ALIYEKUWA KAMISHNA WA TRA NA WEZAKE KULIPA FIDIA YA BILIONI 1.5

BAADA ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka mitano hatimae leo Agosti 26, 2020 Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi imemuhukumu aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (70) na wenzake wanne kulipa fidia ya Sh  bilioni 1.5 baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na kukiri makosa yaliyokuwa yanawowakabili.

Pia mahakama imewataka washtakiwa hao kila mmoja kulipa faini ya Shilingi milioni moja au kwenda jela miezi sita kwa kukiri mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya USD 6,000,000.

Mbali na Kitilya washitakiwa wengine ni Maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare (44), Sion Salomon (44), Kamishina wa Sera ya Uchunguzi wa Madeni kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Benason Shallanda (59)
 na Msaidizi wake Alfred Misana (50).

Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Immaculata Banzi ambapo mapema kabla ya kusomwa kwa adhabu kwa Adhabu, DPP Biswalo Mganga alidai kuwa alipokea barua ya washtakiwa wakiomba kuingia makubaliano ya kukiri makosa yao na kwamba baada ya majadiliano amewafutia washtakiwa hao mashtaka 57 kati ya 58 waliyokuwa wanakabiliwa nayo.

Hivyo aliomba mahakama kuyapokee makubaliano hayo na kuyasajili kwa mujibu wa sheria na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.

Kufuatia taarifa hiyo, mahakama imeyapokea makubaliano hayo kwa mujibu wa kifungu cha 194 (D) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 ambayo inaelekeza kila mshitakiwa ahojiwe na mahakama ichukue majibu yake.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, DPP Mganga alidai hawana rekodi ya makosa ya nyuma ya washtakiwa hivyo, aliomba kwa kujibu wa makubaliano washitakiwa walipe Sh bilioni 1.5 kama fidia ya hasara waliyosababisha.

Katika utetezi wao washtakiwa kupitia jopo la mawakili wa wao  wakiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa walidai washitakiwa ni wakosaji wa kwanza na kwamba mshitakiwa Kitilya ni mzee na anakabiliwa na maradhi mbalimbali hivyo, afya yake sio nzuri.

Akadai kuwa washitakiwa wote wanafamilia zinazowategemea na kitendo cha kukaa rumande kwa miaka minne na nusu, familia zao zilikuwa kwenye mahangaiko ya kimya kimya.

Pia akadai kuwa kukiri kwao makosa kumeokoa rasilimali fedha na muda wa mahakama lakini pia washitakiwa hawa wanatakiwa kulipa fidia katika mazingira hayo unawaingiza katika madeni ili waweze kulipa fidia. Ni rai yetu katika utoaji wa adhabu tunaomba uyazingatie utoe adhabu yenye unafuu na inayotekelezeka ili kukidhi haja ya sheria hii ambayo dhamira yake ni kupunguza mrundikano wa mahabusu gerezani. 

"Nimezingatia hoja za pande zote na kwa kuzingatia makubaliano mliyofikia mahakama inawahukumu kulipa faini ya Sh. milioni moja au kifungo cha miezi sita jela kila mmoja. Washitakiwa wote mlipe fidia ya Sh bilioni 1.5 kwa serikali ya Tanzania kwa hasara iliyopatikana," alifafanua Jaji Banzi

Katika mashtaka mapya iliyosomwa na, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya inadaiwa, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka ya kusababisha serikali hasara.

Imedaiwa Mei Mosi 2012 na Juni 1, 2015 wakiwa jijini Dar es Salaam isivyo halali washitakiwa waliandaa ada ya mkopo kwa serikali ya Tanzania wa  Dola za Marekani  Milioni 600, 000,000  kutoka  asilimia 1.4 hadi 2.4 na kusababisha serikali kupata hasara ya Dola za Marekani Milioni 6,000,00

No comments: