Serikali Yaipongeza Benki Ya Exim Kwa Kuwalinda Wateja Na Athari Za Covid 19

Serikali imeagiza benki na taasisi za fedha kutathmini kwa kina athari zinazotokana na mlipuko wa COVID-19 kwenye urejeshaji wa mikopo ya wateja wa taasisi hizo huku ikipongeza benki ya Exim Tanzania kwa kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo ili kusaidia wateja wa benki hiyo  ambao biashara zao zimeathiriwa zaidi  na janga hilo.
Akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2020/21 jijini Dodoma hivi karibuni , Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.     Philip Mpango mbali na kuipongeza benki hiyo alitoa wito kwa benki nyingine nchini kujadiliana na kukubaliana na wakopaji namna ya kurejesha mikopo na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo.
“Serikali kupitia Benki Kuu itatoa unafuu kwa benki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi na bila upendeleo. Katika hili, napenda kuzipongeza baadhi ya benki kama Exim ambazo tayari zimetangaza kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo ili kusaidia wateja wao katika sekta ambazo biashara zao zimeathiriwa na COVID-19 na naziomba benki nyingine zifuate mfano huo,’’ alisema
Katika kukabiliana na athari za janga hilo serikali ilichukua hatua kadhaa ili kunusuru uchumi ikiwemo kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5 hatua ambayo ililenga kuongeza wigo wa benki kukopa kutoka Benki Kuu kwa riba nafuu ili nazo ziwezi kupunguza riba ya mikopo kwa wateja.
Kauli hiyo ya Waziri Mpango imekuja siku chache kufuatia Benki ya Exim kutangaza msamaha wa likizo ya malipo ya mikopo kwa wateja wake wakubwa, wa kati na wadogo walipo katika sekta zilizo athirika zaidi kiuchumi kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa virus vya Corona (COVID 19).
Hatua hiyo ilitajwa kuwa ni  sehemu ya juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na benki hiyo katika kuwasaidia kifedha wateja wake waliopo sekta ambazo zimeathiriwa zaidi na athari za mlipuko wa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo hivi karibuni ilimnukuu Afisa Mtendaji Mkuu wa hiyo , Bw Jaffari Matundu  akibainisha kuwa msamaha huo wenye thamani ya zaidi ya sh Bilioni 160 ulianza mwezi Juni mwaka huu, ukihusisha likizo ya malipo ya mikopo kwa wateja na nyongeza ya muda wa urejeshaji wa mikopo  ili kusaidia wateja wa benki hiyo katika sekta mbali mbali kutokana na athari za janga hilo kwenye biashara zao.
"Benki inaelewa mahitaji ya wateja wetu wakati huu na tunafanya yote yanayowezekana kuwasaidia ili waweze kuvuka salama katika kipindi hiki kigumu. Jitihada hizi haziishii tu kwenye misamaha hii tunayoitoa bali pia kupitia huduma za ushauri kuhusu mikakati ya biashara ili kuhakikisha kwamba  biashara za wateja wetu zinadumu na zinafanyika kwa mafanikio zaidi,'' alisema.
Alisema msamaha huo unazingatia vigezo mbalimbali kwa kila mteja kwa kuwa athari za COVID-19 hazikuwa sawa katika sekta zote. "Tunafarijika kwa kuwa tayari wateja waliopo kwenye sekta zilizoathiriwa zaidi wameshaanza kusaidiwa. Mazungumzo na wateja wengine bado yanaendelea ili kutambua hatua mbali mbali zinazofaa kulingana na aina ya biashara, " aliongeza.
Akizungumzia uamuzi wa benki hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Bw Peter Kifunguomali alisema kuwa utasaidia wafanyabaishara wengi yakiwemo makampuni hususani yanayohusika  na sekta zilizoathirika zaidi ikiwemo sekta ya utalii kuweza kupata muda wa kutosha kujiimarisha tena kibiashara ili yaweze kupata nguvu ya kurejesha mikopo hiyo bila kutetereka.
“Ukweli ni kwamba athari za Corona zimeathiri kwa kiasi kikubwa  sekta muhimu na wafanyabiashara wengi kwasasa wanaumiza namna ya kujinausua na janga hili. Uamuzi uliofanywa na benki ya Exim unapaswa kufanywa na benki nyingine pia ili kunusuru wateja wao ambao kimsingi kwasasa wanahitaji msaada ambao naamini benki zinaweza kuwasaidia,’’ alisema.’’ Alisema.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.     Philip Mpango

No comments: