WANANCHI SIMANJIRO KUNUFAIKA NA HOSPITALI MPYA YA WILAYA

MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula amezindua hospitali ya Wilaya hiyo hivyo waliokuwa wakisafiri umbali wa zaidi ya kilomita 180 hadi 200 kufuata huduma hiyo jijini Arusha au Mkoani Kilimanjaro wataondokana na adha hiyo. 

Mhandisi Chaula akizungumza jana wakati akizindua hospitali hiyo alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi huo uliogharimu shilingi bilioni 1.8 zilizotumika hadi sasa. 

Alisema tangu wilaya hiyo ianzishwe mwaka 1994 haikuwa na hospitali ya wilaya ila hivi sasa Rais Magufuli alitoa fedha hizo na kujengwa kati ya hospitali mpya 67 zilizojengwa nchini na nyingine 27 za awamu ya pili.

Aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Nadosoito kata ya Langai kwa kutoa ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo mpya ya wilaya. 

"Kipekee nimpongeze mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hii Yefred Myenzi kwa usimamizi wake mzuri hadi kukamilika kwa hospitali hii ambayo leo (jana) ninazindua," alisema Chaula. 

Alisema awali baadhi ya wananchi wa kijiji hicho hawakutaka kutoa eneo hilo wakidai kuwa diwani wao Jackson Sipitieck ameuza kwa serikali jambo ambalo siyo kweli kwani serikali imelichukua bila kulipia. 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi alisema majengo saba ya hospitali hiyo yamekamilika kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wao. 

Myenzi alisema hospitali hiyo ina majengo ya utawala, wodi ya wazazi, wagonjwa wa nje, famasi, la kufulia, mionzi na maabara. 

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Jackson Sipitieck alisema baraza la madiwani lilipitisha azimio la kila kata kuchangia shilingi milioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari. 

Sipitieck alisema wananchi wa kijiji cha Narosoito kata ya Langai wameibeba wilaya hiyo kwa kutoa eneo hilo na kujengwa hospitali hiyo itakayowanufaisha kizazi cha sasa na kijacho. 

Mkazi wa eneo hilo Martha Okida alimshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi huo kwani waathirika wakubwa wa ukosefu wa hospitali ya wilaya walikuwa wanawake na watoto. 

Okida alisema hivi sasa hakuna haja ya kusafirishwa wagonjwa kwani huduma za hospitali ya Wilaya zitakuwa zinapatikana hapo tofauti na awali. 
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula akipima afya yake wakati wa uzinduzi wa huduma ya hospitali mpya ya wilaya hiyo iliyopo Kata ya Langai.

No comments: