RC TANGA APOKEA VIFAA VYENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 20.4 KUTOKA TANGA CEMENT KWA AJILI KUKABILIANA NA CORONA


Mwandishi Wetu, Michuzi TV -Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amepokea misaada yenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 20.4 kutoka Kampuni ya Tanga Cement kwa ajili ya kukabiliana na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mkoani hapa, Shigile amesema kuwa kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo wanaishukuru kampuni hiyo kwa namna ilivyoguswa katika  mapambano dhidi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

"Kama mnavyofahamu tuko katika vita dhidi ya Corona na uwepo wa ugonjwa huu si kwamba Serikali ilikuwa imejiandaa kuwa kutakuwa na gonjwa hili.  Lakini kama Serikali ilikuwa imefanya maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huu kama ilivyo kwa magonjwa mengine. Lakini yapo mengine yanayohitaji kusaidiana na wadau ili kukabiliana nayo. Kwa hiyo tunaishukuru sana Tanga Cement kwa msaada wao huu," amesema Shigela.

Ameongeza msaada huo umekuja wakati muafaka na kumuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Judica Omari kusimamia kuvifikisha kwa wahusika kwa namna njema.Aidha amesema msisitizo wa Rais John Magufuli wa kuchapa kazi ni jambo la msingi kwani haiwezekani kukaa bila ya kufanya kazi.

"Tulipokuwa katika ziara na mhe. Waziri Mkuu Kasim Majaliwa hivi karibuni bado Tanga Cement ilikuwa ikiendelea uzalishaji kama kawaida hata kabla ya Corona. Pia nashukuru mauzo wamekuwa wakipata ya uhakika," amesema Shigela.

Mkuu huyo wa Mkoa ameomba wadau wengine wa uzalishaji kutotetereka na hivyo kuunga mkono juhudi hizo za Rais Magufuli kwa kuchapa kazi kwa sababu hiyo ndio namna ya kujikwamua kiuchumi.

"Nimefarijika vifaa hivi vimenunuliwa hapa nchini,hivyo ninaamini vitakuwa na ubora kwa kuwa tunasisitiza katika ubora kama alivyosema Waziri wa Afya, Ummy Mwalim kwamba vifaa tiba vyote lazima tujiridhishe navyo ili viweze kutumika bila ya kuleta madhara kwa watu," anasema.

Shigela anasema "Niwaombe wadau wengine kuchangia kwa kile walicho nacho lakini pia kuendelea kuzalisha na kuweza kuchangia katika pato la nchi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkazi wa Kampuni ya Tanga Cement Mhandisi Benedict Lema amesema kampuni yake imetikia mwito wa Rais Magufuli, kwa kutoa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 20.4.

" Hili jambo ni vita ya dunia kama vile Jemedari wetu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli anavyozungumza ni lazima tusaidiane nae kupambana dhidi ya gonjwa hili la corona COVID -19. Tumefika hapa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kutoa msaada huu wenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 20.4," amesema Mhandisi Lema.

Ameongeza kuwa Tanga Cement imetoa msaada huo kwa kulenga katika makundi mawili ikiwemo Jeshi la Polisi na hospitali ya Bombo.

"Tumelenga makundi haya mawili kwasababu Jeshi la polisi ndilo linalotoa amri na pasipo kuamrisha umma inaweza kutokea uvunjwaji wa sheria. Tunajua katika wakati huu kuna uvunjwaji wa amri nyingi tu na ndio sababu tumechagua makundi haya mawili," anasema.

Akitaja vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa mkuu huyo wa mkoa wa Tanga, ni pamoja na vipima joto (thermometers 10), sabuni za maji lita 200 kila moja ikiwa na ujazo wa lita 5 (Liquid soap) kwa ajili ya jeshi la polisi na hospitali ya Bombo mkoani Tanga.

Vifaa vingine ni pamoja na Apron pcs 200, mashine za vitakasa mikono (sanitizer dispensing machines), barakoa aina ya N95 pcs 400 na mashine 30 za kuhifadhia tishu (tissue dispensing machines).

Pia Tanga Cement PLC, imefanya ukarabati wa kutenganisha wodi kwa ajili ya waathirika wa virusi vya corona kwenye hospitali ya Bombo.Mbali na hilo, pia kampuni hiyo imetengeneza eneo la uwazi la watu kusubiria huduma ili kuepusha/kupunguza misongamano. Kampuni hiyo imeahidi kutoa mashine za kutolea vipukusi (sanitizer dispensers) 50 kwa ajili ya hospitali ya Bombo.

"Kama Rais anavyosisitiza kuchapa kazi, hatujafunga kiwanda ambapo kampuni yetu imeendelea kutii amri hiyo ambapo jana pekee tumeuza tani 3,600. Kabla ya hapo tulikuwa tukiuza tani 3,000 hadi 4,000 kwa siku kutegemeana na hali halisi. Wiki hii nzima tumekuwa tukiuza saruji kati ya tani 3,000 hadi 4,000," amesema.

Ametoa ombi kwa wadau wengine kushiriki kumuunga mkono Rais ili wananchi waweze kuendelea kuwa salama na afya njema.Wakati huo huo RAS Judica Omari amesema msaada huo utasaidia katika kujikinga dhidi ya gonjwa la COVID - 19.

" Msaada huu umekuja kwa wakati kwani utakwenda kusaidia kuziba pengo la bajeti ya manunuzi ya vifaa kama hivi kwa ajili ya kukabiliana dhidi ya gonjwa la corona COVID -19. Vifaa hivitaimarisha juhudi zetu za utendaji wa watumishi wetu kazini katika kujikinga," amesema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Blasius Chatanda anasema msaada huo umekuja wakati muafaka kwani wanakutana na watu wengi kila siku ikiwemo kupokea mahabusu kila siku.
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela,wa pili kulia akikabidhiwa vifaa na Mhandisi Mtendaji Mkazi wa Kampuni ya Tanga Cement, Bw,Benedict Lema,(wapili kuShoto) Makabidhiano hayo yalifanyika mkoani Tanga , msaada wa vifaa vya kinga vya Homa ya mapafu,(COVID-19) vifaa hivyo vyenye thamani zaidi ya sh, milion 20, kulia ni Katibu tawala Mkoa wa Tanga, Judica Omari, kushoto ni Asp Blasius Chattanda
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela(wa pili kulia) akikabidhiwa vifaa na Mtendaji Mkazi wa Kampuni ya Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema,(wapili kushoto). Makabidhiano hayo yamefanyika mkoani Tanga , msaada uliokabidhiwa ni wa vifaa vya kinga vya Homa ya mapafu,(COVID-19) vyenye thamani zaidi ya sh, milion 20.4.Kulia ni Katibu tawala Mkoa wa Tanga, Judica Omari,
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, kulia akikabidhiwa vifaa na Mhandisi Mtendaji Mkazi wa Kampuni ya Tanga Cement, Bw,Benedict Lema, kuShoto Makabidhiano hayo yalifanyika mkoani Tanga, msaada wa vifaa vya kinga vya Homa ya mapafu,(COVID-19) vifaa hivyo vyenye thamani zaidi ya sh, milion 20,

No comments: