KALEMANI AIPA RUNGU TANESCO KUWAKATIA UMEME WADAIWA SUGU

Veronica Simba – Kilimanjaro

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuanza kuwakatia umeme wateja wake wenye madeni sugu nchi nzima, ifikapo Agosti 31, mwaka huu.

Alitoa maelekezo hayo akiwa katika ziara ya kazi wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo pia aliwasha umeme katika taasisi za umma na makazi ya wananchi.

Alisema TANESCO inadai zaidi ya shilingi bilioni 300 kutoka kwa Mashirika hasa ya Umma, Halmashauri, Sekta ya Afya, Mambo ya Ndani, Maji, Ulinzi na nyingine nyingi.

“Natoa siku 14 kuanzia sasa kwa Taasisi zote zinazodaiwa zikiwemo za Umma, zilipe, zisipolipa tutakata umeme, tena bila huruma wala taarifa nyingine yoyote. Taarifa ndiyo hii,” alisisitiza.

Akielezea sababu za kufikia uamuzi huo, Waziri Kalemani alisema Shirika hilo linajiendesha kibiashara pasipo kupata ruzuku serikalini, hivyo malimbikizo ya madeni ya wateja yanahatarisha uhai wake.

Alieleza baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Shirika hilo kwa kutumia fedha za ndani kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kupeleka gridi ya Taifa mkoani Kigoma pamoja na kusambaza miundombinu mingine katika vijiji na mitaa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Kwahiyo ni lazima tuwe na vyanzo vya uhakika vya ndani ambavyo pamoja na mambo mengine, ni kwa wateja wetu kutulipa kwa wakati.”

Aidha, Dkt Kalemani alitahadharisha kuwa wakati wa utekelezaji wa suala hilo, asipigiwe simu na wadaiwa zenye mlengo wa kumsihi kusitisha kutokana na sababu ambayo hutolewa na wengi kuwa taasisi zao ni muhimu hivyo zisikatiwe umeme. Alisisitiza kuwa badala ya kupiga simu, wadaiwa walipe ankara zao.

Katika hatua nyingine, akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Waziri alimweleza kuwa Mkoa huo una umeme mwingi ikilinganishwa na mahitaji yake.

Alisema kuwa Mkoa una zaidi ya megawati 110 za umeme wakati matumizi yake ni megawati 45 hadi 48, hali inayoufanya kuwa na ziada kubwa kuliko mahitaji.

Aidha, alieleza kuwa kwa sasa Serikali kupitia Wizara yake, inafuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayoendelea, ambayo ni REA II na REA III.

Alisema ameunda kikosi kazi maalumu kinachojumuisha wataalamu kutoka wizarani, TANESCO Makao Makuu na REA Makao Makuu, kitakachowajibika kuhakikisha Miradi hiyo ya umeme inakamilika ifikapo Septemba 15, 2020.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara lakini akaomba kusimikwa kwa nguzo za umeme zilizo imara zaidi, hususan katika maeneo ya milima ambako kuna upepo mkali, ili ziweze kuhimili hali hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu, alisema Wilaya yake ina deni kwa Rais John Magufuli ambalo inawiwa kulilipa kutokana na kuwajali wananchi hao kwa kuendelea kuwapigania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo umeme.

Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga pamoja na Wataalamu wengine mbalimbali kutoka Wizarani na katika Taasisi hizo.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akiwapa uhakika akina mama wa kijiji cha Ngumbilu, wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, kuwa umeme utakuwa umewashwa katika eneo hilo kabla ya Septemba 15, 2020. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Agosti 17, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, wakipita kukagua miundombinu ya umeme katika kijiji cha Ngumbilu, wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wanafunzi, walimu na wakazi jirani wa Shule ya Sekondari Esinyari iliyoko Kata ya Olkolili, wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kuwasha rasmi umeme katika Shule hiyo, Agosti 17, 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira (katikati), akimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, aliyekuwa akimweleza dhamira ya ziara yake mkoani humo, Agosti 17, 2020.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akitoa hamasa kwa wananchi wa Kitongoji cha Lasawana, kijiji cha Lokili, Kata ya Kashashi, wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, waige mfano wa Mzee Abrahamu Kileo (mwenye kofia ya njano), kwa kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe umeme. Waziri aliwasha rasmi umeme katika nyumba ya Mzee huyo akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 17, 2020.

 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt Tito Mwinuka (kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, wakiwa katika ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Kata ya Olkolili, wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu (kushoto), akimwomba Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, kufikisha salamu za pongezi na shukrani kutoka kwa wananchi wa Wilaya hiyo kutokana na jitihada zake kuwapelekea maendeleo ikiwemo umeme. Waziri aliwasha rasmi umeme katika Kitongoji cha Lasawana, kijiji cha Lokili, Kata ya Kashashi, wilayani humo akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 17, 2020.

No comments: