COSTECH yamwezesha Mbunifu kutengeneza mashine ya kuchenjua dhahabu

 Mbunifu George Mkama  akiwaonesha mashine ambayo ameibuni kwaajili ya kuchenjulia dhahabu.

TANZANIA ni nchi ya nne kwa uchimbaji wa dhahabu Afrika huku ikitajwa kuwa na hazina kubwa ya madini mengine kama vile Almasi na Tanzanite.

Kwa miaka mingi, kabla sheria ya madini haijafanyiwa marekebisho bado, kwa mwaka 2017, Sekta hiyo ilikuwa inachangia chini ya asilimia tano kwenye pato la Taifa.

Kwa sasa mipango ya serikali ni kuifanya sekta ya madini  ichangie kwenye pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Ili kufanikisha mipango hiyo serikali imekuwa ikitekeleza mikakati kadhaa wa kadha ikiwemo na kuwapa wachimbaji wadogo maeneo ya kuchimba ambayo hapo mwanzo yalikuwa yakishikiliwa na wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi.

Serikali pia inawasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapa taarifa za kitafiti kuhusiana na madini na imewajengea vituo maalumu vya kuwafundisha uchimbaji wa madini kwanjia za kisasa.

Vituo hivyo viko kwenye mikoa saba yenye migodi ya mfano  yaani Kantente-Ushirombo na Rwamgasa (Geita), Itumbi-Chunya (Mbeya), Buhemba –Butihama (Mara), Mpanda (Katavi), Kange (Tanga), Kyerwa Syndicate (Kyerwa-Kagera) na Masakasa (Lindi).

Tangu ilipoanza kutumika sheria mpya ya madini mnamo mwezi Julai mwaka 2017, zaidi ya leseni mpya 7,000 za wachimbaji wa madini zimetolewa.

Licha ya leseni, tayari masoko 28 ya madini na vituo 28 vya ununuzi wa madini vimeanzishwa nchini kukabili utoroshaji na biashara haramu ya madini, hivyo kuongeza mapato ya wachimbaji wadogo na Serikali pia.

Tatizo kubwa linalowakabili wachimbaji wadogo ni ukosefu wa zana za kuchimbia unaosababishwa na kuwa na mitaji midogo ya kununua vifaa vya kisasa vya kuchimbia.

JITIHADA ZA KUTAMBUA TEKNOLOJIA
Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kupitia COSTECH ilizindua makisatu ili kuwatambua, kuendeleza na kuwawezesha wabunifu na wenye mawazo ya asili.

Makisatuni mashindano  yanayotoa jukwaa la wabunifu wazawa kutambua thamani walicho nacho katika kutatua kero na changamoto zilizopo kwenye jamii inayowazunguka.

Endapo kutakuwa na uwezekano, basi ubunifu walionao uwasaidie kuingiza kipato kwa kutatua kero za jamii.       

Mashindano ya makisatu yalianza mwaka jana (2019), takriban washiriki 60 walijitokeza na serikali ikasema wote wapewe ruzuku ili kuwatia moyo na kwa vile walikuwa wanaundakundi la kwanza linalotambulika.

Ili kusaidia wachimbaji wadogo hasa katika upatikanaji wa vifaa vya kuchenjua madini, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ilimuibua na kumuwezesha mbunifu George Mkama kutoka kata ya Kisesa, wilaya ya Magu jijini Mwanza ambaye amebuni mashine ya kuchenjua dhahabu.

Mkama amebuni mashine ya kuchenjua dhahabu, eneo muhimu kwa uchumi   wa Taifa.

Dhahabu ni madini yanayoongoza kwa kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni, iwapo uwekezaji utafanywa kwa kiasi kikubwa hasa na wachimbaji wadogo na wakati, itaongeza uzalishaji hivyo kukaribisha wawekezaji wengine mfano masonara, wakataji nakadhalika.

Kutokana na hali hiyo, jamii itapata mtaji wakuanzisha viwanda vya bidhaa nyingine kwa ajili ya kuihudumia sekta ya madini na jamii nzima kwa ujumla

Mashine hii inaweza kuwasaidia wachimbaji wadogo wadhahabu kwa kuongeza ufanisi wa kuchenjuaji na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za utafutaji wa madini ya dhahabu.

Mkama ambaye ni mtaalamu wa upasuaji miamba akiwa na uzoefu wa miaka mingi kwenye shughuli za uchimbaji madini anasema, kama wachimbaji wadogo watahamasishwa na kuhamasika kutumia mashine aliyoibuni, wana uhakika wa kupata asilimia 80 ya dhahabu iliyomo kwenye udongo uliochimbwa.

“Kwenye kila uzalishaji uliokuwa unafanyika, mashine hii ina uwezo wa kuongeza tija mpaka mara tatu. Inachuja dhahabu kwa kitambaa maalumu huku mashine ikitoa mitetemo inayoshusha dhahabu chini,” anasema Mkama.
Muonekano wa mashine ya kuchenjulia dhahabu.

Kwa sasa, wachimbaji wadogo hutumia makalai kuchuja dhahabu kutoka kwenye miamba iliyosagwa suala ambalo mbunifu huyu anasema hupoteza kiasi kikubwa cha madini hayo.

Mkama anaelezea kuwa upotevu wa dhahabu inayochenjuliwa kwa kutumia makalai, huanzia kwenye upotevu wa udogo wenye dhahabu mara tu unapochangaywa na maji kwani huwa hauchanganyiki kiurahisi hivyo udogo mwingine hupotea na madini yakiwa ndani yake.

“Mashine hii inaukoroga udongo kutokana na mitetemo yake. Kwa namna hii lazima dhahabu nyingi zaidi ibaki jambo linalomnufaisha mchimbaji,” anasema Mkama.

COSTECH iliwapa ruzuku wabunifu wote walioshinda kwenye mashindano ya MAKISATU 2019 kwa ajili ya kuendeleza bunifu zao.

Wabunifu wote waliohitaji kupata mafunzo ya kiufundi walipelekwa kwenye taasisi za mafunzo ya ufundi kwa ajili ya kuboresha bunifu zao.

UBUNIFU HUO UNAFAIDA GANI KWA JAMII
Mkama ni miongoni mwa wabunifu waliopelekwa kwenye chuo cha VETA tawi la Mwanza.

Mwalimu Lawrence Mashindano ambaye ni mtalamu wa mitambo katika chuo cha VETA tawi la Mwanza anaeleza kuwa mashine aliyo ibuni Mkama italeta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya madini hasa kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwani ina uwezo mkubwa wa kuchenjua madini hayo.

“Kwa kawaida, wachenjuaji wa makalai hupata kati ya asilimia 20 na 30 ya dhahabu iliyomo kwenye udongo walio uchimba. Mashine hii inauwezo wa kusaidia upatikanaji wa dhahabu kwa asilimia 80 hivyo inaongeza mavuno ya dhahabu.

“Lakini pia mashine hii haihitaji watu wengi ili kuiendesha hivyo itasaidia kupunguza idadi ya wafanyakazi kwenye kitengo cha uchenjuaji wa dhahabu,” anasema Mwalimu Mashindano.

Kwa ruzuku aliyopewa na COSTECH, Mkama anasema ataituimia kuandaa mashine tatu za kuchenjulia madini na kuzitawanya kwenye mikoa mitatu ili itumiwe na wachimbaji wadogo kwa ajili ya kuona ufanisi wake katika uchenjuaji wa dhahabu.

Anasema kwa wachimbaji wenye upungufuy wa wafanyakazi, mashine hiyo inawafaa zaidi kwani ina uwezo wa kutekeleza majukumu ya watu 15 kwa siku.

“Kazi inayofanywa na watu 18 watatakiwa wabaki watatu tu kwa ajili ya kuiendesha mashine hii. Wengine watakuwa hawana cha kufanya, hii itampunguzia mmiliki gharama za uendeshaji hivyo kumuongezea faida,” anasema Mkama.

No comments: