WALIOKUWA VIGOGO KAMPUNI YA ACACIA WANAOKABILIWA NA KESI YA UHUJUMU UCHUMI WAANDIKA BARUA KULALAMIKIA UPELELEZI KUCHUKUA MUDA MREFU

 Na Karama Kenyunko Michuzi TV

ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Kampuni ya ACASIA Deo Mwanyika na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka ya tuhuma za uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wameandikia barua katika Mahakama ya hiyo wakilalamikia upelelezi katika kesi yao kuchukua muda mrefu.

Washtakiwa hao wamedai hayo leo Mei 8, mwaka 2020 mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya, kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali Ester Martin kueleza kuwa upelelezi bado haujakamilika hivyo ameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa Utetezi Hudson Ndusyepo alidai wateja wake wameandika barua mahakamani wakilalamikia upelelezi kuchukua muda mrefu ambao ni takribani siku 526 na wao wako gerezani kwa kuwa mashtaka yao hayana dhamana.

Alidai wanaomba Mahakama imwelekeze Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), aweze kujibu kiofisi malalamiko hayo ya kuchelewesha upelelezi huku pia wakiomba kuonana na mawakili wao ili waweze kujadiliana kuhusu kesi hiyo.

Akijibu hoja hizo Hakimu Isaya ameutaka upande wa mashtaka kuwasiliana na Mamlaka ya juu ili Mei 22, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa waweze kuja na majibu ya malalamiko hayo.

Aidha, alikubaliana na maombi ya washtakiwa kukutana na mawakili wao ambapo aliamuru Mei 22, waletwe mahakamani hapo.

Mbali na Mwanyika, washtakiwa wengine ni, Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo,  Mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku Assa Mwaipopo, Kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Wote wanakabiliwa na mashitaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya fedha za Marekani milioni 112.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama , mashitaka saba ya kughushi , mashitaka 17 ya utakatishaji wa fedha, Kuwasilisha nyaraka  za uongo  kwa  Mamlaka ya Mapato Tanzanian (TRA),  kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashitaka nane ya kukwepa kodi na shitaka moja la kutoa rushwa.

No comments: