UHAKIKI WA KAYA MASIKINI MPANGO WA TASAF KIPINDI CHA KWANZA AWAMU YA TATU


Zoezi la uhakiki wa kaya zilizopo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) kipindi cha kwanza awamu ya tatu limefanyika wilayani Busega huku kukiwa na muitikio mkubwa wa walengwa hivyo kuwezesha zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi mkubwa. Zoezi hilo lililokuwa la siku tatu limeweza kufanyika kwa mafanikio makubwa huku kaya 3155 zikihakikiwa kati ya kaya 3826 zilizokusudiwa, huku baadhi ya kaya zikiwa zimehama makazi yao hivyo kukosa sifa ya kaya lengwa.

Nuru Mkomambo, mwakilishi wa Mkurugenzi wa TASAF Taifa, alisisitiza ushirikiano wa viongozi kwa ngazi mbalimbali ni moja ya njia sahihi ya kufanikisha zoezi hilo la uhakiki wa kaya masikini. Aidha aliongeza kwa kuwataka wawezeshaji kuwa na uadilifu katika zoezi hilo ili kutimiza lengo la zoezi.

Uhakiki umefanyika katika vijiji 41 kati ya 59 vilivyopo kwenye mpango wa TASAF kipindi cha kwanza awamu ya tatu. Mpango wa TASAF ni miongoni mwa dhima kubwa na kipaumbele cha kupunguza umasikini kwa kaya masikini nchini Tanzania, huku kaya lengwa zikiwa na matumanini makubwa katika mpango huu.

Kufanyika kwa uhakiki huo kuna kuna dhima ya kujua uhai wa kaya lengwa kwaajili ya kutekeleza kipindi cha pili awamu ya tatu. Mpango wa TASAF ni chachu kubwa ya kuboresha maisha ya kaya na mtu binafsi huku kaya zikijikita kwenye shughuli za maendeleo ikiwemo ufugaji, biashara ndogondogo, kusomesha watoto na shughuli za kilimo. Baadhi ya walengwa wamekiri kwamba mpango huu wa TASAF ni mkombozi kwao kwakua umefanya maisha ya kaya nyingi kuinuka kiuchumi kwa kujishughulisha na ujasirilimali.

Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Mussa Mbyana akifungua mafunzo kwaajili ya uhakiki kwa wawezeshaji, aliwataka wawezeshaji wa zoezi hilo kuwa na maadili na ufanisi na hakutakuwa na mzaha kwa atakaye vuruga zoezi hilo kwani lengo la serikali hali ya umaskini nchini chini ya mpango wa TASAF.

Mratibu wa mpango wa TASAF wilaya ya Busega Bi. Wema Mmari amekiri kuwa kuna mwamko mkubwa kwa kaya lengwa katika zoezi la uhakiki. Kata zote 15 zilizopo wilayani Busega zimekuwa katika mpango wa TASAF kipindi cha kwanza awamu ya tatu. Jamii na kaya lengwa zimekuwa zikipata elimu ya kuhakikisha maisha yao yanaboreshwa kutoka katika utegemezi kwa kutumia fedha wanazopata kikamilifu kwa mambo yenye tija ya ushawishi wa maendeleo.

Kwa kuona umuhimu wa mpango wa TASAF, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Joseph Maguful, tarehe 17 Februari, 2020 alizindua TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu. Mpango ambao unatarajia kugharimu tirioni 2 za kitanzania kwaajili ya kutoa ruzuku kwa kaya masikini nchni.

No comments: