THBUB: Msamaha kwa Wafungwa ni hatua muhimu kuzuia maambukizi ya Korona Magerezani

Na Mbaraka Kambona,

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) amesema uamuzi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli wa kuwasamehe wafungwa 3973 ni hatua muhimu katika kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya maradhi yanayosababishwa na Virusi vya Korona.

Jaji Mwaimu aliyasema hayo leo Mei 7, 2020 Ofisini kwake jijini Dodoma alipokuwa akitoa mtazamo wake juu ya jitihada za Serikali za kudhibiti kuenea kwa maradhi hatari ya Korona.

Alieleza kuwa msamaha huo ni muhimu hasa katika nyakati hizi ambapo Tanzania na nchi nyingine Dunia zipo katika kupambana na vita kubwa ya mlipuko wa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Korona.

Jaji Mwaimu aliendelea kusema kuwa msamaha huo utasaidia sana kupunguza msongamano kwa wafungwa na mahabusu unaoweza kuhatarisha afya zao.

“Kimsingi msamaha huu wa Rais utasaidia kulinda haki ya afya kwa wananchi. Sisi Tume tunaona uamuzi huu wa Rais Magufuli umebebwa na nia njema ya kutaka kuwalinda wananchi anaowaongoza”, alisema Jaji Mwaimu

Aliendelea kusema kuwa Serikali inaweza kuendelea kupunguza misongamano kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Sheria iliyopo kwa kutoa adhabu mbadala ikiwemo matumizi ya Sheria ya Parole ambayo inaruhusu vifungo vya nje kwa wale wafungwa wenye tabia njema.

Katika hatua nyingine, Jaji Mwaimu aliwashauri baadhi ya askari Polisi ambao wamekuwa wanalalamikiwa kuwa na tabia ya kubambikiza kesi wananchi kuacha kufanya hivyo kwani ni moja ya chanzo cha misongamano isiyo ya lazima magerezani.

Aidha, Jaji Mwaimu alimpongeza Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ziara zake za hivi karibuni magerezani ambapo lengo lake ni kupunguza misongamano magerezani kwa kufuta kesi za Mahabusu baada ya kuona baadhi yao kesi zao hazina msingi wala ushahidi wa kutosha.

Hata hivyo alimuomba DPP aendelee na jitihada hizo ili kupunguza misongamano magerezani.

Pia Mwenyekiti anaona kuwa Mahakama ina mchango katika kupunguza misongamano magerezani kwa kutoa dhamana kwa makosa yanayodhaminika kwa masharti nafuu.

Vile vile alisema kuwa ameliomba Jeshi la Polisi kwa mamlaka iliyonayo kutoa dhamana kwa watuhumiwa waliopo katika vituo vyao ambao wana makosa madogomadogo ambayo yanaweza kudhaminika ili kupunguza misongamano katika mahabusu zao.

Aprili 26, 2020 kwenye Maadhimisho ya miaka 56 ya Muungano, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 3,973 ambapo kati ya hao 256 walikuwa wanakabiliwa na adhabu ya kunyongwa na wamebadilishiwa adhabu hiyo.

No comments: