MZEE ALI HASSAN MWINYI ATIMIZA MIAKA 95, WATANZANIA WAMUOMBEA KWA MWENYEZI MUNGU AZIDI KUMPA AFYA NJEMA

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

LEO Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi anasherehekea siku yake ya luzaliwa kwa kufikisha umri wa miaka 95 akiwa mwenye afya njema.

Watanzania wa kada mbalimbali wamempongeza mzee Mwinyi kwa kufikisha umri huo huku wakiendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema na maisha marefu.Mzee Mwinyi ambaye ameliongoza Taifa la Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Pili ameendelea  kuwa Rais mwenye kupendwa na kukumbukwa na hasa kutokana na ile kauli maarufu ya Ruksa ambayo ilifungua fursa ya maendeleo kwa watanzania walio wengi.

Wakati leo Mzee Mwinyi ametimiza miaka 95 tangu kuzaliwa kwake ni vema tukambushana japo kwa ufupi historia yake. Mzee Mwinyi alizaliwa Mei 8 mwaka 1925 visiwani Unguja huko Tanzania Visiwani na alikuwa Rais kuanzia mwaka 1985 mpaka mwaka 1995.

Allipokea kijiti hicho cha urais kutoka kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza Hayati Julius Nyerere.Hata hivyo Mzee Mwinyi naye alikabidhi kijiti cha urais kwa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Mzee Benjamin Mkapa.

Historia ya Mzee Mwinyi inaonesha mbali ya kuwahi kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya pili,pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuanzia mwaka mwaka 1990 hadi mwaka 1996.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi kwa nyakati tofauti kwenye maandiko yao mbalimbali baadhi yao wanaeleza kuwa wakati wa urais wa Mwinyi, sera za Ujamaa zilianza kugeuzwa na kukawa nasera za soko huria.Ambapo masharti ya kuingiza bidhaa kutoka nchi za nje yalipunguzwa na uanzishaji wa biashara ya watu binafsi ulihamasishwa.

Mwaka wa 1991, uanzishaji wa vyama vingi uliruhusiwa.Hata hivyo inaelezwa kupitia historia yake kuwa kabla ya hapo alikuwa Rais wa Tatu wa Zanzibar kuanzia mwaka 1984 hadi 1985.

Aliyemtangulia ni Aboud Jumbe Mwinyi na aliyemfuatia ni Idris AbdulWakil Nombe.Pia kabla hajachaguliwa kuwa Rais, Mzee Mwinyi maarufu kwa jina la Mzee Ruksa alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamu Rais na kina wakati aliamua kujiuzulu nafasi hiyo na kisha kukaa kando lakini nyota yake iliibuka na kung'aa kiasi cha kuwa  Serikali ya Awamu ya Pili.

Mzee Mwinyi licha ya kuwa na umri mkubwa bado ameendelea kuwa na afya njema na amekuwa mstari wa mbele katika kufanya mazoezi na kwanyakati tofauti amekuwa akishiriki mbio mbalimbali ambazo zimekuwa zikiandaliwa na wadau mbalinbali.

Pia uwepo wake na hasa kwa kuzingatia uzoefu wa kuongoza nchi,Mzee Mwinyi ameendelea kuwa moja ya viongozi ambao Taifa letu la Tanzania linamtegemea katika kushauri na kutoa maelekezo kuhusu mambo mbalimbali pale ambapo anaombwa kutoa ushauri.

Hata hivyo historia ya Mzee Mwinyi ni ndefu ambayo huwezi kuielezea na kuimaliza, hivyo kilichoelezwa hapo juu ni sehemu ndogo tu ya historia yake.Pamoja na hayo Michuzi Media Group inayosimamia Michuzi Blog na Michuzi TV inaungana na Watanzania wote katika kumbukizi ya kuzaliwa ya Mzee Mwinyi na kubwa zaidi inamtakia maisha mema na yenye afya tele.
 
 Mzee Ali Hassan Mwinyi

No comments: