WAMILIKI WA VIWANDA NCHINI WAELEKEZWA KUKATA BIMA ZA MOTO.

Na Eliud Rwechungura – Wizara ya Viwanda na Biashara

Waziri wa viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa viwanda nchini kuhakikisha wanakata bima za moto ili pale wanapokumbwa na ajali za moto wapate wepesi wa kulipwa fidia za mali zao.

Bashungwa alitoa wito huo akiwa ziarani Karagwe mkoani Kagera 17 mei 2020, baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Amri Amir AL-HABSSY kilichoungua kwa moto Mei 07, 2020 nakuona mashine zilivyoharibika baada ya kuunguzwa na moto ambao chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokana na radi kubwa iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo.

Akiongea baada ya kukagua Mhe. Bashungwa alitoa pole kwa mkurugenzi wa kiwanda hicho Karim Amri pamoja na wafanyakazi ambao kwasasa wamepoteza ajira zao, ambapo alirithishwa na hatua ambazo zimekwishachukuliwa na wamiliki wa kiwanda hicho ambazo ni kufatilia bima kwaajili ya kulipwa fidia.

“Tunapokuwa na viwanda hatujui mambo ya kesho na keshokutwa, mambo ya ajari unaweza kupanga kila kitu lakini hakuna anayetegemea ajari itatokea muda gani, kwahiyo kupitia kiwanda hiki nitoe wito kwa viwanda vyote nchini tuwe tunakata bima, maana kiwanda hiki kimeungua lakini walikuwa na bima ya moto.”

Awali meneja wa kiwanda hicho Daniel Ndayanse akitoa taarifa kwa Waziri alieleza hasara walioipata baada ya kufanya tathimini ya hasara iliyotokana na kuungua kwa kiwanda hicho kuwa ni mashine za kiwanda ni takribani Tsh.1,328,940,000.00 na jingo la takribani Tsh. 49,275,750.00 na kuongeza kuwa kiwanda kilikuwa na waajiliwa wa kudumu 16 ambao wapo kwa kipindi chote cha mwaka na wakati wa msimu huwa kinaajili watu kuanzia 800 hadi 1000 kulingana na kazi ya siku.

Aidha, Meneja alieleza kuwa “Kiwanda chetu tulikuwa tumekiimalisha kwa kukifanya cha kisasa ambapo tuliweza kuzalisha kati ya tani 50 hadi tani 65 za kahawa safi ambazo ni takribani gunia kati ya 800 hadi 1,000 kwa masaa 24, kwa kukoboa kahawa maganda kati ya tani 115 hadi tani 140 kwa masaa hayo 24 kama hakuna tatizo la umeme.” 

Kwaupande wake mmiliki wa kiwanda Bw.Karim Amri alimshukuru Mhe.Rais John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuimarisha na kuweka sera bora za viwanda kwa wawekezaji nchini, ambapo alitumia fursa hiyo kutoa maombi maalumu kwa Mhe.Waziri Bashungwa.

“Tunakuomba wewe Mhe.Waziri kuweka msukumo kwa watu wa bima BRITAM INSURANCE ambao tulikata bima kwao waweze kutufanyia haraka watulipe ili tuweze kununua mashine kufikia mwezi julai mwaka huu kiwanda kianze kufanya kazi”.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio waliyo nayo kwa upande wa viwanda wilayani Karagwe alifafanua changamoto kubwa inayowasumbu mara kwa mara kuwa ni tatizo la umeme ambalo limekuwa tatizo sugu kwa wenye viwanda ambapo alisema kuwa kuna siku umeme unakatika na kuwaka Zaidi ya mara 20 hivyo husababisha kuungua kwa Motors,taa, na mitambo mingine.

Kufatia kukithiri kwa matukio ya moto wilayani Karagwe, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake mkuu wa wilaya Godfrey Muheruka imeamua kujenga kituomcha zima moto na uokoaji ambacho kitakuwa kikisaidia kwenye ajali za moto pale zinapotokea.

Hata hivyo kitendo cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya karagwe kuamua kujenga jingo la zima moto na uokoaji kikamshawishi waziri Bashungwa kuchangia mifuko 200 ya saruji na kuwataka wadau wa maendeleo kuchangia ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.



Waziri wa viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa{aliyevaa koti} akikagua kiwanda kukoboa kahawa cha Amri Amir AL-HABSSY kilichoungua kwa moto Mei 07, 2020 ambacho chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokana na radi kubwa iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo iliyosabisha hasara ya takribani Tsh.1,328,940,000.00 kushoto ni mmilioki wa kiwanda Karim Amri, kulia ni Mkuu wa wilaya Karagwe Godfrey Muheruka. Karagwe, Kagera {Picha na Eliud Rwechungura – Wizara ya Viwanda na Biashara}.
Waziri wa viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa{aliyevaa koti} akiongea na uongozi wa kiwanda kukoboa kahawa cha Amri Amir AL-HABSSY kilichoungua kwa moto Mei 07, 2020 ambacho chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokana na radi kubwa iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo iliyosabisha hasara ya takribani Tsh.1,328,940,000.00 Karagwe, Kagera {Picha na Eliud Rwechungura – Wizara ya Viwanda na Biashara}

No comments: