UJUMBE WA SADC KUELEKEA SIKU YA UELEWA KUHUSU UALBINO DUNIANI

 
Na Leandra Gabriel, Michuzi

JUMUIYA ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imeungana na wanajamii kote duniani katika maadhimisho ya siku ya uelewa kuhus watu wanaoishi na ualbino inayoadhimishwa kila Juni 13 na hiyo ni kufuatia maazimio ya mkutano mkuu wa 69 wa umoja wa mataifa ambao iliazimiwa ushiriki wa kila nchi mwanachama katika kulinda na kuhifadhi haki za watu wenye ualbino katika maisha, utu, ulinzi na nchi wanachama walishauriwa kutumia siku hiyo kwa kujenga uelewa kwa wananchi kuhusiana na haki za mtu mwenye ualbino pamoja na uelewa kwa ujumla.

kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na katibu mtendaji wa SADC, Stargomena Tax imeeleza kuwa kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni "Made to Shine" ambayo imechaguliwa katika kusherekea na kusimama pamoja na watu wenye ualbino kote duniani na kuhakikisha kuwa wanaishi huru bila unyanyasaji huku wakifurahi haki zao za msingi.

taarifa hiyo imeeleza kuwa katika maadhimisho hayo, nchi za SADC zimejizatiti katika kusimamia haki bila kuruhusu aina yoyote ya unyanyasaji kwa mtu mwenye ualbino kote duniani.

"Tunatambua kuwa watu wenye ualbino bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo unyanyasaji, upatikanaji hafifu wa huduma za afya na huduma za kielimu pamoja na ufinyu wa nafasi ushiriki katika shughuli za kijamii na siasa na hata kuuawa, kwa hali hiyo SADC inakemea, inalaani na itaendelea kukemea na kulaani aina yoyote ya unyanyasaji kwa watu wanaoishi na ualbino" imeeleza taarifa hiyo.

Pia katika taarifa hiyo Tax amezitaka nchi wanachama hasa serikali na mawaziri na asasi za kiraia kuwa na programu na mipango kwa azma ya kukemea kila aina ya unyanyasaji unaofanywa dhidi ya watu wanaoishi na ualbino duniani kwa kuhakikisha haki zao za msingi hazivunjwi.

pia imeelezwa kuwa SADC inafurahishwa na nguvu inayofanywa na kuoneshwa na watu wanaoishi na ualbino na wanaendelea kuwahimiza watu mashuhuri wanaoishi na ualbino kueleza safari zao za mafanikio ili kuleta chachu kwa wengine kwa kuwa wanaweza kusimamia haki zao na wakang'ara.

Rais  Dkt John Pombe Magufuli alipokutana na watoto wenye ulemavu wa ngozi wa kituo cha Mtakatifu William cha Jimbo Katoliki la Mbinga Mkoani Ruvuma katika moja ya ziara zake za kikazi hivi karibuni.Rais Magufuli aliwachangia shilingi Milioni 3 kwa ajili ya kununulia kofia na mahitaji mengine huku akitoa wito kwa Watanzania kujitolea kuwasaidia watu wenye ulemavu.

No comments: