VIGOGO SITA WA KAMPUNI YA VIETTEL TANZANIA NA HALOTEL WAMWANDIKIA BARUA DPP KUOMBA KUINGIA MAKUBALIANO YA KUKIRI MASHTAKA YA KUISABABISHIA TCRA HASARA YA SH BILIONI 75

Na Karama Kenyunko

VIGOGO sita wa Kampuni ya Viettel Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Halotel, Son Nguyen (46), wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), wakiomba kuingia makubaliano ya kukiri mashtaka ya kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya zaidi ya Sh bilioni 75.

Mbali na Nguyen washitakiwa wengine ni Nguyen Minh (40)  na Vu Tiep ambao wote ni Mameneja wa Halotel, Ha Than (39) Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) Halotel, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Nguyen Cong na Kampuni ya Viattel yenyewe.

Mapema leo Jumatatu Mei 4, 2020 wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika hivyo, aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Utetezi, Majura Magafu akisaidiana na Idd Msangi alidai, Aprili 21 mwaka huu washtakiwa waliandika barua kwa DPP wakitaka kuingia makubaliano ya kukiri makosa yao.

Magafu alidai walikutana na maofisa wa DPP kuangalia kama maombi yao yamefanyiwa kazi ili kesi hiyo iweze kuisha kwa utaratibu wa makubaliano (bargaining) lakini mkakati wao huo  haukukamilika kwa sababu DPP ambaye ndiye anatakiwa kutoa kibali cha kuipa mahakama ya Kisutu mamlaka ya kusikiliza kesi hii amesafiri kikazi na atakuwepo Dodoma katikati ya wiki hii.

Pia alidai wataendelea na majadiliano kuhakikisha yanafanikiwa hivyo, aliomba mahakama ipange kesi hiyo Ijumaa wiki hii ili kuona kama maombi yao yatakubaliwa.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Simon alidai majadiliano kati ya pande hizo mbili yanaendelea na sio kwamba yamekamilika hivyo, aliomba mahakama ipange kesi hiyo katika utaratibu wa kawaida wa siku 14.

Hakimu Simba alisema endapo makubaliano hayo yatakamilika ndani ya wiki hii washitakiwa wataitwa mahakamani kwa wito maalum ili kusikiliza kesi yao na kuwataka kuendelea na majadiliano ili yakamilike kwa wakati.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.


 Washitakiwa wanadaiwa hao kati ya Juni 8,2017 na Machi 26,2020 maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida, huku pia wakituhumiwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali kutoka TCRA.

Aidha, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Julai 7,2016 na Machi 26, mwaka huu maeneo hayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Vietnam kwa pamoja walitengeneza mfumo ambao ulitumia huduma za mawasiliano zinazojulikana kama Virtual Private Network (VPN) kinyume na taratibu.

Pia kukwepa kulipa kodi kwa TCRA kwa kutumia mitambo ya mawasiliano yaliyounganisha Viettel Tanzania na Vietnam  kinyume na sheria.

Aidha wanadaiwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali cha TCRA na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 75.

Pia wanadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu kwa kutumia mitambo ya VPN waliisababishia TCRA hasara ya Sh bilioni 3.03.

Washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 3.03 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuongoza genge la uhalifu.

Kampuni ya Viettel Tanzania inadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu ilitakatisha Sh bilioni 3.03 na mashitaka ya tisa na 10, washitakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 75 wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu.
. Washitakiwa wapo rumande.
 
 VIGOGO sita wa Kampuni ya Viettel Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Halotel, Son Nguyen (46), wamemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), wakiomba kuingia makubaliano ya kukiri mashtaka ya kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya zaidi ya Sh bilioni 75.

No comments: