Stanbic Tanzania yatoa afueni ya madeni kwa wateja zaidi ya 265

Kufuatia athari za kiuchumi zilizosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa kirusi cha Corona (COVID-19) benki ya Stanbic Tanzania imetangaza kutoa unafuu wa malipo ya mikopo kwa wateja wake kwa muda wa miezi 3 hadi 6. Afueni hiyo ya malipo iliyoanza mwezi Aprili ikilenga sekta ya utalii pekee, hivi sasa imeongezwa na kulenga sekta zingine kama vile usafirishaji, nishati na wafanyabiashara wa kati na wadogo. 

Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati endelevu yenye lengo la kuwawezesha wateja wa benki hiyo kukabiliana na adha za kiuchumi zitokanazo na mlipuko wa ugonjwa wa Corona. 

Mkuu wa Idara ya Huduma Binafsi na Biashara, Brian Ndadzungira alisema kuwa benki hiyo inatambua umuhimu wa wateja wao kuendelea kujishughulisha licha ya uwepo wa janga la COVID-19. “Tunaelewa kwamba shughuli za kibiashara nchini zimeathirika kutokana na hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani katika kupambana na ugonjwa huu. 

Hivyo tukaamua kuja na suluhisho ambalo litasaidia kupunguza athari za kifedha zinazowakabili wateja wetu. Tunaimani kwamba hatua hii haitasaidia tu wateja wetu wa biashara ndogo na kati kuweza kumudu ulipaji wa mikopo yao, bali pia kuwalipa wafanyakazi pamoja na wasambazaji. 

Hadi sasa benki hiyo imeweza kutoa afueni kwa wateja zaidi ya 265, ikiwa ni kiasi zaidi ya shilingi bilioni 37 ya mikopo hiyo. Pia, benki ya Stanbic imeendelea kutoa ushauri wa kifedha kwa wateja wake kuhakikisha wanakuwa na mkakati thabiti wa kuendeleza biashara.

 “Tunawasisitiza wateja wetu wote ambao wanapitia changamoto za kifedha kutokana na uwepo wa COVID-19, kuwasiliana nasi haraka ili kwa pamoja tuweze kutafuta suluhisho madhubuti,” aliongeza Ndadzungira. 

“Kama benki tunaendelea kujidhatiti katika kuleta matokeo chanya kwenye jamii tunayoihudumia na kuunga mkono serikali katika kudhibiti athari za kiuchumi zinazosababishwa na ugonjwa huu,” alisema Ndadzungira. 

No comments: