwa ya ukuaji wa Jiji la Dodoma kwa sasa.

Dkt. Kyaruzi alieleza kuwa kituo cha kupoza na kusambaza Umeme cha Zuzu Dodoma, kina uwezo wa Megawati 48 ambapo kwa sasa zinatumika Megawati 35 kulingana na matumizi yaliyopo, ziada ikiwa ni Megawati 13 kwa Dodoma lakini pia zitaongezwa tena Megawati 250.

Aliongeza kuwa TANESCO tayari wanakamilisha upanuzi wa kituo cha Zuzu, upanuzi ambao utaongeza Megawati hizo 250 za ziada, hivyo kuwezesha upatikanaji wa takriban Megawati 300 kwa Jiji la Dodoma kuendana na kasi ya ukuaji wa Jijini hilo.

Dkt. Kyaruzi aliongeza kuwa, kasi ya Jiji la Dodoma kupanuka kwa ujenzi wa makazi mapya, uwekezaji mpya, huduma za kijamii, ukuaji wa uwekezaji katika biashara pamoja na viwanda ni mkubwa hivyo kufanya mahitaji ya umeme kuongezeka kwa kasi kila siku.

“Tumeridhishwa na kasi ya TANESCO baada ya kujionea kuwa wanakaribia kukamilisha upanuzi wa kituo cha Zuzu kwa kuongeza tranfoma mbili kubwa zitakazo ongeza Megawati 250 za ziada. Ongezeko hilo litawezesha upatikanaji wa umeme mwingi na uwekezaji mkubwa Jijini Dodoma” Alisema Dkt. Kyaruzi

Dkt. Kyaruzi aliongeza kuwa ndani ya mwezi Septemba upanuzi huo utakuwa umekamilika na umeme huo utakuwa tayari kwa matumizi kulingana na mahitaji yote Jijini Dodoma.

Kwa upande wa Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Peter kigadye alieleza kuwa, TANESCO inatekeleza miradi mikubwa ya umeme kwa ustadi mkubwa ikitumia uzoefu ilioupata katika upanuzi na uendelezaji wa miundombinu ya umeme katika majiji ya Dar es Salaama, Mwanza na Arusha.

“Tunatekeleza miradi hii ya upanuzi wa miundombinu ya umeme Dodoma kwa kutumia uzoefu mkubwa tulio upata katika majiji mengine tukizingatia ongezoko la makazi, biashara, Viwanda pamoja na idadi ya watu” alisema Mhandisi Kigadye.

No comments: