CHANGAMOTO YA MAJI JIJINI DAR YAELEKEA UKINGONI


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge (Kushoto) akifafanua jambo mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa maji wa Changanyikeni, Bagamoyo na kueleza kuwa huduma ya maji ni muhimu kwa kila mwananchi na ameielekeza Mamlaka ya maji jijini humo kuendelea kusambaza huduma hiyo, katikati ni Afisa Mtendaji mkuu wa DAWASA Mhandisi. Cyprian Luhemeja, leo jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Ishmmael Kakwezi kutoka DAWASA (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge (kulia) kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa maji wa  Pugu, Gongolamboto mradi unaotegemewa kukamilika Oktoba mwaka huu, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge, leo jijini Dar es Salaam.
  

    Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge (kushoto) akitazama namna ujenzi wa mradi wa maji wa Changanyikeni, Bagamoyo unavyotekelezwa na namna utakavyowanufaisha wakazi wa maeneo mbalimbali ikiwemo Goba Kinzudi na Changanyikeni jijini humo na unatarajiwa kukamilika baada ya mwaka mmoja na nusu, leo jijini Dar  es Salaam.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MAMLAKA Ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) imeendeleza jitihada zake za kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila mwananchi jijini humo kwa kupeleka huduma hizo katika maeneo mengi zaidi jijini humo ikiwemo Goba Kinzudi, Kigamboni hadi Bagamoyo ambapo hadi sasa miradi hiyo inaendelea kutekelezwa katika maeneo hayo ambayo hayakufikiwa na huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua miradi mikubwa mitatu ya maji inayotekelezwa jijini  humo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge amesema kuwa  huduma za maji, barabara na umeme ni muhimu sana kwa wananchi na amewataka viongozi kushirikiana na wakuu wa Wilaya katika Kuhakikisha wananchi wanapata taarifa juu ya miradi inayoendelea ili washiriki katika kuilinda miradi na kujibu changamoto wanazokumbana nazo.

Akizungumzia mradi wa maji wa Kisarawe II (visima vya Kimbiji na Mpera) Kunenge amesema mradi huo umegharimu shilingi bilioni 30 fedha zilizotokana na makusanyo na bili za maji na utakua na tanki la maji lenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 15 kwa siku na wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani watanufaika na mradi huo uliokamilika kwa asilimia 30 na unategemewa kukamilika mwezi Aprili mwakani.

Pia baada ya kukagua mradi wa maji wa Pugu, Gongolamboto, mradi ambao Rais Dkt. John Magufuli aliagiza ukamilike kwa wakati, Kunenge amesema kuwa mradi huo utakamilika mwezi Oktoba badala ya Desemba mwaka huu na utagharimu shilingi bilioni 6.9 fedha zilizotokana na makusanyo ya ndani na bili kutoka DAWASA,  na wakazi wa Temeke, Pugu Station, Temeke, Kivule, Kisarawe, Chuo Cha Kampala, Mongo la ndege, Mombasa na maeneo yote ya kusini yatanufaika na huduma ya maji.

Aidha katika mradi wa maji wa Changanyikeni Bagamoyo, Kunenge amesema kuwa mradi huo wenye gharama ya shilingi bilioni 65 kutoka benki ya dunia utakamilika baada ya mwaka mmoja na nusu na bomba la usambazaji wa maji litalazwa kilomita 1700 ili kuwafikia wananchi.

Mradi huo wa Changanyikeni, Bagamoyo utawanufaisha na kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa Changanyikeni, Salasala, Goba Kinzudi, Tegeta, Wazo, Makongo, Mabwepande hadi Bagamoyo.

Kunenge amewataka wananchi kulipa bili kwa wakati ili kuiwezesha Mamlaka hiyo kutekeleza miradi mingi zaidi na ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) kudhibiti upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa (DAWASA) Mhandisi. Cyprian Luhemeja amesema kuwa Mamlaka hiyo ina mipango mikubwa ya Kuhakikisha kila mkazi wa Dar es Salaam anafikiwa na huduma muhimu ya Maji.

" Wakati miradi inaendelea  tunaendelea kuwaunganisha wateja  ili miradi ikikamilika wateja wapate huduma hiyo kwa haraka na wakati hivyo wateja wenye uhitaji wa huduma hii watembelee ofisi zetu wakiwa na viambata muhimu zikiwemo barua toka watendaji ili wanufaike na huduma hii" amesema Luhemeja.

Vilevile amesema kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya maji.

No comments: