MAFUNZO YA UHAMASISHAJI NA WAELIMISHAJI WA MTANDAO WA WANAWAKE KATIKA JESHI LA MAGEREZA NCHINI YAFANYIKA MKOANI MOROGORO


Na Sajini Taji, Shani Mhando, Morogoro

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Bi.Mboni Mgaza amepongeza kuanzishwa  kwa mtandao wa wanawake katika Jeshi la Magereza nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya  mtandao wa wanawake katika Jeshi la Magereza jana Mkoani Morogoro, Bi Mboni amesema, hii ni hatua nzuri sana yakupongezwa kwa Jeshi hilo kwani itahakikisha wanawake  katika nyanja zote wanatumia fursa mbalimbali zilizopo na zitakazojitokeza ndani ya Jeshi hilo na nje ya Jeshi ili kujipatia mafanikio.

Ameongeza kuwa msingi wa kuwepo kwa mitandao ya wanawake nchini ni kuwawezesha na kuwajengea uwezo  wanawake katika nyanja za kiuchumi, mafunzo, ajira, uongozi na maamuzi ili kuweza kutimiza majukumu yao bila kubaguliwa jinsia zao.

“Ni matarajio yangu kuwa kuanzishwa kwa mtandao huu ndani ya Jeshi la magereza utazingatia miongozo na kanuni mbalimbali zilizotolewa na serikali kuhakikisha katika maeneo yote yenye changamoto za usawa wa kijinsia ili mwanamke awezeshwe na aweze kukabiliana nazo,” alisema Bi. Mboni.

Aidha Bi. Mboni amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia mambo yote watakayofundishwa katika mafunzo hayo ili wawe wawakilishi wazuri kwa askari wote wa kike katika Jeshi la Magereza hivyo kuwajengea uwezo, kukuza uelewa na kuwaunganisha ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Jukumu mlilopewa na Jeshi la Magereza la uelimishaji ni jukumu muhimu sana katika ustawi wa mtandao wa wanawake ndani ya Jeshi la Magereza,
 ninauhakika, mafunzo mtakayoyapata hapa yatawaongezea uwezo wa kutekeleza jukumu hili muhimu na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya mtando ndani ya Jeshi,” alisema Bi Mboni.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Bertha Minde amesema kuwa kuanzishwa kwa mtandao wa wanawake ndani ya Jeshi la Magereza kumewawezesha wanawake kushika nafasi za juu za uongozi katika Jeshi hilo huku akitolea mfano wa baadhi ya viongozi wanawake walioshika nafasi za juu akiwemo Kamishna(01), Kamshna Msaidizi Mwandamizi(01) na Makamishna Wasaidizi(06) ingawa bado kuna upungufu mkubwa wa kinamama katika nafasi za juu za uongozi.

Naye Msemaji wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Amina Kavirondo amemuomba Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo Bi. Mboni Mgaza kuendelea kuwaunga mkono katika mtandao wa wanawake katika Jeshi la Magereza ili kuwezesha kufikia malengo waliyokusudia

Mtandao wa wanawake katika Jeshi la Magereza ulianzishwa rasmi Desemba 7, 2018 baada ya Mkutano wa SADC uliofanyika Desemba, 2011 nchini Afrika ya Kusini ambapo katika kikao hicho wazo la mtandao wa wanawake lilirasimishwa na kuwekewa mikakati.
 Kongamano la siku mbili la Mtandao wa wanawake katika Jeshi Magereza (TPS WOMEN NETWORK) limefanyika Mkoani Morogoro kuanzia  Juni 22, 2020. #Pichani ni Wana Mtandao wanawake wa Jeshi hilo.

No comments: