Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile awapongeza wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Grafting-CABG)
Dkt. Ndugulile: Endeleeni kutibu watu wenye magonjwa mengine na si wa Covid -19 tu
Na John Stephen, WAMJW – Dar es Salaam
07/05/2020 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wataalamu wa afya kuendelea kutibu watu wenye magonjwa mengine kama vile matatizo ya moyo na figo katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Covid-19.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile baada ya kuitembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuwaona wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo.
Dkt. Ndugulile amesema pamoja na kuwapo kwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona, watu wenye matatizo ya moyo, kupumua, figo, kisukari pamoja na matatizo mengine wanapaswa kupatiwa matibabu.
“Tunaweza tukawa tunapambana na Corona, tukawapoteza wagonjwa wengi kwa sababu tu hatujaweza kuwapatia huduma ya matibabu ya kisukari, figo, presha au moyo, hivyo nitoe rai kwa wahudumu wa afya wahakikishe wanaendelea kuwatibu watu wenye magonjwa haya pamoja na magonjwa mengine,” amesema Dkt. Ndugulile.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile amewapongeza wataalamu wa JKCI kwa kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa kwenye moyo kwa wagonjwa waliokuwa na matatizo ya moyo.
“Sisi kama Wizara ya Afya, tunapata faraja sana, mambo kama haya ni mazuri na lazima tuseme kwa hiyo hii operesheni mliofanya ni kubwa na nje ya nchi ingetugharimu shilingi milioni 80 hadi 90 kwa mtu mmoja, lakini hapa tumefanya kwa shilingi milioni 29 kwa kutumia wataalamu wetu na wagonjwa wetu wanaendelea vizuri,” amesema Dkt. Ndugulile.
Amesema awali wataalamu kutoka nje ya nchi walikuwa wanakuja kufanya upasuaji kama huo, lakini sasa Watanzania wazalendo wanafanya baada ya kutoa mishipa kwenye paja na kwenye kifua cha mgonjwa husika.
“Leo nimekuja kuona kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wazalendo wa JKCI ya upasuaji wa kupandikiza mishipa kwenye moyo ili uweze kufanya kazi kwa wagonjwa waliokuwa wakikabiliwa na matatizo ya moyo,” amesema Dkt. Ndugulile.
Naye Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Dkt. Angella Muhozya amesema kuwa wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji na wataalamu wazalendo wanaendelea vizuri na kwamba wataruhusiwa muda wowote kuanzia sasa.
Mmoja wa wagonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa moyo, Bw. Hamid Nassoro amesema baada ya kufanyiwa upasuaji hivi sasa anaweza kuzungumza vizuri tofauti na awali alikuwa hawezi kuzungumza na kwamba tayari ameshaanza mazoezi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua taarifa za mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo (Coronary artery bypass grafting (CABG) na wataalamu wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Dkt Ndugulile alitembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuwajulia hali wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimjulia hali mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Grafting-CABG) na wataalamu wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Dkt Ndugulile alitembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuwajulia hali wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angella Muhozya akimuonesha Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile maendeleo ya afya ya mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Grafting-CABG). Mgonjwa huyo alifanyiwa upasuaji na wataalamu wa Taasisi hiyo ambapo Dkt. Ndugulile aliwatembelea wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo kwa ajili ya kuwajulia hali.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuwajulia hali wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi.
No comments: