WASIMAMIZI WASAIDIZI WA UCHAGUZI JIMBO LA MBINGA MJINI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA NA KANUNI ZA TUME YA UCHAGUZI

Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Mbinga Mjini Grace Quintine akifungua mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata na jimbo kwa ajili ya kuwajengea uwezo kabla yakuanza kwa uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.


Baadhi ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi jimbo la Mbinga mjini wakimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Mbinga Grace Quintine(hayupo pichani)wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi hao yaliyofanyika ukumbi wa Halmashauri Mbinga.
Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Mbinga mjii Amos Sangama akongea jana na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata na jimbo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo.

Mwanasheria wa Halmashauri ya mji Mbinga Elizaberth Moshi akitoa nasaha kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata na Jimbo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya mji Mbinga.

Picha na Muhidin Amri

…………………………………………………………………………

Na Mwandishi Wetu,Mbinga

MSIMAMIZI wa Uchaguzi jimbo la Mbinga mjini Grace Quintine,amewataka wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata, kufuata kanuni na sheria za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 Mwaka huu.

Quintine ametoa rai hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa maafisa hao katika Ukumbi wa Halmashauri ya mji Mbinga ambayo yanalenga kuwajengea uwezo katika kusimamia uchaguzi huo.

Alisema, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 74kifungu kidogo cha 6,Tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Madiwani,Wabunge na Rais.

Hata hivyo,pamoja na kuwa Tume hiyo ndiyo yenye jukumu hilo,watakaoratibu na kusimamia uchaguzi katika mikoa na Halmashauri kwa karibu zaidi ni watendaji hao walioteuliwa na tume hiyo.

Alisema, Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatia kwani hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri,wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato huo.

Aidha, amewataka kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea,na wahakikishe wanazingatia matakwa ya katiba,sheria na kanuni zinazosimamia zoezi zima la uchaguzi Mkuu.

Amewaeleza kuwa, wameaminiwa na kuteuliwa kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi hiyo na kwamba wanapaswa kujiamini,kujitambua na kuzingatia katiba ya nchi,sheria za uchaguzi na kanuni zake,maadili ya uchaguzi na melekezo mbalimbali yanayotolewa na tume.

Quintine amewataka maafisa hao kuhakikisha,katika utekelezaji wa majukumu yao wanapaswa kuvishirikisha vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ambayo wanastahili kushirikishwa na siyo vinginevyo.

Kwa upande wake Afisa Msaidizi wa Uchaguzi jimbo la Mbinga mjini Amos Sangana alisema, katika jimbo hilo kuna kata 19 ambapo jumla ya watendaji 30 wamepewa mafunzo kwa ajili ya kwenda kusimamia uchaguzi mkuu ngazi ya kata.

Alisema, tume inatarajia mara baada ya mafunzo hayo watendaji hao watakwenda kusimamia kikamilifu mchakato wa uchaguzi kwa kuanzia zoezi la utoaji fomu na uteuzi wa wagombea.

Kwa mujibu wa Sangana,tume ina amini mafunzo hayo yatawezesha wateule hao kwenda kutekeleza majukumu yao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na weledi wa hali ya juu.

Naye afisa Utumishi wa Halmashauri ya mji Mbinga Elizabert Moshi amewataka maafisa hao kuwa makini wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea au kufuata maelekezo kwa watu wasiohusika na tume ya uchaguzi.

Alisema, suala la uchaguzi ni jambo nyeti katika nchi yeyote inayofuata na kuzingatia utawala wa sheria na katika utumishi wa umma kuna utaratibu wa maalum wa kufanya mawasiliano, hivyo katika mchakato huo watatakiwa kufuata maelekezo ya Tume na wasimamizi wa uchaguzi na siyo vinginevyo.

No comments: