BONANZA LA MNYALU TANZANITE COMPLEX LAFANA
Timu ya Mirerani veterani ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ikifanya mazoezi ya kupasha misuli moto kabla ya kuingia kwenye michuano ya bonanza katika uwanja wa Tanzanite Complex.
BONANZA la soka lililoshirikisha timu nne za maveterani wa Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro limefana baada ya kufanyika kwenye uwanja wa Tanzanite Complex Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
Mmiliki wa Tanzanite Complex, Charles Mnyalu akizungumza kwenye bonanza hilo amesema limefana baada ya kushirikisha timu za maveterani kutoka mikoa mitatu.
Mnyalu amezitaja timu zilizoshiriki michuano hiyo ya bonanza ni Mirerani veterani, Hai veterani na Kia veterani za mkoani Kilimanjaro na wafanyakazi wa nishati ya umeme, Tanesco veterani ya mkoani Arusha.
Amesema katika michuano hiyo timu ya Hai Veterani ya Kilimanjaro iliibuka mabingwa wa bonanza hiyo baada ya kupata pointi tano kwa kushinda mchezo mmoja na kutoka suluhu michezo miwili.
Amesema timu ya Mirerani veterani imeshika nafasi ya pili kwa kupata pointi tatu kwani ilitoka sare baada ya kucheza na timu tatu.
Katika bonanza hilo lililohudhuriwa na umati wa wanamichezo wa Mirerani, Mnyalu amesema lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuboresha ushirikiano na kuongeza hamasa ya soka.
"Hamasa ya tamasha ni kubwa kwani watu wamejitokeza kwa wingi kupata burudani na kudhihirisha mapenzi makubwa ya soka yaliyopo Mirerani," amesema Mnyalu.
Mmiliki wa Jatong' Grand Hotel, Samuel Ogoye Nyamaroko (Tajiri mtoto) amesema bonanza lilikuwa zuri kwani watu wamepata burudani japokuwa timu yao ya Mirerani veterani haikushinda ubingwa.
"Tumecheza michezo mitatu kwa kutoka sare tatizo letu lilikuwa umaliziaji mbovu ila bonanza lilikuwa zuri watu wamepata burudani," amesema Nyamaroko.
Kocha wa timu ya Hai Veterani, Shabani Isango ambao ni mabingwa wa bonanza hilo kwa mwaka 2020 amesema siri ya ushindi wao ni mazoezi kwani mchezo kwao ni burudani.
"Pamoja na kushinda lakini watu wamepata burudani na nimpongeze Mnyalu kwa kuandaa bonanza hili kwani badala ya vijana kwenda katika mambo mabaya ya kuvuta bangi, kukaba au kuiba, wamepata burudani," amesema.
Katika bonanza hilo waamuzi wasaidizi chipukizi wa mji mdogo wa Mirerani Msafiri Chama na Martin Chama walikuwa kivutio kwa namna walivyochezesha kwa umahiri mkubwa.
No comments: