NIT KUTOA WATAALAMU WA ANGA, WATAWEZA KUSAIDIA UENDESHAJI WA ATCL
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa wa kushoto waliokaa katikati akizungumza na uongozi wa ATCL namna wanavyoendesha mitaala mbali mbali ya mafunzo ya ndege wakati wa ziara ya viongozi wa baraza la chuo cha NIT katika kampuni hiyo ya ndege jijini Dar es Salaam. Kulia kwake aliyekaa miwani ni Blastus Nyichomba
Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, Kapteni Said Hamad akiwaeleza viongozi wa NIT namna Shirika hilo linavyofanua kazi zake na changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa ziara ya viongozi wa barazanla Chuo cha NIT katika Shirika hilo
Picha ya Pamoja.
MKUU wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa amesema kituo cha umahiri cha mafunzo ya usafiri wa anga kitazalisha wataalamu wengi ambao watasaidia uendeshaji wa Shirika la Ndege nchini (ATCL).
Amesema serikali imewekeza fedha zaidi ya Sh bilioni 50 ambazo zimewekwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kuzalisha wataalamu wa sekta ya anga.
Profesa Mganilwa amesema hayo leo wakati alipotembelea shirika hilo la ATCL, ili kuangalia mkataba wa makubaliano waliosaini mwaka 2012 kati ya NIT na ATCL.
Amesema kwa kutumia utaalamu mkubwa wa wataalamu waliopo ATCL, wataweza kuwapa mafunzo watanzania wengine wanaopenda kujifunza mashaka ya usafirishaji wa anga hivyo, wanatarajia kupata wataalamu wengi watakaoendesha shirika hilo liweze kukua.
"Leo hii shirika lina wafanyakazi 575 lakini baada ya miaka miwili ama mitatu litakuwa na wafanyakazi zaidi ya 1,000 ambao watakuwa ni watanzania, hivyo, niwasihi someni vizuri mpate maarifa katika kiwango cha kimataifa muweze kulihudumia Shirika letu la ndege la Taifa," amesema Profesa Mganilwa.
Amesema, hapo awali ATCL walikuwa na ndege mbili lakini baada ya serikali kuweka uwekezaji mkubwa, wamekuwa na ndege nane ambapo serikali imeweka zaidi ya Sh bilioni 15 katika shirika hilo.
Amesema lengo kubwa la kukutana ni mafunzo ya wataalamu wa usafirishaji wa anga kwamba hayawezi kukamilika kwa kumtoa mtu aliyeiva kama hakuna chuo karibu.
"Tumekuja hapa tuweze ku exchange notes ili mkataba huu wa makubaliano tulionao tuurudishe ili yale mawazo tuliyokuwa nayo kipindi hicho cha 2012 yaweze kukua zaidi kuendana na matakwa ama matarajio ya serikali," amesisitiza.
Amesema wanapokuwa pamoja na serikali kwa namna moja na watanzania ambao wanaolipa kodi watashuhudia kukua kwa uchumi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa ATCL Kapteni Said Hamad amelishukuru baraza la Chuo cha NIT na ATCL kwani walikuwa na majadiliano mazuri, wamepata faida kubwa sana.
"Moja ya vitu ambavyo tumeamua kuviendeleza ni kuongeza mshikamano kukaa pamoja na kuratibu njia sahihi ambazo zitatuwezesha kuendana na hali halisi ya soko ili kuwezesha NIT kuzalisha vijana ambao wataweza kuja kuwa faida katika shirika la ndege," amesema.
Pia amesema ATCL kuweza kubadilishana utaalamu kwa ajili ya kuisaidia NIT na hili litatusaidia kupeleka mbele mipango ya taasisi hizi mbili.
Kapteni huyo amesema miaka mitano ijayo wanatarajia kufanya mafunzo ili kupata rasilimali watu na kwamba wataanza kuona matunda ya namna wanavyoweza kuzalisha wataalamu kutoka humu humu ndani kwa gharama nafuu ambazo zitamuwezesha hata yule maskini waweze kufanya kazi hizo na kumaliza vizuri sana.
No comments: