TAASISI YA AMANI TANZANIA YAWATAKA WANASAISA KUACHA KUTUMIA JANGA LA CORONA KAMA MTAJI WA KISIASA, WAUNGA MKONO HOTUBA YA RAIS MAGUFULI
Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani Tanzania Sadiki Godigodi(kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Mei 20 jijini Dar es Salaam wakati akielezea taasisi hiyo inavyomuunga mkono Rais Dk.John Magufuli katika mapambano dhidi ya janga la Corona.Katikati ni Mkurugenzi wa Siasa na Dini wa taasisi hiyo Alhaji Dk.Sule Seif na kushoto ni Mshauri wa taasisi hiyo Issa Mkalinga.
Mshauri wa Taasisi ya Amani Tanzania Issa Mkalinga (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.Wengine ni Mkurugenzi wa Siasa na Dini wa taasisi hiyo Alhaji Dk.Sule Seif(katikati) na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sadiki Godigodi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani Tanzania Sadiki Godigodi(kulia) akisisitiza jambo kwa waaandishi wa habari wakati wa mkutano kati ya taasisi hiyo na waandishi wa habari.Wengine ni Mshauri wa taasisi hiyo Issa Mkalinga(kushoto) na Mkurugenzi wa Siasa na Dini wa taasisi Alhaji Dk.Sule Seif.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV.
TAASISI ya Amani Tanzania imewaonya baadhi ya wanasiasa nchini ambao wanatumia nguvu katika janga la Corona kufanikiza adhima zao za kisiasa, ni vema wakati huu wakatumia nguvu hiyo hiyo kuunga mkono juhudi za Rais Dk.John Magufuli na timu yake ili kupambana ugonjwa huo ambao umekuwa vita kubwa.
Imesema ni vema wanasiasa wa aina hiyo wakaacha kupotosha na kuwatia hofu wananchi kwa kueleza kuwa Tanzania haijafuata ushauri na maelekezo ya Shirika la Afya Duniani(WHO) na badala yake wajenge umoja , ushirikiano na kuilinda nchi yao kwa kutoa mawazo mazuri yatakayoleta faida kwa wananchi wote sasa na vizazi vijavyo .
Hayo yameelezwa leo Mei 20 jijini Dar es Salaam wakati viongozi wa ngazi za juu wa Taasisi ya Amani Tanzania walipokutana na waandishi wa vyombo vya habari nchini kwa lengo la kuelezea namna ambavyo wamefurahishwa na hatua ambazo zimechukuliwa na Rais Magufuli kukabiliana na Covid-19.
Mkurugenzi wa Siasa na Dini wa Taasisi hiyo ya Amani Tanzania Alhaji Dk.Sule Seif amesema kuwa jambo kubwa la kumpongeza Rais Magufuli katika kulishugghulia janga la Corona ameweka msimamo thabiti juu ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kutofunga nyumba za ibada na kuendesha dua na maombi mbalimbali ili kukabiliana nalo janga hilo kwa msaada wa Mungu.
Dk.Sule amesema hatua hiyo imeleta tija kubwa kwani makadirio ya vifo pamoja na maambukizi yaliyokuwa yamekadiriwa na WHO hayakufikia yalivyotarajiwa."Jambo ambalo tunaamini maombi yetu Watanzania yamejibiwa na Mwenyezi Mungu.Hivyo hatuoni sababu ya Corona kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kama mtaji wa kufanikisha mambo yao, bali tuungane na Rais kwenye vita hii."
Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sadiki Godigodi amesema kuwa taasisi yao imekuwa ikiwaita waandishi wa habari mara kwa mara hasa linapotokea jambo linalohusu Taifa na maslahi mapana kwa nchi.Hivyo wameona haja ya kuzungumzia hotuba ya Rais Dk.Magufuli aliyoitoa Mei 17 mwaka huu akiwa kwenye Ibada iliyofanyika Kanisa la KKKT Usharika wa Chato mkoani Geita.
Godigodi amesema Rais kwenye hotuba hiyo amezungumzia mambo mengi ya msingi na yenye maslahi kwa Taifa kutokana na sababu hizo wameona haja ya kuungana naye katika hotuba yake hiyo ili kumpongeza na kuendelea kumtia moyo.
"Kwanza kabisa kuendelea kumpongeza kwa msimamo usiyoyumba kuhusu vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 , miongoni mwa hayo ni kutoiweka nchini kwenye Lockdown , jambo ambalo lingeleta maafa makubwa kwa jamii yetu kuliko ugonjwa wenyewe.Pia hata nchi ambazo zimeweka sheria hiyo imeonekana ni kuwatesa wananchi wake , jambo ambalo limeleta vurugu katika baadhi ya nchi.
"Na katika nchi nyingine wameamua kuindoa sheria hiyo ili wananchi waendelee kujitafutia riziki zao jambo ambalo kwa hapa Tanzania Rais wetu aliliona mapema na hakuwa tayari kuwatesa wananchi wake , hii inathibisha kwamba Rais Magufuli ni kiongozi anayezingatia maisha ya wanyonge,"amesema Godigodi.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo imeendelea kushuhudia namna ambavyo mataifa mengine duniani yanavyofuata mbinu anazotumia Rais Magufuli katika vita dhidi ya Corona."Mtakumbuka mambo kadhaa aliyoyasema Rais na sasa ndio yanatokea, mfano Rais wetu alieleza kuwa virusi vya Corona havifi kwa kunyunyuzia dawa ya kuua wa wadudu , tumesikia WHO likiunga mkono kauli hiyo ya Rais."
Pia Rais Magufuli alisema kuwa mazingira ya ugonjwa wa Covid-19 yataendelea kuwepo kama ilivyo kwa magonjwa mengine na hivyo kuwataka watanzania wasijenge hofu na badala yake wachape kazi huku wakiendelea kuchukua tahadhari muhimu dhidi ya kujikinga na ugonjwa huo zinazoendelea kutolewa na watalaam wa afya nchini.
No comments: