MIAKA MINNE NA MIEZI NANE YA MAFANIKIO, MBUNGE WA MANONGA SEIF KHAMIS GULAMALI AWASHUKURU WANANCHI


 Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
IKIWA Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba Mwaka huu, mafanikio katika Jimbo la Manonga Wilayani Igunga yameonekana dhahiri na hiyo ni baada ya jitihada zilizofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo Seif Khamis Gulamali katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kutekeleza ahadi alizoahidi hasa katika sekta ya Elimu na Afya.

Akizungumza na Michuzi Blog Gulamali amewashukuru Wananchi wa Manonga na Wilaya ya Igunga kwa ushirikiano walioonesha katika kuendeleza gurudumu la maendeleo Jimboni humo.

Gulamali amesema kuwa ni Miaka 4 na miezi 8 ya utumishi wa Ubunge akiwakilisha Jimbo hilo sambamba na kuhakikisha yale yote yaliyoahidiwa yanatimizwa kwa manufaa ya Wananchi kuhusiana na Sekta ya Elimu amesema kuwa;

"Tulikuwa hatuna Shule za kidato cha Tano hata moja na sasa Tunazo mbili, ambazo ni Mwisi na Ziba Sekondari na hii ni kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa Vijana wetu" amesema.

Aidha amesema kuwa baadhi ya maeneo hayakuwa Shule za Msingi na kufikia sasa Shule Mpya Tano zimejengwa na kusajiliwa ili watoto wapate elimu bora na katika mazingira rafiki.

Kuhusiana na Elimu ya Sekondari ambayo Gulamali amekua akiipigania kwa Kuhakikisha Wanafunzi wanafanya vyema zaidi amesema;
"Kata 6 zilikuwa hazina shule za Sekondari na hadi sasa tumejenga shule  mpya Saba na Tatu kati ya hizo zimepata Usajili huku shule nne zikiwa mbioni kusajiliwa" ameeleza Gulamali.

Vilevile amesema kuwa Awali hakukuwa na Motisha ya Kusomeshwa Bure kwa Wafaulu wote wa Kidato cha Nne kupitia utaratibu wa utoaji Motisha ya kusomesha Wanafunzi waliofanya vizuri Jimboni humo kwa Miaka Mitatu mfululizo zoezi hilo limefanyika huku alieleza utaratibu huo umeleta ushindani baina ya wanafunzi hali inayopelekea kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu.

"Ufaulu kwa shule za Sekondari ulikuwa chini na kwa sasa tumefikia kiwango kizuri zaidi na hiyo ni baada ya kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi na walimu pia" ameeleza.

Kuhusiana na sekta ya Afya jimboni humo Gulamali amesema kuwa awali hawakuwa na  kituo cha afya cha kisasa na kwa sasa kuna kituo bora cha Simbo kinachokidhi mahitaji ya Wananchi.

Pia amesema kuwa changamoto ya gari ya wagonjwa imetatuliwa baada ya kununua gari la kubeba wagonjwa pamoja na kuboresha huduma kwa Zahanati na Vituo vya afya.

Aidha Gulamali amesema kuwa hadi kufikia sasa Umeme unawaka kwa baadhi ya Vijiji vilivyokosa huduma hiyo na hiyo ni sambamba na kupelekwa kwa huduma ya Maji kwa Vijiji vichache vilivyokosa huduma hiyo.

" Katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumehakikisha huduma zote za msingi zinapatikana hata kwa baadhi ya vijiji vilivyokosa huduma ya mawasiliano ya simu kwa sasa wanapata huduma hiyo" amesema. 

Mbali na hayo Gulamali amesema kuwa wamefanikiwa kufufua kiwanda cha Pamba cha Manonga kilichokufa miaka 20 iliyopita na kimeanza kufanya kazi kwa miaka miwili sasa.

"Ni mengi tumefanya kwa wanamanonga na tumeweza kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano inayokwenda kwa kauli mbiu ya  Hapa kazi Tuu! Kwani hata uhitaji wa muda mrefu wa uwepo wa daraja la Manonga sasa upo katika ujenzi" ameeleza.

Kuhusiana na sekta ya michezo Mbunge huyo amesema kuwa licha ya kuwa chini hapo awali  sasa wapo katika kiwango cha juu zaidi na tayari wanaligi zinazoshirikisha Shule za Sekondari na Vijana kwa kila kitongoji Jimboni humo kwa Muda wote wa Miaka 5.

No comments: