SHIRIKISHENI WANANCHI KWENYE MIRADI YA MAENDELEO - RC KUNENGE


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge (Katikati) akikagua mradi wa maji wa Pugu, Gongolamboto ambapo ameagiza miradi yote aliyoitembelea ikamilike kwa wakati ili wananchi wafurahie huduma hizo kutoka kwa Serikali, leo jijini Dar es Salaam.

Afisa mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi. Cyprian Luhemeja (katikati) akimwongoza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge (kulia) kukagua mradi wa maji wa Pugu, Gongolamboto, Luhemeja  amesema kuwa Mamlaka hiyo itaendelea na kasi ya usambazaji maji kwa kila mwananchi, leo jiji Dar es Salaam.

Afisa mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi. Cyprian Luhemeja (katikati) akimwonesha  Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge (kushoto) maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Pugu, Gongolamboto, leo jiji Dar es Salaam.


Zoezi la ukaguzi wa miradi likiendelea.


*Aipongeza DAWASA kwa kasi ya usambazaji wa huduma ya maji

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MKUU Wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge amesema kuwa wananchi wana haki ya kushirikishwa katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayojengwa  katika maeneo yao kwa kupewa taarifa za utekelezaji na ukamilikaji wake ili waone namna Serikali inavyofanya kazi katika Kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma zote muhimu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi wa maji ya Kisarawe II, unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) utakaowanufaisha wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani  jijini humo, Kunenge amesema kuwa ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya maendeleo ni muhimu sana ili wajue ni nini Serikali  inafanya.

"Ni muhimu wananchi wakajua ni nini Serikali inafanya, hivyo ni vyema viongozi wakatoa taarifa kwa wananchi juu ya miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na ni lini itakamilika ili waweze kufaidi matunda ya Serikali ambayo imejizatiti katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msingi" amesema Kunenge. 

Aidha ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kwa kuendeleza  juhudi za kumtua mama ndoo kichwani na kueleza kuwa maeneo ya uwekezaji kama Kigamboni  lazima yafikiwe na huduma za msingi kama maji, barabara na umeme ili kuvutia uwekezaji.

"Miradi itekelezwe kwa kiwango bora kulingana na fedha inayotumika na eneo kama Kigamboni huduma za maji, barabara na umeme ni  muhimu kutokana na shughuli za uwekezaji unaofanyika huku....DAWASA najua mlikotoka mnafanya kazi nzuri sana na endeleeni hivyo" amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa hadi kufikia Aprili mwaka ujao changamoto ya Maji kwa wakazi wa Kigamboni itakuwa ni historia na hiyo ni kutokana na ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Kimbiji na Mpera utakaokua na taki lenye ujazo wa lita milioni 15 zitakazosambazwa kwa wananchi wa  Kigamboni na maeneo ya jirani.

Mhandisi. Luhemeja amesema kuwa katika mradi huo tanki lenye uwezo wa kubeba lita milioni 15 litajengwa na  umetengewa shilingi bilioni 30 ambazo ni fedha za ndani zinazotokana na makusanyo na bili za maji na tayari umekamilika kwa asilimia 30 hadi kufikia mwezi Aprili mwakani na wakazi wa Kigamboni, Mjimwema, Kibada, Kisarawe II, na Vijibweni watafurahia huduma ya maji kutoka Mamlaka hiyo.

No comments: