Naibu Waziri Nyongo autaka uongozi wa Stamigold kushirikiana na wafanyakazi kuzalisha kwa ufanisi



Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akionesha eneo alipokuwa akipewa maelekezo ya namna kazi za uchimbaji zinavyofanyika katika mgodi wa Stamigold uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera alipofanya ziara ya kikazi mgodini hapo. (Picha na Wizara ya Madini).

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akitoa maelekezo kwa viongozi na watumishi wa mgodi wa Stamigold mara baada ya kupokea taarifa za kiutendaji na kukagua mgodi huo. (Picha na Wizara ya Madini).
Meneja wa uchimbaji, Mhandisi Benson Mgimba akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Madini na walioambatana naye wakati wa ziara ya kikazi mgodini hapo. (Picha na Wizara ya Madini).
Watumishi wa mgodi wa Biharamulo mbele kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Mhandisi Mlekwa na Meneja wa mgodi, Mhandisi Gilay Shamika wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alipokuwa akizungumza nao katika ukumbi wa mgodi huo uliopo Biharamulo mkoani Kagera. (Picha na Wizara ya Madini).
Naibu Waziri wa Madini, akiandika maelezo anayopokea kutoka kwa Meneja wa Mgodi wa Stamigold alipotembelea mgodi huo na kuzungumza na wafanyakazi wa mgodi huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera na mwakilishi kutoka Shirika la Taifa la Madini tarehe 13 Aprili,2020. (Picha na Wizara ya Madini). Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa Naibu Waziri wa Madini wakati wa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Stamigold mkoani Kagera. (Picha na Wizara ya Madini).

******************************

Na Nuru Mwasampeta, WM

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameutaka uongozi wa Mgodi wa Stamigold kuwajali wafanyakazi na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuongeza uzalishaji katika mgodi huo. Amesema ,uongozi wa wizara utafika mgodini hapo mara kwa mara kusikiliza na kutatua changamoto zao ili kuongeza uzalishaji.

Amewataka viongozi hao kufanya kazi na wasambazaji na wataalamu wa nje wenye uadilifu na ufanisi mkubwa ili kusaidia katika kuongeza uzalishaji mgodini hapo. “Msione shida kuvunja mikataba na makampuni yasiyokwenda na kasi mnayoitaka katika kuzalisha dhahabu mgonini hapa,”Nyongo alisisitiza.

Nyongo alitoa kauli hiyo Aprili 13, 2020 alipotembelea Mgodi wa Serikali wa Stamigold unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) na kukiri kuridhishwa na maendeleo ya uzalishaji mgodini hapo.

Amesema, tofauti na ilivyokuwa awali kwa mgodi huo, mwaka huu faida ya uzalishaji imeonekana kabla hata ya kumaliza mwaka ambapo faida ya uzalishaji imeongezeka kutoka shilingi billioni 2.7 mpaka kufikia shilingi billioni 5 na kuwa na mategemeo ya kuongezeka kwa faida mpaka bilioni kumi kwa mwaka ujao.

Kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona duniani, Naibu Waziri Nyongo amesema, bado bei ya dhahabu katika soko la dunia ipo juu na kuwataka watumishi katika mgodi huo kuhakikisha wanachukua taadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya huku wakiendelea kufanya kazi kwa juhudi.

Akizungumzia bei ya dhahabu katika soko la dunia, Nyongo amesema kuwa, bei ya wakia moja imepanda kutoka dola za kimarekani 1200 hadi dola 1500. “Kutokana na ongezeko hilo la bei ya dhahabu duniani Tanzania na Stamigold kama wazalishaji wa bidhaa hiyo tunapaswa kutumia fursa hiyo kuzalisha kwa wingi ili kupata faida kulingana na uhitaji wake kwa sasa,”Nyongo alisisitiza.

Waziri Nyongo alibainisha kuwa, kunapotokea majanga kama la corona nchi nyingi zinatunza fedha zao kwa mfumo wa dhahabu hivyo hununua na kuhifadhi dhahabu kutokana na ukweli kwamba thamani ya dhahabu huongezeka kadri siku zinavyoendelea.

Hivyo sekta ya madini ni sekta pekee yenye inayoonesha uwepo wa fursa hata katika msimu huu wa corona hivyo tuchukue tahadhari zote na kuendelea kuzalisha kwa bidii.

Aidha, ameushukuru uongozi wa mgodi huo kukubali maelekezo ya Serikali ya kuwataka kuuza dhahabu inayozalishwa mgodini hapo katika soko la ndani ambapo faida ya shilingi milioni 132 zimepatikana kutokana na uuzwaji wa dhahabu hiyo nchini.

Kwa upande wake Meneja wa Mgodi, Mhandisi Gilay Shamika amesema, utafiti uliofanywa na kampuni hiyo umeonesha uwepo wa wakia 71146 zitakazozalishwa kwa muda wa miaka mitano na wakati huo huo utafiti mwingine umeonesha kuwepo kwa wakia 106854 zitakazozalisha dhahabu kwa kipindi cha miaka saba na hivyo kufanya uhai wa mgodi kuwa wa miaka 12 kuanzia mwaka 2019/2020.

Pamoja na mradi huo, Shamika amebainisha uwepo wa mradi wa visusu, amesema visusu ni mbale zilizokuwa zimechenjuliwa lakini bado zinamabaki ya dhahabu yanayoweza kuchenjuliwa tena na kuzalisha dhahabu nyingine na kukiri utekelezaji wa mradi huo utaongeza uhai wa mgodi kutoka miaka 12 na kuendelea.

Akizungumzia soko inakouzwa dhahabu inayozalishwa mgodini hapo, Shamika amesema kuanzia mwezi Desemba 2019 dhahabu yote inayozalishwa mgodini hapo inauzwa katika soko ndani ya nchi na uuzaji huo umewaletea faida ya kiasi cha shilingi 132 milioni zilizopatikana kutokana na kupungua kwa gharama ya kusafirisha dhahabu kwenda kwenye soko la dunia pamoja na malipo yaliyokuwa yakilipwa kwa wakala waliokuwa wakipokea mzigo na kuupeleka katika soko la dunia kupungua.

Pamoja na hayo Shamika ameeleza mchango wa mgodi kwa jamii inayowazunguka kuwa ni pamoja na kupata mahitaji yote muhimu ikiwepo chakula kutoka kwa jamii hiyo na kubainisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 262 kinatumika kununua mahitaji ya mgodi kutoka kwa jamii hiyo.

Akizungumzia changamoto zinazoukabili mgodi huo, Shamika alisema mitambo mgodini hapo inaendeshwa kwa kutumia mafuta na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.01 kwa mwezi kiasi ambacho ni kikubwa kwa mgodi na kubainisha kuwa endapo wataunganishiwa umeme wa gridi ya taifa kiasi kitakachokuwa kikitumika ni shilingi milioni 300 pekee jambo ambalo litasaidia katika kupunguza gharama inayotumika hivi sasa.

Hata hivyo, amesema tayari mazungumzo na Shirika la Umeme la Taifa yamefanyika na mchakato unaendelea kujadili mahali sahihi kwa kuunganishia umeme huo kati ya Geita au Nyakanazi kulingana na umuhimu na uharaka wa huduma hiyo na kuiomba serikali kuwashika mkono ili kuweza kuondokana na changamoto hiyo kwa wakati.

Changamoto nyingine amesema, ni pamoja na ufinyu wa mtaji wa visusu kutokana na kuwa na kiasi kidogo walichonacho wanahitaji wizara iwashike mkono ili kuwawezesha kupata mkopo na kuendesha mradi huo kwa manufaa ya taifa ili kwa haraka.

Mbali na hayo, Shamika ameishukuru Serikali kwa namna inavyosimamia na kuwatia moyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili.

No comments: