ZHANG YIMING, MGUNDUZI WA TikTok ILIYOLEGEZA LOCKDOWN


 
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

WAKATI dunia ikiendelea kupambana na mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19,) huku baadhi ya nchi zikiweka vizuizi hasa vya wananchi kutotoka nje, baadhi ya shughuli zimeendelea kufanyika ikiwemo burudani, wengi wameonekana kufurahia maisha kwa kushiriki na wenzao kupitia mtandao wa TikTok kwa kushiriki video mbalimbali hasa za vichekesho.

Zhang Yiming (37) kutoka nchini China ndiye aliyeanzisha mtandao huo kupitia kampuni yake ya Bytedance iliyoanza 2012 na hiyo ni baada yakuona matumizi ya kompyuta yanahamia katika simu.

Mtandao wa TikTok umekuwa maarufu sana kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambapo ndani ya mwezi mmoja watumiaji wapya zaidi ya milioni miatano hujiunga na TikTok, hali iliyopelekea ushindani mkubwa na mitandao mingine ikiwemo Facebook, Instagram na Snapchat.

Imeelezwa kuwa Zhang ni tajiri anayeshikilia nafasi ya tisa nchini China akiwa na fani ya uhandisi katika masuala ya kompyuta kutoka Chuo kikuu cha Nankai, na amefanya kazi katika kampuni za Microsoft na Kuxun kabla ya kuanzisha kampuni yake ya Bytedance.

TikTok ilianzishwa kwa malengo ya kutengeneza video fupi, zenye ubunifu pamoja na vichekesho na kwa mara ya kwanza ilizinduliwa kwa kuilenga China mwaka 2016 na mwaka uliofuata ikazinduliwa nje ya China huku mataifa ambayo TikTok imekuwa maarufu zaidi ni Marekani na barani Asia.

TikTok iliundwa kwa siku 200 na ndani ya mwaka mmoja ikapakuliwa na watumiaji wapatao milioni mia moja huku video zaidi ya bilioni moja zikitazamwa kila siku.

Imeelezwa kuwa kwa mwaka 2019 TikTok ilipakuliwa na watu wapatao bilioni moja.

Kwa mujibu wa Forbes Zhang ana utajiri wa dola za kimarekani bilioni 16.2 na hiyo ni kupitia TikTok ambayo inapatikana katika lugha 75 duniani na pia huwawesha watumiaji kurekodi video kwa sekunde sitini na kuwashirikisha watu wao wa karibu.

No comments: