SPIKA NDUGAI AWATAKA WABUNGE CHADEMA KURUDISHA POSHO WALIOZOCHUKUA BUNGENI

*Pia aagiza warudi bungeni haraka wakiwa na vipimo vyao vya majibu ya Corona
*Watakaogoma majina yao kukabidhiwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama

Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

SPIKA wa Bunge Job Ndugai amekunjua makucha yake kwa wabunge wa Chadema ambao wametoroka Bungeni wakiongozwa na Freeman Mbowe huku akiwataka warudi bungeni haraka iwezekanavyo na fedha za posho wamechukua kwa siku 14 wanatakiwa kuzirudisha kwa kuziweka katika akaunti ya Bunge.

Pia Spika Ngugai amewaagiza wabunge hao kuwa wakati wanarudi bungeni watatakiwa kuwa na vipimo vyao vya Corona ili kujua kama wana maambukizi au laa kwani hivi sasa baada ya kuondoka bungeni wamekuwa wakizurula mikoani wakati wabunge wengine wakiendelea na vikao vya Bunge.

Akizungumza leo Mei 6,2020 Bungeni Mjini Dodoma, Spika Ndugai amelieleza Bunge Mbowe hana mamlaka ya kuitisha utoro na mgomo kwa wabunge na kufafanua anachokifanya ni kama Kaka Mkuu wa Shule ya Sekondari.

"Haya mambo nayakumbuka enzi hizo tukiwa sekondari lakini yeye anayafanya sasa, atambue huwezi kuendesha mambo kama yuko Sekondari.Haiwezekani na taarifa nilizonazo japo wameambiana wakea Dodoma, wako wanazurula nchi nzima.

"Wanazagaa zagaa huko, barua yao si halali kwa wabunge, kwa hiyo haitambuliki, haina nafasi.Wabunge hao kokote waliko warudi bungeni haraka sana, watakaokaidi na kuendelea na huo mgomo wajue hawatapokelewa bungeni hadi pale itakapooekana kila mmoja wao amefanyiwa vipimo vya Covid-19 na kuonekana hata ugonjwa,"amesema Spika Ndugai.

Ameongeza kwasababu wao wako bungeni lakini wao wanazurula nchi nzima , hivyo hawawezi kujua wako salama au laa.Pia maagizo mengine ambayo Spika wa Bunge ameyatoa kwa wabunge hao watoro huko mikoani waliko wakati wanaondoka bungeni walikuwa wameshalipwa posho za siku 14 kuanzia Mei 1 hadi Mei 17, 2020.

"Jumla ya wabunge wote wa kundi hil wamechukua posho ya Sh.110,160,000, hivyo ukiondoa hawa ambao wamendeelea na vikao ambao hatutawadai, wabunge wengine wote kuanzia na Freeman Mbowe mwenyewe kurudisha Sh.2,040,000 ambazo wamelipwa kila mmoja, na wabunge wenzake nao warudishe kiasi kama hicho hicho ambacho wamechukua.

"Kwa vile ule ni utoro wa hiyari na hizo ni fedha za wananchi, na walichokifanya ni wizi, na ni mfano mbaya kwa viongozi, unachukua fedha za wananchi maskini uwafanyie kazi yao wewe unatoroka, unajiwekea migomo ambayo haina kichwa wala miguu na tena fedha hizo ziko mfukoni na ndio wanazulia.

"Pia kuna wabunge waliolipwa Sh.milioni tatu kwa kila mmoja na wabunge hao ni Catherine Ruge , Devotha Minja , Joyce Nkya, Rhoda Muchela,, Zainabu Mussa Bakari na Zebeda Hassan na waliobakia wote walichukua Sh.milioni mbili na elfu arobaini.Maagizo yangu kila mmoja wao arudishe hizi fedha, anapofika getini mgomo wake umeisha bila fedha hizi hataruhusiwa kuingia bungeni,"amesema.

Ameongeza baada ya tarehe hizo ambazo wamejiwekea kama hawatarudisha fedha hizo atapeleka orodha ya majina yao kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na litakuwa jambo ambalo sasa Mwanasheria Mkuu atasaidia kuona hatua gani inafaa kushughulikia suala hilo.

"Mimi kama Spika wa Bunge warudishe fedha hizo haraka kwenye akaunti ya Bunge vinginevyo hawatapokelewa bungeni.Hivyo mambo mawili lazima wayafanye , warudishe fedha walizochukua na pili wawe wamepima Corona na majibu yanaonesha hawana tatizo.

"Hatua nyingine zinafuatia, kwasababu wao si wababe bwana... na wapo mwisho mwisho hapa wajue wanacheza na moto, na yanayofuata kwa kundi hili la wabunge watoro yanafurahisha zaidi,"amesema Spika Ndugai huku akishangiliwa na wabunge.

No comments: