NAIBU WAZIRI NISHATI AZINDUA MRADI WA UMEME JUA NANJIRINJI
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akisisitiza jambo, mara baada ya kuzindua rasmi mradi wa umeme jua Nanjirinji, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi, Mei 17, 2020. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba-meza kuu), katika kijiji na Kata ya Nanjirinji, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi ambapo alizindua rasmi mradi wa umeme jua Mei 17, 2020.
Baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakifuatilia hafla ya uzinduzi rasmi wa mradi wa umeme jua Nanjirinji, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi, uliofanywa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Mei 17, 2020.
Na Veronica Simba, Lindi
NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amezindua rasmi mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika vijiji vya Kata ya Nanjirinji, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.
Akizungumza na viongozi wa eneo hilo akiwemo Mkuu wa Wilaya, Diwani na viongozi wa vijiji husika, muda mfupi kabla ya kufanya uzinduzi, Mei 17, 2020, Naibu Waziri alieleza kuwa mradi huo unalenga kuwapatia huduma ya umeme wananchi wakati serikali ikijiandaa kupeleka umeme wa uhakika kupitia mradi wa umeme vijijini.
“Tunashukuru Bunge kwa kupitisha bajeti ya Wizara yetu kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambayo pamoja na mambo mengine, imejikita katika upelekaji umeme vijijini. Nafurahi kuwajulisha kuwa vijiji vya Nanjirinji ni miongoni mwa vitakavyopelekewa umeme ndani ya kipindi husika,” alisema.
Aidha, Naibu Waziri alieleza kuwa mradi huo ambao pia unatekelezwa Kilwa kisiwani ni mpango mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya umeme mkubwa, vikiwemo visiwa, wanafikishiwa pia huduma ya umeme ili waweze kunufaika sawa na wananchi wa maeneo mengine.
Aliwataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ndiyo wafadhili wa miradi ya aina hiyo kote nchini, kujenga utaratibu wa kutembelea miradi hiyo ili kujiridhisha endapo fedha zilizotolewa na Wadau wa Maendeleo katika kutekeleza miradi hiyo zinatumika kwa tija.
Kwa mantiki hiyo, aliutaka Wakala huo kuanzisha kitengo cha tathmini na ufuatiliaji, ambacho kitashughulikia masuala hayo katika miradi yote ya umeme jadidifu.
Halikadhalika, alitoa maelekezo hayo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
“TANESCO ninyi ndiyo mnahusika na uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, hivyo mnawajibika pia kufuatilia miradi hii na kufanya tathmini badala ya kuwaacha wananchi wakiwa hawana pa kukimbilia kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.”
Alisema, katika ziara zake sehemu mbalimbali nchini kukagua miradi ya aina hiyo, amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuwa miradi hiyo haina mfuatiliaji badala yake anaachwa mkandarasi pekee pasipo usimamizi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alitumia fursa hiyo kuwaeleza viongozi hao kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imeanza kulipa fidia kwa wananchi wa eneo la Likong’o mkoani humo, ambao wamepisha mradi wa kuchakata gesi.
Alisema jumla ya shilingi bilioni tano zimetolewa na kwamba mazungumzo yanaendelea baina ya serikali na wawekezaji kuhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachochochea uchumi wa Mkoa wa Lindi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi walioshiriki tukio hilo, waliipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma hiyo ya umeme lakini wakaomba wapelekewe umeme wa uhakika zaidi kulingana na mahitaji makubwa waliyonayo hususani katika kuendesha viwanda vya kuchakata ufuta ambao huzalishwa kwa wingi wilayani humo.
Aidha, walimwomba Naibu Waziri afikishe kilio chao cha ubovu wa barabara kwa Waziri mwenye dhamana ya miundombinu, wakisema hiyo ni changamoto kuu katika eneo hilo.
Mradi huo wa Umeme Jua ulianza kutekelezwa mwaka 2017 na ulipangwa kukamilika mwaka huu wa 2020. Mradi umelenga kuunganisha umeme kwa wateja 80 katika vijiji vya Nanjirinji, ambao hata hivyo imeelezwa kuwa mahitaji yameongezeka kufikia wateja 350 wenye uhitaji.
Gharama ya mradi ni Dola za Marekani 40,000 ambapo mpaka sasa, Mkandarasi (Kampuni ya Greenleaf Technology Solutions Limited) amekwishalipwa asilimia 70 ya gharama hizo, ambazo ni Dola za Marekani 28,000.
No comments: