WATANZANIA NAOMBA KUANZIA SASA CORONA AWE RAFIKI YETU...KWELI TENA , ASIWE ADUI TENA


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

CORONA mambo vipi? Natumai uko salama na unaendelea vema na majukumu yako ya kila siku hapa duniani tangu ulipokuja Desemba mwaka 2019.

Karibu Corona, karibu Duniani, karibu kila unapotaka kuingia. Ndio karibu Corona maana umekuja na malengo yako.

Malengo ya kuua maelfu ya binadamu. Sawa Corona maana ndicho unachoona kwetu sisi.

Dunia inalia tangu ulipokuja na kuanza kuua watu wasio na hatia. Umetutia majonzi makubwa sana,  tunalia kwa ajili yako, wengi wamepoteza ndugu, jamaa na marafiki kwa sababu ya wewe Corona.

Kuna wakati najiuliza kuhusu Corona kwamba ni Shetani au Jini? Nakosa jibu la moja kwa moja.

Sawa tunaambiwa na watalaam Corona ni virusi ambavyo hushambulia mfumo wa upumuaji na hivyo kusababisha aliyepatwa na virusi hivyo kushindwa kupumua na hatimaye hufariki dunia.

Kweli hadi sasa maelfu ya watu Duniani wamefariki. Corona uko kimya tu na unaendelea kutumaliza.

Hata hivyo nieleze tu wakati naendelea kuandika hiki ninachoandika bado hofu imetanda kila kona ya Dunia, bado vichwa vya Wataalam na Wabobezi wa masuala ya afya vinawaka moto. Nani wa kuleta utatuzi wa janga hili. Corona unachotufanyia ujue sio poa kabisa.Kuwa na huruma basi hata kidogo. CORONA why uko hivyo.

Ukweli tangu janga la Corona liiingie nchini kwetu Tanzania muda mwingi nimekuwa nikitakari sana kuhusu maisha ambayo tunayaishi hivi sasa.

Kuna wakati huwa namtazama mwanangu, na kisha najitazama mwenyewe, nawatazama ndugu, nawatazama jamaa zangu, nawatazama na marafiki zangu. Hivi usalama wetu uko wapi, Mwenyezi Mungu tunaomba tulinde na kutunusuru dhidi ya Corona.

Corona nikwambie ukweli tunakuchukia sana. Wewe ni adui yetu kwa sasa, umeanzisha vita na ulimwengu. Sawa tu iko siku tutashinda vita dhidi yako ,hata kama kwa sasa unajiona wewe ndio mshindi.

Hata hivyo maneno ya wahenga yananijia hakuna marefu yasiyo na ncha.Utafika wakati utamalizika.Uwepo wako umesababisha hata ndugu hawazikani kama zamani, watu wanashindwa kukaa vijiweni kupiga soga kama zamani.Umesababisha watu kushindwa kwenda nyumba za ibada.

Nchi nyingi duniani zimetoa maelekezo kwa waumini wa dini zote kuwa kutokana na Corona basi wafanyie Ibada nyumbani.Kweli Corona wewe wa kutaka kutuweka kando na Muumba wetu . Unatukosea sana Corona.Ujue umekuja Duniani umetukuta na dini zetu tuachie tuendelee kufanya Ibada kama zamani

Corona umesababisha nchi nyingi Duniani watu wake kukaa ndani kwa ajili ya kukwepa virusi.Watu hawatakiwi kutoka nje kabisa. Kuna nchi vyombo vya ulinzi na usalama ndio vimepewa jukumu la kuhakikisha hakuna anayetoka nje ,kisa Corona.

Binafsi namshukuru Mungu sana kunifanya niwe Mtanzania, ahsante Mungu kwa kunifanya nizaliwe Tanzania.Naona raha yake, ndio nchi pekee kwa Afrika Mashariki na hata katika Afrika ambayo imesema hakuna kufungia watu ndani.

Ndio nchi ambayo imewataka watu wake kuendelea kufanya Ibada tena kwa kuzidisha maombi kwa Mungu ili atunusuru na gonjwa la Covid-19.

Ni Tanzania tu ndio wenye uthubutu na uthubutu huo umetokana na maamuzi magumu lakini yenye busara kubwa ndani yake kutoka kwa Rais Dk.John Magufuli.

Aliona mbali na hivyo akasema Watanzania lazima waendelee na shughuli zao za kila siku.Akasisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kukabiliana na Corona.Akawataka watu wake kutokuwa na hofu kwani hofu ni hatari zaidi kuliko Corona . Ahsante Rais.Umekuwa Rais wa mfano.

Ukweli nchi nyingi za Afrika zenyewe katika kukabiliana na Corona walichofanya Ni kuiga kila kitu kutoka nchi za Ulaya na Amerika. Eti wamefungia watu ndani.Sasa sijui wanaenda mwezi wa pili huu watu wako ndani.

Wanatamani kuruhusu watu watoke nje lakini wanawaza wakubwa (mataifa makubwa) wasemaje.Kwa Tanzania Rais tangu mwanzo kabisa alijiuliza maswali ya msingi na kwa maslahi mapana kwa watu wake.Akaona hakuna sababu ya kufungia watu ndani.Ahsante Rais.

Mungu alikuwa na sababu ya kumfanya Rais Magufuli kuwa Rais kwa nyakati hizi zenye changamoto nyingi.Kuna wakati najiuliza hivi kwenye Corona hii halafu hatuna kiongozi wa nchi mwenye uthubutu sijui ingekuaje,Nadhan muda huu tungekuwa na sisi tuko ndani.

Najua wapo wengi wakiwemo baadhi ya Watanzania wanapambana kuhakikisha eti Rais atangaze watu wafungiwe ndani.Nadhani watu hao wana malengo yao binafsi sio kwa ajili ya Watanzania.

Kuna mijitu mingine huko mtandaoni kazi yao Ni kutengeneza hofu kwa Watanzania kuhusu Corona.Wamekuwa wakipotosha na kutisha watu.Ndio hao wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kuhusu idadi ya wagonjwa na idadi ya vifo.Ni kama vile wametumwa kuichafua Tanzania kwa kutumia ugonjwa Covid-19.

Wamekuwa na roho za shetani,Ni watu wa hovyo sana na kwa bahati mbaya wapo wanaowaaamini.Kuna wakati huwa najiuliza hivi Watanzania walio wengi wana shida gani? Hivi kwanini ukubali kushikiwa akili kwenye kila Jambo?

Yaani hata kwenye matukio ya majanga nako unashikiwa akili.Sasa akili zako zinafanya kazi wakati gani.Tumekuwa wa ajabu kwani kushikiwa akili limesababisha kuibuka tabia ya kupinga kila ambacho Serikali inaeleza na hasa kwenye takwimu.Kila Serikali ya Tanzania inavyoweka uwazi na usahihi wa takwimu za kesi za Corona bado watu wanaenda mitandaoni na kuaminishana ujinga.

Waziri Mkuu na hata Rais Magufuli wameomba Watanzania kupuuza habari zinazoandikwa mtandaoni kuhusu Corona na taarifa zote sahihi ni zile za Serikali kupitia wasemaji rasmi.

Baada ya kueleza hayo kwa kirefu sasa kuna jambo nimefikiria kuhusu Corona na nadhani ndio sahihi.Naomba tuelewane vizuri, sikiliza na Soma kwa makini.Ni hivi Corona ndiyo tunayo tayari Duniani na hatujui itakwisha lini. Ni lazima sasa badala ya kuendelea kumchukulia kama adui pamoja na vifo anavyosababisha ni vema tukamfanya kuwa rafiki.

Ndio Corona ili tumshinde lazima tubadili mbinu,tumuombe na akikubali basi awe rafiki yetu.Kwanza tumpokee na kumkaribisha Duniani. Wakati nimeanza kuandika huko mwanzoni nilianza kwa kumkaribisha na kumjulia hali.

Ukweli Corona akiwa rafiki yetu na tukakubali kuishi naye tutamuelewa anahitaji nini? Tutajua mbinu zake,tutajua ujasiri wake,tutajua udhaifu wake.Yaani naomba mnielewe huyu Corona tukimfanya kuwa rafiki anaweza kutuambia vitu gani ambavyo ni rahisi kumdhuru na kumuondosha kabisa Duniani.

Atatuambia tu ,si unajua tena kawaida ya marafiki, wanaambian kila kitu na huko kuambiana ndiko kuna wakati unasikia wanakula kiapo .Utasikia hii iwe siri yetu.Naamini hata Corona akiwa rafiki kuna siri zake atatueleza.

Kwanza tukumbushane, hata Ukimwi wakati unaingia Duniani nao uliingia kama adui.Na kweli ameua watu wengi na bado anaendelea kuua.Ukimwi hauna tiba.Hauna dawa.Hata hivyo Baada ya kumpokea na kumkaribisha kwenye Jamii Ukimwi pamoja na kuwa hana tiba angalau tunajua namna ya kuishi naye.Tunajua namna ya kumkwepa.

Tunajua hata kumpunguzia nguvu kwa kutumia  dawa za ARV. Leo hii ugonjwa wa Ukimwi unazaidi ya miaka 35 au zaidi kwa hapa Tanzania.Sawa Kuna tofauti Kati ya Ukimwi na Corona lakini Ukweli wote Ni virusi,kazi inabaki kwenye kutofautiana kwenye kuambukiza.

Hivyo hata Corona naye tukisema yupo na lazima tukubali yupo tutamshinda tu.Kwa siku chache tu ambazo amekuwepo tunaambiwa hata maji tiririka na sabuni inamtosha kumuondoa.Sasa tukikubali kuwa karibu tutashindwa nini kumuelewa zaidi.

Utafiti wangu mdogo usio wa kitalaam naamini kabisa Corona namna ambavyo ameingia Tanzania naamini atakuwa anashangaa.Hakuna anayemuogopa.Yupo mtaani na sisi tupo mtaani.Hakuna aliyerudi nyuma kwasababu yake.Kwetu Corona ni mdudu mdogo tu na siku zake za kuishi zinahesabika.

Mungu yuko pamoja nasi, aliumba Dunia na kisha kutuweka wanadamu tuitawale,leo eti Corona ndio anataka kuitawala Dunia haiwezekani.Tuache kutiana hofu, Corona sawa ni hatari lakini umeshafuatilia kuhusu ugonjwa Kifua Kikuu( TB) .Kwa Tanzania kila ndani ya saa 24(Siku moja) watu 61 wanafariki Dunia.

Swali TB imekuwepo kwa miaka mingapi? Kisha aangalia idadi ya watu waliofariki kwa TB kisha linganisha na Corona kwa hapa kwetu Tanzania.TB Ni ugonjwa hatari lakini tumekubali kuishi nao na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikiweka mikakati.mbalimbali ya kukomesha ugonjwa huo.

Hata hivyo pamoja na TB kuua watu 61 moja kila siku bado tuko nje, bado shughuli za kiuchumi zinaendelea.Kwanini kwenye Corona mnataka shughuli zisimame,kwanini mnataka watu wafungiwe ndani na ninachojiuliza shinikizo la watu kufungiwa ndani limekuwa kubwa sana, kwanini?

Tanzania tunashambuliwa na baadhi ya mataifa kisa tu tumeamua kupambana na Corona kwa mfumo tofuati na wengine. Naomba nihitimishe kwa kusisitiza lazima tukubali kumfanya Corona kuwa rafiki badala ya adui.

Mawasiliano yangu ni yale yale kabla na baada ya Corona 0713833822

No comments: