TUME YA UCHAGUZI YAKANUSHA UWEPO WA WAGOMBEA WALIOPITISHWA BILA KUPINGWA
Charles James, Michuzi TV.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba wapo wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani waliopitishwa bila kupingwa.
NEC pia imesambaa hakuna pingamizi lolote lililotolewa kwa wagombea wa Urais wa vyama 15 ambavyo jana vilipitishwa na tume kugombea.
Akizungumza na wandishi wa habari katika Ofisi za Tume Njedengwa jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Dk Wilson Charles amesema tume bado haijatoa taarifa yoyote ya kutangaza mgombea wa mbunge au Udiwani ambaye amepitishwa bila kupingwa.
Dk Wilson amesema haiwezekani wawepo wagombea ambao wamepita bila kupingwa ilihali muda wa kuwekewa mapingamizi ambao kisheria ni kuanzia jana saa kumi jioni baada ya kupitishwa hadi leo saa kumi jioni.
" Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (2) cha sheria ya Tume ya Uchaguzi sura ya 343 pingamizi linaweza kuwekwa kwa wagombea wa ubunge kama zuio kwa wagombea aliyeteuliwa kuanzia saa kumi jioni ya siku ya uteuzi hadi saa kumi jioni ya siku inayofuatia baada ya siku ya uteuzi.
Sasa ni jambo la kushangaza kuona vipo vyombo vya habari ambavyo vinatangaza uwepo wa wagombea waliopitishwa bila kupingwa kabla ya muda wa mapingamizi kuisha, tunawasihi sana ndugu zetu wanahabari kuepusha kutoa taarifa ambazo hazijathibitishwa na tume," Amesema Dk Wilson.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk Wilson Charles Mahela akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma
No comments: