Benki ya Exim Yatangaza Ongezeko La Faida Licha Ya Changamoto Ya Corona
Benki ya Exim imepata ongezeko la faida (kabla ya kodi) kwa asilimia 35 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka kilichoisha mwezi Juni 30 mwaka huu, mafanikio yanayotajwa kuwa yametokana na ufanisi kiutendaji licha ya changamoto za kiuchumi kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam leo na Afisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo Bw. Shani Kinswaga imeonyesha kuwa benki hiyo imefanikiwa kupata faida ya sh. Billioni 6.58 katika robo ya pili ya mwaka huu ikilinganishwa na faida ya Sh. Bilioni 4.90 kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.
"Tunafurahi kuripoti matokeo mazuri kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020 licha ya athari kubwa ya janga la Covid-19 kwenye uchumi. Tumerejesha asilimia 8% kwenye mfuko wa wanahisa. Tunayachukulia mafanikio haya kama chachu ya kuendelea kufanya vizuri ili kutimiza malengo yetu na ya wateja wetu” alisema.
Aidha alibainisha kuwa benki hiyo imeshirikiana kikamilifu na na sekta zilizo athirika zaidi kiuchumi kutokana na janga la Covid-19 katika kuhakikisha sekta hizo zinajikwamua kwenye changamoto ya kifedha baada ya kuathirika na janga hilo.
Mnamo Juni 2020, benki ya Exim ilitoa msamaha wa zaidi ya TZS bilioni 160 kwa njia ya likizo ya malipo na upanuzi wa vipindi vya ulipaji wa mikopo ili kusaidia wateja wa benki hiyo ambao biashara zao zilizoathirika zaidi na athari za kiuchumi za Covid-19.
"Jumla kuu ya Mali zetu zote imebaki kuwa TZS 1.8 Trilioni, ikichangiwa hasa na ongezeko la 3% ya amana za wateja wetu katika kipindi hiki cha robo ya pili ya mwaka na hivyo kufanya jumla ya amana zote za wateja wetu kuwa TZS 1.33 Trilioni. Aidha, shughuli zetu nchini Tanzania, Comoros na Uganda zote zimerekodi ukuaji wa amana za wateja wakati wa robo hii "aliongeza.
Zaidi Bw Kinswaga alibainisha: "Benki imerekebisha mkakati wake wa muda wa kati (Medium Term Plan) kufuatia changamoto ya Covid-19 kwa lengo la kuendeleza kasi ya ukuaji. Mkakati huo unategemea 'Rasilimali watu, Mchakato (Processes) na Teknolojia' katika kukuza ukuaji endelevu. Matokeo ya robo hii ni ushahidi wa maendeleo yaliyofanywa. "
Katika kipindi hicho cha robo mwaka, Benki ya Exim ilizindua kampeni yake mpya ‘Maliza Kirahisi Kidigitali' inayolenga kuhamasisha wateja wa benki hiyo kutumia zaidi huduma za kiditali ili kurahisha upatikanaji wa huduma zinazotolewa na benki hiyo sambamba na kuokoa muda ambao wangeutumia kufuata huduma hizo kwenye matawi ya benki hiyo.
Kampeni hiyo ilikuja kipindi ambacho jamii inapitia mabadiliko kuelekea huduma za kidigitali hususani katika huduma za kifedha na manunuzi, hali iliyochochewa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa virus vya Corona (COVID 19).
Aidha katika kutekeleza Mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaofahamika kwa jina "Exim Cares", benki hiyo ilikabidhi msaada ya vyakula na vifaa kinga dhidi ya maambukuzi ya Virus vya Corona kwa vituo vinne vya kulelea yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara na Tanga.
Afisa Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim Bw. Shani Kinswaga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya utendaji wa kifedha wa benki hiyo katika robo ya pili ya mwaka 2020 ambapo pamoja na mambo mengine taarifa hiyo inaonyesha faida ya benki hiyo (kabla ya kodi) imekua kwa asilimia 35 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Wengine ni pamoja na Naibu Afisa Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim Bw Issa Hamis (Kulia) pamoja na Mkuu wa Hazina na Masoko ya Fedha wa benki hiyo Bw Arafat Haji.
Mkuu wa Hazina na Masoko ya Fedha wa benki ya Exim Bw Arafat Haji (Kushoto) akizungumza kwenye hafla hiyo. Kulia ni Afisa Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim Bw. Shani Kinswaga.
No comments: