FCS YATOA BARAKOA 5000 KWA CHAVITA
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KATIKA kuonesha ushiriki wa mapambano dhidi ya mlipuko wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid -19,) asasi ya kiraia ya Foundation for Civil Society (FCS) imeendelea kuonesha ushiriki huo kwa kutoa vifaa na ruzuku kwa makundi maalumu na watu wenye ulemavu ili kuendelea kuwaweka salama zaidi pamoja na kuzuia maambukizi zaidi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi barakoa 5000 kwa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkurugenzi Mtendaji wa FSC, Francis Kimwanga amesema FCS imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na wadau wa maendeleo hasa katika kupambana na ugonjwa wa mlipuko wa Covid-19.
"Tumefanya kazi na asasi za kiraia na kutoa ruzuku maalumu kwa ajili ya kupambana na Covid -19 na mashirika zaidia ya 39 yamefaidika na zaidi ya asilimia 20 ya rasilimali hizo zimewafikia watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo watu wenye ulemavu ambao walipatiwa vifaa maalumu vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo" ameeleza Kimwanga.
Aidha amesema kuwa wametoa barakoa 5000 kwa Chama cha Viziwi Tanzania ikiwa ni muendelezo wa kupambana na kuenea kwa virusi hivyo.
"Lengo ni moja kushirikiana na kuendelea kuchukua tahadhari zinazotolewa na Wizara ya afya na wataalamu huku tukizingatia matumizi sahihi ya barakoa pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka" amesema Kimwanga.
Kwa upande wake mwakilishi na mhasibu wa Chama cha Viziwi Tanzania Sospeter Makori, ameishukuru FCS kwa kuendelea kujali makundi maalumu hasa kwa kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Covid-19.
"Kwa niaba ya wenzangu wote tunawashukuru FCS kwa kuwa na mahusiano mema na ya muda mrefu na taasisi yetu, nawaomba muendelee kutushika mkono kwa kuendelea kutupatia mahitaji ya msingi sisi pamoja na makundi mengine yenye uhitaji" amesema Makori.
Aidha amesema kuwa barakoa hizo zitawafikia watu wenye matatizo ya kusikia jijini Dar es Salaam na hata mikoani.
"Nitasambaza barakoa hizi katika matawi yote ya viziwi nchi nzima ili ziwasaidie wahitaji katika kujikinga na maambukizi wa virusi vya Corona" ameeleza.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kimwanga (kulia) akikabidhi baadhi ya barakoa kwa mhasibu wa Chama cha Viziwi Tanzania Sospeter Makori (kushoto) ili ziweze kuwasaidia kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, leo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa makasha yaliyobeba barakoa 5000 zilizokabidhiwa na FCS kwa Chama cha Viziwi Tanzania ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Covid-19, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kimwanga akizungumza na wanahabari mara baada ya kukabidhi barakoa hizo ambapo amesisitiza ushirikiano na uchukuaji wa tahadhari ili kuweza kushinda vita hivyo, leo jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi na Mhasibu wa Chama cha Viziwi Tanzania Sospeter Makori akizungumza mara baada ya kukabidhiwa barakoa hizo na ameahidi kuzifikisha barakoa hizo kwa wahitaji jijini Dar es Salaam na mikoani, leo jijini Dar es Salaam.
No comments: