SHUGHULI ZA UTALII KUANZA TENA NCHINI.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, leo ametoa mwongozo kuhusu kuendelea kwa shughuli za utalii nchini katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID -19

Akizungumza na waandishi wa habari jijini leo, Dkt. Kigwangalla amesema shughuli za Utalii zimeanza tena rasmi leo huku akisisitiza kuwa, Tanzania itafuata utaratibu wa kujikinga na kuwakinga watalii dhidi ya ugonjwa wa COVID - 19 kwa kufuata na kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani ( WHO)

Akisisitiza zaidi, Waziri Kigwangalla amesema "Jukumu letu la kwanza tunalinda afya za watanzania Na kuwalinda watalii wasipate virusi vya CORONA hadi pale watakapoondoka nchini."

Dkt. Kigwangalla amesema, watalii watakaokuja hapa nchini watakuwa salama kiafya kwani watakuwa tayari wamepimwa katika vituo vya afya vinavyoaminika kabla ya kuanza safari.

Amesema, Serikali itahakikisha watoa huduma walioko kwenye Mnyororo wa Utalii kuanzia katika viwanja vya ndege, hotelini na kote wanakohudumia watalii, wanazingatia taratibu za kiafya ili kuwalinda watalii wanaokuja hapa Tanzania dhidi ya virusi vya CORONA.

Waziri Kigwangalla amefafanua kuwa, wahudumu wote walioko kwenye mnyororo wa Utalii, watakuwa wanapimwa mara kwa mara pale wanapojichanganya na watu wengine ili kuhakikisha hawana virusi vya CORONA.

Waziri Kigwangalla amemshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kufungua tena anga la Tanzania na kuondoa sharti la watalii kukaa  kwenye karantini kwa siku 14 wanapoingia nchini.

No comments: