Benki Ya Crdb Yazindua Tawi La Kisasa Linalotembea Wilayani Mlele, Katavi

Benki ya CRDB imeendelea na jitihada za kupanua wigo wake wa kuwahudumia wateja na kufikisha huduma za benki hiyo kwa Watanzania walio wengi kwa kuzindua tawi jipya na la kisasa linalotembea "Mobile branch" katika wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mh. Juma Zubier Homea ameipongeza Benki ya CRDB kwa uzinduzi wa tawi hilo linalotembea katika wilaya ya Mlele huku akisema tawi hilo litasaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo na wilaya za jirani.

Mkuu wa mkoa huyo alisema wilaya hiyo ya Mlele ni moja ya kiungo muhimu cha uchumi katika mkoa huo wa Katavi, hivyo uwepo wa tawi hilo utasidia upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongeza fursa nyingi za maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Katavi.

"Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuendelea kuonyesha uzalendo wenu kwa kubuni njia mbalimbali za kufikisha huduma kwa Watanzania, tawi hili litakwenda kuwa kichocheo kwa maendeleo ya wana mlele na Katavi kwa ujumla," alisema Mh. Homea huku akibainisha tawi hilo linalotembea linaonyesha ubunifu wa hali ya juu na kuyataka mabenki mengine yaweze kuiga mfano wa Benki ya CRDB kwa kutumia njia mbadala kufikisha huduma kwa wateja.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Juma Zuberi Homera akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi linalotembea “Mobile Branch 19” la Benki ya CRDB katika mji wa Majimoto wilayani Mlele Mkoani Katavi. Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Benki ya CRDB, Bw.Denis Mwoleka, Kulia wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Rachel Kassanda, na Kulia wa pili ni Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Mahusiano, Emmanuel Kiondo. Uzinduzi huo uliambatana Benki ya CRDB kukabidhi msaada wa pikipiki 7 zenye thamani ya Milioni 17.5 kwa vyama vya ushirika vya wilaya za Mkoa wa Katavi

Homela aliwataka wananchi wa Mlele na Vitongoji vyake sasa kuchangamkia fursa mbalimbali zitolewazo na Benki ya CRDB katika kukuza uchimi na uzalishaji kwa mtu mmojamoja na hata vikundi kwa ujumla. Hasa katika kujipatia mikopo nafuu itolewayo na benki hiyo katika kuinua shughuli za kilimo, biashara na ufugaji.

Katika uzinduzi huo Benki ya CRDB pia ili mkabidhi mkuu wa mkoa wa Katavi msaada wa pikipiki 7 zenye thamani ya shilingi milioni 17.5 kwa ajili ya kusaidia shughuli za vyama vya ushirika katika wilaya za Mkoa wa Katavi. Msaada huo ni sehemu ya sera ya Benki ya CRDB ya kusaidia jamii (CSR Policy) inayoelekeza matumizi ya asilimia 1% ya faida ya Benki kila mwaka katika kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki hiyo, Tully Mwambapa, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Mahusiano wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo alisema uzinduzi wa tawi hilo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo katika kusaidia jitihada za serikali ya awamu ya tano ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kurahisisha ufanikishaji wa miamala ya kifedha kwa wananchi mmoja mmoja na biashara.

Kiondo alisema uzinduzi huo wa tawi hilo linalotembea unaenda sambamba na utoaji huduma kupitia njia mbalimbali mbadala za kidijitali ili kuongeza urahisi na unafuu wa upatikanaji wa huduma kwa wateja. Huduma hizo ni pamoja na CRDB Wakala, SimBanking, SimAccount, na huduma kupitia mtandao 'Internet Banking'.

“Njia hizi za kidijitali za utoaji huduma zinamuwezesha mteja kufanya miamala yake yote popote pale alipo na wakati wote masaa 24” alisisitiza Kiondo huku akibainisha kuwa benki katika mkoa wa Katavi benki hiyo pia inatoa huduma kupitia CRDB Wakala zaidi ya 60.

Akizungumza juu ya huduma zinazotolewa na tawi hilo linalotembea, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Benki ya CRDB, Denis Mwoleka alisema wateja watapata huduma zote kuanzia kufungua akaunti, kuweka fedha, huduma za fedha za kigeni, pamoja na maombi ya mikopo.

Mwoleka alibainisha kuwa tawi hilo litakuwa likitoa huduma kwa siku 6 za wiki kuanzia jumatatu mpaka jumamosi huku huduma za ATM zikipatikana siku zote za wiki masaa 24.

Benki ya CRDB inaongoza nchini kwa kuwa na mtandao mpana wa matawi zaidi ya 260, CRDB Wakala zaidi ya 15,000, ATM zaidi ya 550, mashine za manunuzi (PoS) zaidi ya 1,500. Benki hiyo pia inatoa huduma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.


No comments: