WAMILIKI WA VIWANDA KUZALISHA UNGA WALALAMIKIA KUSHUKA KWA UZALISHAJI


NA DENIS MLOWE, IRINGA

WAMILIKI wa viwanda vya kuzalisha unga wa sembena wafanyabiashara wa chakula ‘mama lishe’ mkoani Iringa wamelalamika kuporomoka kwa uzalishaji na wateja kutokana na janga la Corona linaloendelea duniani kote.

Wakizungumza na mwanahabari wamiliki hao wamesema kwamba hali ya sasa ya uzalishaji imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na biashara hiyo kuathiriwa na kuenea kwa virus vya corona nchini.

Mmoja wa wa wamiliki hao, Alfred Mpanga mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha unga wa Sembe wa AMP Sembe alisema kuwa kwa sasa uzalishaji umepungua kwa kiasi kikubwa kuytokana na janga la virusi vya Corona hali ambayo imewaathiri kwa kiasi kikubwa katika biashara.

Alisema kuwa awali walikuwa wanazalisha zaidi ya tani 6 hadi 8 kwa siku tofauti na sasa ambapo wanazalisha tani mbili kwa siku hii yote kutokana na kupungua kwa wateja ambao walikuwa wanawategemea nje ya mkoa wa Iringa.

Mpanga alisema kuwa hali hiyo imewafanya kukabiliana na hali ngumu ya maisha kwani uchumi wao kwa ujumla umepungua na kuwa katika hatari ya kupoteza hata mtaji kwani biashata hakuna na taasisi za kifedha zinawadai.

Alisema kuwa kutokana na kupungua kwa uzalishaji amelazimika kuponguza idadi ya wafanyakazi katika kiwanda hicho ili kuendana na hali ya soko kwani wakati mwingine wamekuwa wakifunga kabisa ofisi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji kuliko kipato wanachopata.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kiwanda kinachozalisha unga wa sembe cha Ihemi, Dickens Lulandala alisema kwa kuwa kufungwa kwa shule za sekondari na msingi ambazo zilikuwa zinanunua unga kwenye kiwanda hicho kimewaathiri kwa kiasi kikubwa na hii kutokana na kuenea kwa virusi vya corona.

Lundala alitoa wito kwa serikali na taasisi za Fedha kurekebisha mifumo ya Ulipaji wa Madeni yao kutokana na kuporomoka kwa Biashara ya chakula na kushindwa kumudu gharama za maisha.

Kwa upande wao mamalishe ambao wanafanya shughuli zao katika eneo la Igumbilo, Devotha Salim, Getruda Mwipoki walisema kuwa kwa sasa biashara ya chakula imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana wateja wao wengi kujifungia nyumbani hali ambayo wanapika kilo mbili za chakula lakini bado zinabaki.
Walisema kuwa hali hii ikiendelea basi maisha yatakuwa magumu zaidi kwani wanategemea biashara kuendesha maisha yao na kulipa mikopo wanayodaiwa kwenye taasisi za kifedha hivyo kuporomoka kwa Biashara za Chakula na Nafaka kunatajwa kuwa na athari zinazowafanya washindwe kuendesha maisha yao ikiwa ni pamoja na Ulipaji wa Kodi ya serikali.
Mkurugenzi wa kiwanda cha kualisha unga wa sembe wenye virutubishi wa AMP Sembe, Alfred Mpanga akizungumza na na wanahabari kuhusu changamoto wanazokumbana nazo kutokana na kushuka kwa uzalishaji. (PICHA NA DENIS MLOWE)
viroba vya mahindi vikiwa nje kwa ajili ya kwenda kusagwa huku shehena ya unga ukiwa kiwandani hapo kusubiri wateja.

No comments: