NHIF YAWASHAURI WANANCHI KUCHANGAMKIA HUDUMA ZA MFUKO HUO
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MFUKO Wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF) umeendelea kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko huo ili kupata huduma za afya bila changamoto pindi wanapougua.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano mkuu wa klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DPCP) Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bi. Anjela Mziray amesema kuwa fursa ni kwa makundi ya watu wote na hiyo ni kulingana na vifurushi vilivyoainishwa na mfuko huo.
Amesema kuwa katika utekelezaji kazi wa mfuko huo tangu ulipoanza wanamkumbuka sana Hayati Rais Benjamin Mkapa kwa kupigania uanzishwaji wa mfuko huo mwaka 2001.
Aidha amesema kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kuhabarisha umma kuhusiana na mfuko hasa kwa kupeleka tarifa muhimu kwa wananchi ili waweze kupata huduma bora za afya.
Kwa upande wake Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja wa NHIF Hipolite Lelo amesema kuwa mfuko huo ulianza rasmi Julai Mosi mwaka 2001 na ulianza kutoa huduma kwa watumishi wa Umma ila kufikia sasa kila mmoja ana nafasi ya kupata huduma kutoka katika mfuko huo kulingana na vifurushi vilivyoainishwa na mfuko huo.
Pia amewashauri waandishi wa habari kutumia fursa hiyo kwa kujiunga na utaratibu wa kupata huduma pamoja na kuto maoni mbalimbali na fafanuzi kutoka kwa wananchi ili kuleta mizania katika habari.
"Yeyote anayetaka kujiunga na kifurushi anaweza kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa njia ya mtandao kwa kutumia kitambulisho cha utaifa na kupata huduma kutoka katika mfuko huo kwa miezi 13" ameeleza Lelo.
Mwisho.
No comments: