MAZIKO YA SHEIKH KILEMILE YATUFANYE TUJITAFAKARI THAMANI YETU KWA BINADAMU WENGINE
Charles James, Michuzi TV
NILIITAZAMA jana jioni, nikaitazama tena usiku, kisha nikaitazama mara nyingi mfululizo. Sijachoka kuitazama hata leo nimeamka naitazama tena. Nadhani nitaitazama mara nyingi kwa muda mrefu.
Wakati nikiitazama machozi yalikua yakinitoka. Imani yangu ilikua ikisulubika, nikijitafakari kama mimi ni binadamu mwenye thamani mbele ya wanadamu wengi.
Video niliyokua naitazama ni ya Maziko ya mmoja wa Masheikh mashuhuri na Mwanazuoni nguli wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Suleimani Imran Kilemile.
Wingi wa watu waliomzika jana Sheikh Kilemile ambaye alifariki usiku wa kuamkia jana haikua na mfanano wake. Idadi ya watu ilikuwa kubwa kweli kweli.
Pamoja na janga zito la Corona lililopo duniani kote na hata hapa kwetu, bado watu hawakujali kuhusu maambukizi. Wao waliwaza kumsitiri Mwanazuoni huyu mbobezi na nguli wa Dini ya Mwenyezi Mungu.
Sheikh Kilemile alikua Mwalimu wa wengi kwenye Uislamu, alikua mbobezi na mwenye uelewa mkubwa kwenye elimu ya Dini. Amekua msaada wa wengi kwa miaka zaidi ya 30 aliyokua akifanya kazi ya ki-Dini.
Siyo tu Tanzania wala Afrika Mashariki, Sheikh Kilemile amekua maarufu na mwenye kufundisha mafundisho ya kumpendeza Mungu duniani kote.
Nenda YouTube katafute masomo yake ya 'Tafsiri ya Quran Suratul, Nafasi ya Mwanamke katika Uislamu, Lengo la Kuletwa Mitume na Vitabu vyake utaelewa nini nachozungumza.
Turejee kwenye idadi ya watu waliojitokeza kwenye maziko yake; Wingi wa watu wale Waislamu na wenye imani nyingine ulitosha kunifanya niyatafakari maisha yangu hapa duniani.
Ni kweli wapo watu waliozikwa na idadi kubwa ya watu. Tena idadi kubwa haswa. Lakini Sheikh Kilemile amezikwa na idadi kubwa katika kipindi kigumu cha maambukizi ya Corona.
Sura za watu wale hazikuonesha dalili yoyote ya kuogopa kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Sauti zao zilikua 'busy' kusoma dua ya kumuomba Mwenyezi Mungu amuepushe na adhabu ya Kaburi Mwalimu aliyekua msaada wa wengi. Kila mmoja alitamani kuligusa jeneza lenye mwili wake.
Hofu ya Corona ingetoka wapi mbele ya mwili wa mtu ambaye ameyagusa maisha ya kundi la watu wengi kwa muda wote wa maisha yake.
Uoga wa nini katika kumsitiri binadamu ambaye ameutumia ubinadamu wake kuwafundisha binadamu wenzake matendo ya kuwapeleka peponi? Sheikh Kilemile amenifanya niililie nafsi yangu.
Jiulize ni idadi ya watu wangapi ambao hawatokua na hofu ya Corona ili tu wakusindikize katika safari yako ya mwisho siku utakayokufa?
Wangapi wataacha biashara zao, familia zao, ubize wao ili tu waje kukusitiri na kukuombea dua mbele ya Mwenyezi Mungu uepukane na adhabu ya kaburi?
Tumejiandaa kwa kiasi gani ndugu zangu? Maziko ya Sheikh Kilemile yatumike kutubadilisha tabia na mienendo yetu mbele ya wanadamu wenzetu.
Mwanasaikolojia Ramadhan Masenga amesema kupitia maziko ya Sheikh Kilemile tumepata ile tafsiri isemayo,
" Usinitafute kwenye uzuri wa kaburi lenye marumaru na chokaa bali nenda kanitazame kwenye mioyo ya watu niliowatumikia,".
Hakika Sheikh Kilemile hatutomtafuta kwenye uzuri wa Kaburi lake. Tumemuona kwenye mioyo ya watu aliowatumikia kwa maisha yake aliyoishi duniani.
Hili ni funzo siyo tu kwa binadamu wengine bali hata viongozi wa Dini zetu wanapaswa kujiuliza thamani yao kwa watu wanaowatumikia hapa duniani. Wajiulize wameyagusa maisha yao kwa kiasi gani.
Kwa viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa watumie video ile kujiuliza. Je wanauthamani gani kwa watu waliowaweka madarakani? Wametugusa kiasi kwamba tunaweza kuwazika kwa wingi ule wa Sheikh Kilemile? WAJITAFAKARI!
Nataka kusema nini? Tutendeane yaliyo mema haina maana ya kuwafanyia wenzako yale ambayo wewe hupendi kufanyiwa.
Tugeuke kuwa watu wema kwa binadamu wenzetu, Kama unampenda mtu mueleze, msifie akiwa hadharani, msamehe anayekukosea, ondoa kinyongo na chuki moyoni mwako. Mwisho tutambue kila Nyumba itaingiza Jeneza ndani na italitoa nje. TUJIULIZE!
0683 015145
No comments: