VIONGOZI WA TANCDA WAMPONGEZA WAZIRI WA AFYA KUKEMEA MATUMIZI YA TUMBAKU KWA KUWA NI HATARI
Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
VIONGOZI wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA)limeamua kutoa pongezi kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa hatua yake ya kukemea matumizi ya tumbaku kwa kuwa ni hatari kwa afya.
Kwa mujibu wa TANCDA ni kwamba tamko la Waziri Ummy Mwalimu linaonesha namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyojali afya za Watanzania, lakini pia kulinda maslahi ya kiuchumi na kijamii.Waziri wakati akizindua Ripoti ya Utafiti wa Matumizi ya Tumbaku kwa watu wazima ya mwaka 2018 nchini, mjini Dodoma Juni 4, ndipo alitumia nafasi hiyo kutoa onyo hilo.
Wakati anatoa anazindua ripoto hiyo Waziri Ummy alisema Tanzania kama ilivyo nchi nyingine za Afrika watumiaji wa tumbaku wapo hatarini kupata magonjwa yasiyoambukiza na hata kuyumba kuchumi.
Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Meneja Mradi wa TANCDA Happy Nchimbi amesema kuwa wanampongeza Waziri Ummy pamoja na Serikali kwa ujumla inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kujali afya za Watanzania kwa kuzingatia madhara yanayotokana na matumizi ya tumbaku nchini.
Amesema kuwa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza limetoa machapisho mbalimbali ya kuelimisha jamii kuhusu athari za kiafya zinazosababishwa na matumizi ya tumbaku. Kwa ujumla ni kwamba moshi wa tumbaku unamadhara kwa watumiaji na hata watu waliokaribu na mvutaji ambao watafikiwa na moshi huo.
"Moshi wa tumbaku una kemikali zaidi ya 400 na kati ya hizo 250 zinajulikana kuwa ni hatari. Kati ya hizo 50 husababisha ugonjwa wa saratani," amesema katika taarifa hiyo na kuongeza "Wanaotumia tumbaku na hata wanaofikiwa na moshi wa wavutaji wako hatarini kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kifua sugu, saratani ya mapafu, koo, kizazi, mifupa na ngozi."
Hata hivyo TANCDA imesema tafiti mbalimbali zinaonyesha matumizi ya tumbaku kwa wajawazito yanaweza kusababisha mimba kuhaharibika au mtoto kuzaliwa na uzito pungufu, kutokuwa vizuri, vifo vya ghafla pamoja na magonjwa ya mapafu na njia za hewa.
"Madhara mengine ya matumizi ya tumbaku kuwa ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, vidonda vya tumbo, meno kuoza na kupungua nguvu za kiume,"amesema Nchimbi kupitia taarifa hiyo.
Ilifafanua kwamba nusu ya watumia tumbaku kwa muda mrefu hufa kutokana na madhara yake, huku nusu ya vifo hivyo vikiwakuta watu walio chini ya miaka 70.
Pia Shirikisho hilo limeleeza vifo hivyo vya mapema, huziacha familia, hasa watoto, katika hali mbaya kiuchumi na kushindwa kumudu gharama maisha ikiwamo za afya, chakula, mavazi, malazi na elimu.
"Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa hivi karibuni inaonesha kuwa Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu wa COVID 19 huwaathiri zaidi watu wanaotumia tumbaku.WHO imesema wanaotumia tumbaku mapafu yao huwa dhaifu hivyo wakipata ugonjwa wa COVID19 huathirika kwa kiwango kikubwa na kuwa rahisi kupatwa na shida ya upumuaji.
"TANCDA imewashauri watu wasiotumia tumbaku kutoijaribu na watumiaji kupata msaada wa kuacha ili kulinda afya zao, hasa watoto. Tuanawashauri wanaovuta kutoitumia ndani ya nyumba, karibu na watu hasa watoto ambao mapafu yao bado yanakua kuepuka kuwaathiri,"ameeleza Nchimbi kwenye taarifa hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
No comments: