KATIBU WA MUFTI ZANZIBAR AIFUNGA MADRASA KWA KUKITHIRI VITENDO VICHAFU.

Na Issa Mzee –Maelezo.

Ofisi ya Mufti Zanzibar imeifungia Madrasati Ridhwa Madihi-Rassuli iliyopo maeneo ya uwanja wa timu ya Taifa ya Jang’ombe kutokana na kukithiri vitendo vya udhalilishaji.

Uamuzi huo umechukuliwa na Ofisi ya Mufti kufuatia malalamiko ya baadhi ya wazazi kuharibiwa watoto wao na walimu wa Madrasa hiyo na wanafunzi kwa wanafunzi wenyewe.

Akitoa uamuzi huo Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema udhalilishaji huo unafanywa hata kinyume cha maumbile na hufanyiwa watoto wa kike na kiume.

Alisema katika mwaka 2011 Ofisi ya Mufti ilipokea malalamiko ya wanafunzi sita wa kiume kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na walimu wa Madrasa hiyo.

“Sisi kama ofisi ya mufti hatuwezi kuona walimu wa Madrsa wanaendesha vitendo vya aina hii, mwalimu ni mlezi ndio maana wazazi wanaleta watoto wao ili wawasimamie kielimu na kimaadili,” alisema Katibu wa Mufti Sheikh Khalid.

Sheikh Khalid alisema kabla ya kuchukua uamuzi wa kuifunga Madarasa hiyo, walifanya utafiti wa malalamiko ya wazazi na wananchi wanaokaa karibu na Madrasa hiyo ili kujua ukweli wa malalamiko hayo.

Alisema baada ya kujiridhisha kufanyika vitendo vya udhalilishaji katika Madrasa ya Ridhwa Madihi Rassul walifanya juhudi ya kuwaita walimu na kuwaonya waache vitendo hivyo lakini waliendelea kuvifanya.

Kufuatia kufungiwa Madrasa hiyo wazazi wenye wanafunzi wanaosoma katika madrasa hiyo wametakiwa kuwatafutia madrasa nyengine na walimu wote hawaruhusiwi kufundisha sehemu nyengine yoyote na wamefutiwa usajili.

Aidha aliongeza kuwa pamoja na kuifungia Madrsa hiyo na kufutiwa usajili, vyombo vinavyoshughulikia vitendo vya udhalilishaji ikiwemo Jeshi la Polisi vinaendelea kuzifuatilia kesi hizo.

Aliwakumbusha walimu wa madrasa zote nchini kuwa wao wamepewa dhamana ya kuwalea watoto na hakuna mzazi anaeridhika kuona mtoto wake anafanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na Madrasa hiyo walikiri kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji pamoja na kufanyika mabadiliko ya uongozi vitendo hivyo viliendelea kufanyika.

Walisema mara nyingi vitendo vya udhalilishaji vilikuwa vikifanyika hasa wakati walimu na wanafunzi wanaporudi kupiga dufu katika shughuli za arusi za usiku.
  Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume akiifunga Madrasa  ya Ridhwa Mad-hi Rasul iliopo Jangombe Zanzibar  kutokana na Walimu na Wanafunzi kukithiri  kwa  Vitendo Vichafu Visivyo na Maadili ya Dini .
 Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume akisisitiza Jambo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari na Wananchi baada ya kuifunga Madrasa  Ridhwa Mad-hi Rasul  iliopo Jangombe Zanzibar kutokana na Walimu na Wanafunzi kukithiri  kwa  Vitendo Vichafu Visivyo na Maadili ya Dini .
 Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume  akizungumza na Waandishi wa Habari na Wananchi mbalimbali baada ya kuifunga Madrasa  Ridhwa Mad-hi Rasul  iliopo Jangombe Zanzibar kutokana na Walimu na Wanafunzi kukithiri  kwa  Vitendo Vichafu Visivyo na Maadili ya Dini .
 Madrasa ya Ridhwa Mad-hi Rasul iliopo Jangombe Zanzibar iliofungwa na Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume kutokana na Walimu na Wanafunzi kukithiri  kwa  Vitendo Vichafu Visivyo na Maadili ya Dini .

No comments: