MAMBO YAMEIVA CCM...WANAOTAKA KUGOMBEA URAIS WAPEWA RATIBA YA KUCHUKUA NA KUREJESHA FOMU

Na Said Mwishehe, Michuzi TV.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimetengaza rasmi ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tekiti cha Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25,2020.

Akitangaza ratiba hiyo leo Juni 12,2020 jijini Dar es Salaa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Humphrey Polepole amesema ratiba ya kumpata mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaanza Juni 15 mpaka Juni 30 mwaka huu wagombea kuchukua fomu na kurejesha fomu.Mwisho wa kurejesha fomu itakuwa Juni 30,2020 ,saa 10 kamili jioni.

"Tukio la pili itakuwa ni kati ya Juni 15 hadi Juni 30 mwaka huu, mgombe wa CCM atakuwa na kazi ya kutafuta wadhamini mikoani na kisha kuirejesha ndani ya muda huo ambao umetangazwa.

"Hatua itakayofuata itakuwa ni uchujaji wa majina ya wagombea ambapo Julai 6 hadi Julai saba mwaka huu, kitaketi kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama chetu kuanzisha mchakato wa uchujaji, lakini Julai 8 mwaka huu kitaketi kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa .
 
Julai 9 kitaketi kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho kitafiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu majina ya wanachama wasiozidi watano wanaomba kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"amesema Polepole.

Ameongeza Julai 10,2020 kitaketi kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho na chenyewe kitakuwa na kazi ya kupendekeza kwa Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa majina matatu ya wanachama wanaomba dhamana ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Na Julai 11 na Julai 12 mwaka huu utaketi Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambao na wenyewe utakuwa na kazi ya kuchagua jina moja la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa rais kwa tiketi ya rais wa Tanzania.

Kuhusu Zanzibar, Polepole amesema kuwa kuanzia Juni 15 mpaka Juni 30 mwaka huu ni kuchukua na kurejesha fomu na tarehe ya mwisho ya kurejesha ni Juni 30,2020 saa 10:00 jioni.

"Juni 15 mpaka Juni 30 mwaka huu itakuwa ni kipindi cha kutafuta wadhamini mikoani na baada ya hapo vitafuata vikao vya kuchuja majina ya wagombea .Julai 1 mpaka 2 vitaketi vikao vya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa kule Zanzibar.

"Julai 3 mwaka huu kitaketi kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama kule Zanzibar na Julai 4 mwaka huu kitaketi kikao cha Kamati Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambacho kitafikiria na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu kuhusu wanaomba nafasi ya Urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama chetu.

"Julai 9 mwaka huu kitaketi kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho kitafikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu majina wa wanachama yasizidi matatu wanaoomba kugombea kiti cha Urais Zanzibar,"amesema.

Ameongeza kuwa Julai 10 mwaka huu kitaketi kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho kitakuwa na kazi ya kuchagua jina moja la mwanachama ayatekasimama kugombea Urais Zanzibar.

"Julai 11 hadi Julai 12 utaketi Mkutano Mkuu wa CCM ambao utakuwa na kazi ya kuthibitisha jina la mwanachama atakeysimama katika nafasi ya Urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama hicho,"amesema Polepole.

No comments: