HOTUBA YA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/2021
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA
HOTUBA FUPI (TALKING NOTES)
YA
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA (MB.),
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/2021
-
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika; kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ambayo ilichambua Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara Fungu 44 (Viwanda) na Fungu 60 (Biashara) tarehe 24 na 25 Machi, 2020 Jijini Dodoma, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu sasa likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mipango na Bajeti kwa Mwaka 2019/2020. Aidha, naliomba Bunge lako tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, naomba Hotuba yangu yote iliyowasilishwa kwa Waheshimiwa Wabunge iweze kuingia katika kumbukumbu za Bunge (Hansard) kama ilivyo.
Mheshimiwa Spika; awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na baraka katika majukumu niliyokasimiwa. Kwa namna ya pekee namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Waziri na kunipa majukumu yanayobeba ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda. Nampongeza kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC na namna anavyoshughulikia masuala ya biashara katika nchi za SADC na EAC ikiwa ni pamoja na kuomba kufutiwa madeni kwa nchi za Afrika katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa COVID -19. Nampongeza pia kwa namna anavyotuongoza kwa ujasiri na misingi imara, yenye kusheheni uzalendo na mapenzi kwa nchi yetu. Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; na Mheshimiwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kwa jinsi wanavyomsaidia Mhe. Rais kusimamia ipasavyo misingi ya utaifa wetu kupunguza pengo la walionacho na wasiokuwa nacho, kujenga Tanzania yenye kutoa fursa za uhakika za kujiletea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika; napenda kuchukua nafasi hii, kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika kwa umakini wenu katika kuliongoza na kulisimamia Bunge letu. Pia, naipongeza na kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Suleiman Ahmed Saddiq, Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Makamu wake Mheshimiwa Kanali Mstaafu Ali Khamis Masoud, Mbunge wa Jimbo la Mfenesini na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati. Ushauri na maelekezo yao yamekuwa chachu muhimu sana, katika mageuzi ya kifikra na kiutendaji ya Wizara, na hivyo kuchochea kasi ya maendeleo ya viwanda na biashara nchini.
Mheshimiwa Spika; kwa namna ya pekee, niwashukuru watangulizi wangu Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini na Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, waliokuwa mawaziri wa Viwanda na Biashara. Nikiri kuwa misingi waliyoweka imeendelea kuwa chachu muhimu katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara nchini. Aidha, nimshukuru Katibu Mkuu mstaafu Prof. Joseph Buchweshaija kwa ushirikiano alionipa kipindi nilichofanya naye kazi na nimkaribishe Prof. Riziki Shemdoe Katibu Mkuu wetu mpya. Nampongeza Prof. Shemdoe kwa nguvu na kasi aliyokuja nayo kwenye Wizara.
Mheshimiwa Spika; niwapongeze pia Mhe. Mussa Zungu, Mbunge wa Ilala, Mhe. Geogre Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe na Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi kwa kuaminiwa na Mhe. Rais na kuteuliwa kuwa Mawaziri. Naahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kutimiza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika; naungana pia na Waheshimiwa Wabunge kutoa pole kwa familia zilizoondokewa na Wabunge wenzetu ambao ni Mheshimiwa Rashid Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini; Mheshimiwa Dkt. Getrude Rwakatare aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum; Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Sumve; na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustino Mahiga aliyekuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Spika; naomba kutumia fursa hii pia kuwashukuru viongozi na watendaji wote wa sekta binafsi, kwa michango yao katika kuendeleza Sekta za Viwanda na Biashara. Nawashukuru TPSF, CTI, TCCIA, TNBC, CEO Roundtable, JWT na wengine wengi. Tunaendelea kuwategemea kama nguzo na mihimili ya kushirikiana katika kuendeleza viwanda na biashara na kuchochea uchumi wetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika; hotuba hii ya Bajeti ninayoiwasilisha leo ni matokeo ya uratibu na ushirikiano mzuri wa viongozi wenzangu katika Wizara, akiwemo Naibu Waziri Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa; Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe; Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Ludovick Nduhiye; Wakuu wa Idara, Vitengo, Taasisi na Watumishi wote wa Wizara na Taasisi. Napenda kuwashukuru na kuwapongeza kwa kujituma, na kuonesha daima utayari wa kuboresha mbinu na mikakati ya kisekta kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika; nawapongeza na kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Karagwe kwa kuendelea kunipa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kitaifa na ya Jimbo. Nawapongeza kwa namna wanavyojibidiisha katika kujiletea maendeleo. Aidha, ninawaahidi kwamba nitaendelea kutetea maslahi yenu hapa Bungeni na hata nje ya Bunge ili kuhakikisha Karagwe inaendelea kushamiri na kuleta matokeo ya mtu mmoja mmoja, Wilaya, Mkoa na hatimaye kuongeza mchango wake kwa Taifa letu. Kipekee namshukuru sana mke wangu mpendwa Jennifer Bashungwa, watoto na familia yangu kwa upendo wao, uvumilivu na maombi yao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ya kitaifa.
Mheshimiwa Spika; naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuomba ushiriki wa dhati wa kila Mtanzania katika kupambana na virusi vya KORONA ili kulinda nguvukazi ya Taifa. Nawaomba sana Watanzania wote kuwa kila mmoja, kila familia na jumuiya zote nchini, kutambua kuwa usalama wetu hutegemea jitihada ya kila mmoja kujilinda na kumlinda mwenzake.
Mheshimiwa Spika; katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa KORONA, Kampuni ya Kilombero Sugar ilichangia jumla ya lita 30,000 za Ethanol kwa ajili ya kutengeneza vitakasa mikono ambapo Wizara ya Afya ilipewa lita 20,000 na kiasi kilichobaki cha kita 10,000 zilipewa Taasisi za SIDO na TIRDO.
Mheshimiwa Spika; hadi sasa tayari Viwanda na Makampuni 65 yanazalisha vitakasa mikono vyenye ubora unaokubalika na TMDA. Kwa Wastani Viwanda hivyo vinatumia kiasi cha Ethanol kwa mwezi kisichopungua lita 2,548,951. Umoja wa wenye Viwanda Vya Dawa na Vifaa Tiba (TMPA) kwa ujumla wao (viwanda vikubwa 4) vinazalisha vitakasa mikono kwa mwezi lita zipatazo 900,000 na viwanda vya kati na vidogo vipatavyo 61, vinazalisha lita zipatazo 2,745,000 za vitasa mikono kwa mwezi, na kufanya jumla ya uzalishaji vitakasa mikono kuwa lita 3,645,000 kila mwezi. Kati ya hizo TIRDO huzalisha lita 90,000 kwa mwezi na SIDO huzalisha lita 18,000.
Mheshimiwa Spika; kwa sasa tuna viwanda viwili vya kutengeneza barakoa aina ya Surgical Masks ambavyo ni Pristine na Five Star. Viwanda hivyo vina uwezo uliosimikwa wa kutengeneza barakoa 150,000 kwa siku na uwezo wa uzalishaji kwa sasa ni barakoa 30,000 kwa kiwanda cha Pristine na barakoa 40,000 kwa kiwanda cha Five Star kwa siku. Aidha, barakoa za vitambaa (cloth masks) kwa ajili ya kujikinga, tayari jumla ya viwanda 123 vimeitikia wito wa kutengeneza barakoa hizo ambapo kati yao viwanda vikubwa ni 13 na vidogo 110. Wizara inaendelea kuhamasiha viwanda vya ndani vya nguo kutengeneza barakoa kwa wingi kuwasaidia watanzania na mapambano ya KORONA. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zetu kuhamasisha na mafundi vyerehani kwenye kila kijiji kushona barakoa za nguo kuwasaidia wananchi vijijini. TMDA na TBS toeni mafunzo kupitia vyombo vya habari na wapeni ushirikiano Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika majukumu haya.
-
MAFANIKIO YA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA KATIKA AWAMU YA TANO
Mheshimiwa Spika; katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali iliweka nguvu kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015 – 2020. Umakini wa utekelezaji Ilani ya CCM umehamasisha na kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa 2025.
-
Kukidhi Mahitaji ya Ndani ya Bidhaa za Viwandani
Mheshimiwa Spika; Nchi yetu imejitosheleza katika baadhi ya bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini. Saruji (uzalishaji halisi ni tani Milioni 7.4 na mahitaji halisi tani Milioni 4.8); marumaru (uzalishaji halisi ni mita za mraba Milioni 32.4 na mahitaji halisi ni wastani wa mita za mraba Milioni 30).
-
Ujenzi wa Viwanda Vipya
Mheshimiwa Spika; Serikali inaendelea kuhamasisha uendelezaji na ujenzi wa viwanda nchini. Kutokana na uhamasishaji huo, jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa kati ya mwaka 2015 hadi 2019. Viwanda hivyo vinajumuisha, viwanda 201 vikubwa, 460 vya kati, 3,406 vidogo; na 4,410 vidogo sana.
Mheshimiwa Spika; Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imetoa ajira kwa wingi kwa Watanzania ambapo kwa sasa inaajiri zaidi ya Watanzania 8,000,000. Ajira hizo zimewezesha wananchi kujiongezea vipato na kutatua changamoto zao za kijamii na kiuchumi. Hii imetokea kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kupunguza mamlaka za udhibiti na kufanya watanzania wengi kujiajiri na kutekeleza azma ya ujenzi wa viwanda nchini ambapo takribani asilimia 99 ya viwanda vyote nchini vipo chini ya sekta hiyo.
-
Uzalishaji wa Dawa na Vifaa Tiba
Mheshimiwa Spika; Sekta ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba kwa sasa ina jumla ya viwanda 15 ambapo viwanda 12 vinatengeneza dawa za binadamu, viwanda 2 ni vya dawa za mifugo na kiwanda 1 kinatengeneza vifaa tiba. Kwa sasa viwanda vya dawa vinazalisha chini ya asilimia 12 ya uwezo wake uliosimikwa na Serikali imekuwa ikiwawekea wawekezaji mazingira wezeshi ili kufikia asilimia 60 ya uwezo uliosimikwa. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka vivutio vya uwekezaji kwa lengo la kuhamasisha wawekezaji wa ndani na Nje ya Nchi kwa kuondoa VAT kwa vifungashio vya dawa zinazozalishwa nje na ndani ya nchi; kushusha kodi ya mapato kutoka asilimia 30 hadi 20 kwa mwekezaji mpya ndani ya miaka mitatu ya mwanzo; na kuweka upendeleo maalum kwa ununuzi wa dawa zinazozalishwa na viwanda vya ndani kupitia MSD.
-
Uzalishaji wa Sukari
Mheshimiwa Spika; makadirio ya uzalishaji wa sukari kwa msimu wa mwaka 2019/2020 yalikuwa tani 345,296 kwa viwanda vya ndani sawa na asilimia 73.46 ya kiasi cha sukari inayokadiriwa kwa matumizi ya kawaida. Aidha, hadi kufikia mwezi Aprili, 2020 uzalishaji wa sukari nchini ulikuwa jumla ya tani 298,949, wakati mahitaji ya sukari kwa mwaka ni wastani wa tani 635,000. Kati ya mahitaji hayo, tani 470,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na tani 165,000 kwa matumizi ya viwandani. Makadirio hayo yametokana na ukweli kwamba mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida kwa mwezi ni wastani wa tani 38,000. Sababu zilipelekea kushuka kwa bei ni pamoja na mvua nyingi kipindi cha vuli na kupunguza kiwango cha sukari kwenye miwa na taratibu za usafirishaji ambazo zimesababishwa na ugonjwa wa KORONA ulioenea duniani.
Mheshimiwa Spika; kwa sasa Serikali imetoa tamko kuhusu uuzaji wa sukari. Matamko hayo ni pamoja na sukari iuzwe kwa kuzingatia bei elekezi na endapo wafanyabiashara hawatazingatia maelekezo hayo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Napenda kuwapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao tumeshuhudia jitihada zao katika kusimamia tamko la bei elekezi kwa lengo la kuwalinda walaji. Aiidha, niwaombe Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kwa kutumia kamati za ulinzi na usalama kuendelea kusimamia bei za ukomo zilizotangazwa na Serikali ili wananchi waweze kupata bidhaa hii muhimu kwa bei nafuu.
-
Uendelezaji Maeneo Maalum ya Uwekezaji na Mapato Kutokana na Uwekezaji Chini ya EPZA/SEZ
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia EPZA, imefanya tafiti tatu kutathmini tija inayopatikana kutokana na kampuni zilizowekeza chini ya EPZA na tafiti hizo zimeonesha uwepo wa tija katika uwekezaji wa maeneo hayo. Hadi kufikia Desemba 2019, chini ya BWM-SEZ, mauzo ya Nje ya Nchi yameingizia nchi Tsh. Bilioni 293.56 (USD 127.64); matumizi mengine ya kuendeshea biashara yameingiza Tsh. Bilioni 146.58 (USD 63.73); kodi na tozo mbalimbali zilizolipwa kupitia TRA zimeingiza Tsh. Bilioni 17.24 (USD 7.50); na zimepatikana ajira za moja kwa moja viwandani zipatazo 3,000.
Kutokana na manufaa hayo, Wizara kupitia EPZA, imekuwa ikihamasisha ushiriki wa Serikali za Mikoa katika uendelezaji wa Maeneo ya SEZ ili kuiwezesha Mikoa husika kutumia Maeneo ya SEZ kama chanzo cha mapato na mbinu mojawapo ya kuchochea shughuli za kiuchumi katika mikoa husika. Hadi sasa, mikoa ya Arusha, Geita, Mwanza, Kigoma na Songwe imetenga maeneo yatakayoendelezwa kama Maeneo Maalum ya Kiuchumi. Kupitia uhamasishaji huo, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 EPZA imesajili kampuni sita (06) na hivyo kufanya viwanda vilivyo chini ya EPZA kuongezeka kutoka viwanda 163 hadi viwanda 169 vikichangia ongezeko la mtaji unaokadiriwa kutoka Tsh. Tilioni 5.41 (USD Bilioni 2.35) hadi Tsh. Tilioni 5.47 (USD Bilioni 2.38). Mauzo ya nje yanakadiriwa kuongezeka kutoka Tsh. Trilioni 5.17 (USD Bilioni 2.25) hadi takriban Tsh. Trilioni 5.21 (USD Bilioni 2.27) na fursa za ajira za moja kwa moja kutoka 56,442 hadi 57,342.
Mheshimiwa Spika; utekelezaji wa mradi wa Kurasini ni kuliendeleza eneo hilo kama Kituo cha Biashara na Ugavi -“Trade and Logistic Centre”. Serikali kupitia Mamlaka ya EPZ imedhamiria kuliendeleza eneo la kituo cha Biashara cha kurasini kama Soko la Mazao Mchanganyiko kwa kuanzia na zao la chai, kahawa na mazao ya bustani.
Umuhimu wa kutekeleza wazo la kujenga kituo cha Biashara na Ugavi -Kurasini kwa ajili ya mazao ya kilimo ni kuwezesha Sekta ya kilimo kuchangia vizuri zaidi katika pato la Taifa kwa kuwezesha uongezaji wa thamani ya mazao na biashara ya mauzo ya nje kufanyika. Baada ya kilimo shughuli zinazofuata ni uchakataji (viwanda) na hatimae mauzo (biashara).
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia NDC imekamilisha upimaji wa eneo la TAMCO ambapo jumla ya ekari 201.63 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na miundombinu. Hadi sasa viwanda viwili (02) vinavyofanya kazi vimeajiri watumishi 200 na ujenzi wa viwanda vipya eneo la TAMCO kibaha vinakadiriwa vitaajiri watumishi 21,220 ajira za kudumu. Madhumuni ya Serikali ni kuwa na Industrial Park nyingi nchini ama kupitia EPZA ama NDC ama Halmashauri zetu ili wafanyabishara na wawekezaji wenye mtaji na business plan wakute tayari eneo lina maji, umeme na huduma nyingine muhimu.
-
Mikopo kwa Wajasiriamali
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia SIDO imefanikiwa kuchochea uanzishwaji wa shughuli za kiuchumi kwa kutumia mikopo inayotolewa na Skimu ya Ukopeshaji kwa Wajasirimali (SME Credit Guarantee Scheme-CGS) na Mfuko wa Wafanyabiashara Wananchi (NEDF). Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Machi 2020, mtaji wa Mfuko wa NEDF umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 6.429 Machi 2016 hadi Bilioni 8.65 Machi, 2020 ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 2.22. Ongezeko hilo limetokana na riba inayopatikana kutokana na fedha inayojizungusha (Revolving Fund) kupitia mikopo hiyo. Aidha, jumla ya wajasiriamali 17,696 wakiwemo wanawake 8,933 na wanaume 8,721 walipatiwa mikopo iliyowezesha kupatikana jumla ya ajira 47,180. Kupitia mifuko hiyo, jumla ya viwanda vipya 437 vilianzishwa na kutoa ajira 1,481. Jitihada hizo ni kichocheo na chachu kubwa kwa huduma na taasisi za fedha ambazo nazo hutoa huduma ya mikopo.
Mheshimiwa Spika; mwezi Februari 2020, yalisainiwa makubaliano kati ya SIDO, VETA, AZANIA BANK, NSSF na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ya kuanzisha programu ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali waliohudumiwa na SIDO na wahitimu wa VETA kupitia Benki ya AZANIA. Makubaliano hayo yalifanyika chini ya uratibu wa NEEC yanatoa nafasi kwa SIDO na VETA kuwapeleka wajasiriamali na wahitimu Benki ya AZANIA kuomba mikopo ya viwanda ya kuanzia Tshs milioni 8 hadi milioni 500. Fedha zitakazokopeshwa kiasi cha TSh. Bilioni tano (5) zimetolewa na NSSF kwa mkopeshaji ambaye ni Benki ya AZANIA.
Mwongozo wa utekelezaji wa programu unaandaliwa ndipo utekelezaji wa programu hiyo uanze. Wizara inakusudia kuweka msukumo mkubwa wa program hiyo ili iwafikie wajasiriamali wengi nchini na wapate kunufaika. Tunawashukuru NSSF na AZANIA Bank na natoa wito kwa mabenki yote nchini na mifuko ya jamii kuiga mfano huu ili kuinua wajasiriamali nchini.
-
Majengo na Maeneo kwa Shughuli za Wajasiriamali
Mheshimiwa Spika; Serikali imefanikiwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wajasiriamali kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Jitihada hizo zimewezesha ujenzi wa majengo viwanda (Industrial Shades) 12 katika mitaa ya viwanda ya SIDO iliyopo mikoa ya Dodoma (3), Manyara (3), Kagera (1), Mtwara (1) na Geita (4). Jumla ya viwanda 29 vimeweza kusimikwa katika majengo hayo na hivyo kuzalisha ajira 648. Kutokana na umuhimu huo, Wizara inaendelea na ujenzi wa majengo ya viwanda katika mikoa mingine kwa kuanzia mikoa ya Kigoma, Mtwara na Ruvuma ambapo SIDO imekamilisha upembuzi yakinifu wa majengo matatu pamoja na michoro ya usanifu (architectural drawings) katika mikoa ya Mtwara (2) na Kigoma (1) na ujenzi umeanza.
Mheshimiwa Spika; ukamilishaji wa majengo viwanda (industrial sheds) unategemewa kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vipya saba vitakavyotengeneza ajira 76. Vilevile, Serikali imefanikisha kusogeza karibu huduma za kusaidia na kuhamasisha wananchi kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kujenga ofisi nne (4) za SIDO katika mikoa mipya ya Simiyu, Katavi na Geita.
-
Fursa za Biashara na Masoko ya Kikanda
Mheshimiwa Spika; katika kutumia fursa za masoko ya kikanda, Wizara imefanikisha kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa na huduma kwenye masoko hayo yanayotoa fursa za upendeleo maalum (preferential market access). Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwenda kwenye masoko ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Mfano, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2018 Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwa wastani wa USD Milioni 288.04.
-
Uboreshaji Mazingira ya Biashara Nchini
Mheshimiwa Spika; katika kuboresha mazingira ya biashara nchini, Wizara imefanikiwa kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara Nchini – BLUEPRINT. Mpango huo umewezesha maboresho ya tozo 173 ambapo tozo 163 zimefutwa na tozo kero 10 zimepunguzwa kiwango. Kati ya tozo zilizofutwa, 114 ni za Sekta ya Kilimo na Mifugo, 5 za OSHA, 44 za TBS, Mamlaka za Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Utalii, Maji, Uvuvi na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA. Aidha, tozo zilizopunguzwa ni za GCLA. Mpango huo umewezesha kuhamisha jukumu la usimamizi wa masuala ya chakula kutoka iliyokuwa TFDA kwenda TBS, ili kuondoa muingiliano wa majukumu. Maboresho hayo yamesaidia kuondoa urasimu na kupunguza gharama za kufanya biashara.
-
Utoaji Huduma za Kieletroniki kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali Nchini
Mheshimiwa Spika; kutokana na kufutwa kwa tozo hizo, usajili wa usalama mahali pa kazi (workplace) umeongezeka kutoka 16,457 mwaka 2019 ikilinganishwa na mahala pa kazi 11,963 mwaka 2018. Aidha, BLUEPRINT imeandaliwa Mpango Kazi (Blueprint Action Plan-BAP) ili kuongoza utekelezaji wake. Sambamba na hilo, Serikali inaendelea na maandalizi ya kutunga Sheria ya Uwezeshaji Biashara ya mwaka 2020 (Business Facilitation Act, 2020), ili kuipa nguvu ya kisheria misingi ya maboresho iliyobainishwa katika Blueprint. Rasimu ya Waraka wa Sheria hiyo imekwishawasilishwa kwenye ngazi za maamuzi Serikalini.
Mheshimiwa Spika; Wizara inafanya kila linalowezekana kuboresha utendaji wa BRELA na mifumo yake ya Usajili wa Majina ya Biashara, Makampuni, Alama za Biashara na Huduma, Hataza, Leseni za Viwanda na Leseni za Biashara kwa njia ya Mtandao. Hadi kufikia Machi, 2020, Wakala imesajili Makampuni 7,549, Majina ya Biashara 12,627, Alama za Biashara na Huduma 1,970, Hataza 55, Leseni za Viwanda 200 na Leseni za Biashara 9,927.
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia BRELA imekusanya taarifa za bidhaa mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali zaidi ya ishirini (20) za kutoka Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tayari taarifa za bidhaa zaidi ya 18 zinazosafirishwa nje ya nchi (Export) na zaidi ya bidhaa 8 zinazoingizwa nchini (Import) zimekwishakusanywa na kuingizwa kwenye Mfumo.
-
Kuwaunganisha Wazalishaji, Wasindikaji na Wafanyabiashara na Masoko ya Ndani na Nje ya Nchi
Mheshimiwa Spika; Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Taasisi za Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) na AGRA inaandaa mkakati wa namna bora ya kufungamanisha Sekta za Kilimo na masoko kwa mazao ya kimkakati yatakayozalishwa nchini. Mkakati huo unalenga: Kuunganisha wazalishaji ikiwemo wakulima na wasindikaji wa ndani na nje ya nchi; Kujenga na kuhamasisha uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya uwezeshaji badala ya kudhibiti biashara kwa Taasisi na Mamlaka za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali na leseni za biashara; na Kuweka vivutio kwa sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika; Wizara kupitia TanTrade imeratibu tafiti za kutambua fursa za masoko ili kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje. Kipaumbele ni katika masoko ya: China (Madini, Vito, Nyama, Tumbaku, Korosho na Muhogo); India (Mikunde, Korosho, Ngozi na Nafaka); Ulaya (Matunda, Mbogamboga, Asali, Kahawa na Korosho); na Nchi za EAC (nafaka, bidhaa za ujenzi, bidhaa za ngozi, bidhaa za viwandani na vyakula vya mifugo); na Nchi za SADC (Madini, nafaka, bidhaa za viwandani, bidhaa za ujenzi). Aidha, mikutano na misafara ya kibiashara iliyoratibiwa ilizingatia na kutumia matokeo ya tafiti hizo na hivyo kufanikisha kutumia fursa hizo za biashara.
-
Kuimarika kwa Biashara za Mipakani
Mheshimiwa Spika; Serikali imewezesha kuanzishwa kwa Vituo kumi vya Mipakani. Aidha, kati ya hivyo Vituo sita vinafanya kazi kwa mujibu wa utaratibu wa OSBPs, Vituo viwili (Hororo/Lungalunga; na Sirari/Isebania) ujenzi wake umeshakamilika vinasubiri kuzinduliwa rasmi. Vituo viwili vilivyobaki (Kasumulo/Songwe; na Mugina/Manyovu) viko kwenye hatua za awali za ujenzi. Vilevile, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na masoko ya kimkakati kwa ajili ya kukuza biashara na mauzo nje ya nchi kwa maendeleo ya wananchi wake na Taifa kwa ujumla. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuanzisha, kuboresha na kuendeleza masoko ya kimkakati ya mipakani ya Nkwenda na Murongo (Kyerwa), Kabanga (Ngara), Kahama (Kahama), Remagwa (Tarime) na Bweranyange (Karagwe) ili kurasimisha ufanyaji biashara. Kwa sasa Wizara inaratibu Mradi wa Ujenzi na Uboreshaji wa Masoko ya Mipakani ili kuhakikisha wananchi waishio mipakani wananufaika ipasavyo. Jitihada hizo zimekwenda sambamba na mpango wa Wizara wa ujenzi wa masoko ya kimkakati mipakani.
-
Kuhuisha Soko la Biashara ya Zao la Tumbaku
Mheshimiwa Spika; kipekee naomba nimpongeze Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali anayoingoza kwa namna alivyosimama imara na kuweka msimamo thabiti dhidi ya mifumo ya kumyonya mkulima katika mazao mbalimbali na hususan korosho, pamba, kahawa na mazao mengine. Wizara itahakikisha kupitia taasisi zake ikiwemo FCC inasimamia na maeneo mengine kuharibu mifumo ya aina hiyo iliyowekwa na wafanyabishara wasio waaminifu kwa lengo la kumnyonya mkulima. Mheshimiwa Rais ni mfano wa kuigwa katika utendaji wetu hasa katika kuhakikisha haki za wakulima na wananchi wanyonge zinalindwa. Na hii inadhihirisha utayari wake katika kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa kujituma na hivyo kuakisi kauli yake ya “HAPA KAZI TU”.
Mheshimiwa Spika; Wizara imefanikiwa kuhuisha soko la zao la Sekta ya Tumbaku baada ya Serikali kufikia muafaka na wanunuzi wakuu wa zao hilo kuhusiana na madai ya ukiukwaji wa taratibu za ushindani. Mahauri dhidi ya allince one, Alliance one international na ATTT yameshamalizika kwa suluhu na kufungwa ili wadau hao waendelee na shughuli zao katika kuendeleza sekta ya tumbaku. Aidha, mashuri yaliyokuwa yanaikabili TLTC, TTPL, ULT na ATTT nayo pia yamemalizwa kwa suluhu.
Hadi sasa mchakato wa kumaliza kwa suluhu mashauri yanayowakabili kampuni ya JTI Leaf Services Limited na JT International uko hatua za mwisho. Kutokana na mwenendo huu wa suluhu kampuni ya JTI Leaf Services Limited katika mpango wake wa ununuzi imethibitisha kununua tumbaku yenye thamani ya USD Milioni 12.6 kwa mwaka 2019/2020, USD Milioni 14.1 kwa mwaka 2020/2021, USD Milioni 15 kwa mwaka 2021/2022 na USD Milioni 15.5 kwa mwaka 2022/2023.
-
Miradi ya NDC
Mheshimiwa Spika; Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) inatekeleza miradi mikubwa mitatu ambayo ni; mradi wa kuunganisha na kuuza matrekta aina ya URSUS (Ubia wa NDC na kampuni ya URSUS ya Poland); mradi wa ujenzi na uendeshaji wa kiwanda cha viuadudu (Ubia wa NDC na kampuni ya LABIOFAM ya Cuba); na mradi wa makaa ya mawe (Ubia wa NDC na kampuni ya Intra Energy Tanzania Ltd na kuendesha kampuni ya TANCOAL Energy Ltd).
Mheshimiwa Spika; utekelezaji wa miradi hiyo umekabiliwa na changamoto mbalimbali kiasi cha kuathiri matokeo chanya yaliyotarajiwa na Serikali. Aidha, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo. Mwezi Machi,2019 Wizara kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali tumeanza kufanya mapitio, tathmini na uchunguzi wa miradi hiyo, ikiwemo kuunda timu za Serikali zijadiliane na timu ya Serikali ya Poland kwa mradi wa matrekta ya URSUS; Serikali ya Cuba kwa mradi wa viuadudu uliopo Kibaha; na timu ya kampuni ya Intraenergy Tanzania kwa ajili ya mradi wa makaa ya mawe ya ngaka (TANCOAL).
Mheshimiwa Spika; timu hizo zimeshaundwa na zinatarajia kuanza vikao vyake hivi karibuni. Kutokana na changamoto za CORONA tunatarajia vikao hivyo vitafanyika kwa njia ya Video Conference. Wizara inaamini kuwa makubaliano katika majadilino hayo yataleta matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi hiyo na inakuwa na manufaa zaidi kiuchumi na kijamii kwa Taifa, hususani katika ujenzi na uendelezaji wa sekta ya viwanda nchini.
-
Mikataba na Itifaki na Marekebisho ya Sheria
Mheshimiwa Spika; Wizara iliandaa na kuwasilisha Waraka wa Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba wa Marrakesh ulionzisha Shirika la Biashara la Dunia ili kufanya Mkataba wa Uwezeshaji Biashara (Trade Facilitation Agreement) kuwa sehemu rasmi ya mikataba ya WTO. Tayari waraka huo umekwisharidhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Hati ya Kuridhia (Instrument of Ratification) ya Itifaki hiyo imekwishasainiwa na kuwasilishwa WTO. Vilevile, Itifaki ya Marrakesh inayolenga kuwezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu, ulemavu unaofanya mtu kushindwa kusoma wa mwaka 2013 iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tayari, Hati ya Itifaki hiyo imesainiwa na kuwasilishwa WIPO. Tunashukuru Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Rais kwa kuridhia na kufanikisha Mikataba na Itifaki hizo.
-
MWELEKEO NA VIPAUMBELE VYA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA
-
Mwelekeo wa Sekta ya Viwanda na Biashara
-
Mheshimiwa Spika; mtazamo na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kuhusu maendeleo ya viwanda na biashara nchini, unalenga kujenga uchumi wa viwanda utakaowawezesha Watanzania kufikia na kunufaika na uchumi wa kati ifikapo 2025. Hatua hiyo itawezesha Watanzania kutumia fursa za kiuchumi na kijamii katika mifumo iliyoboreshwa na inayozingatia haki na utawala bora. Ni dhamira ya nchi yetu kumfanya kila Mtanzania kuwa na maisha bora na kunufaika na rasilimali na fursa zilizopo na zinazojitokeza.
-
Kuhamasisha Uendelezaji na Matumizi ya Bidhaa za Ndani
Mheshimiwa Spika; kuthamini rasilimali na bidhaa za ndani ni ukombozi muhimu wa kiuchumi kwa Taifa lolote. Mifano hai ni nchi ya Japan na China ambazo wananchi wake wamejijengea utamaduni wa kuthamini bidhaa zinazozalishwa katika uchumi wao. Hivyo, Wizara itaendelea kuhamasisha uimarishaji wa ubora na matumizi ya bidhaa za ndani, nguvukazi na malighafi za ndani ili kuleta ufungamanisho wa sekta katika kujenga uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TanTrade inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani kupitia kauli mbiu ya Nunua Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania (Buy Tanzania, Build Tanzania). Mbinu hiyo ni muhimu sana katika kipindi hiki cha ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuimarisha viwanda vya ndani na kutumia Kiswahili katika bidhaa.
-
Kuimarisha SIDO
Mheshimiwa Spika; kwa kutambua umuhimu na mchango wa Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo katika uchumi na hususan ujenzi wa viwanda, Serikali itachukua hatua za makusudi kuimarisha ujasiriamali nchini. Kipaumbele kitakuwa katika kuimarisha taasisi ya SIDO kwa kupitia upya muundo wake na kuijengea uwezo ili iweze kubeba ipasavyo dhamana ya uendelezaji wa viwanda vidogo na biashara ndogo inayowabeba Watanzania walio wengi. Jitihada hizo zitaenda sambamba na kuendelea ujenzi wa shades katika mikoa yote nchini ili manufaa yalioyoonekana ya ajira na uongezaji thamani wa mazao, na kuongeza ushindani katika soko yasambae nchi nzima.
Mweshimiwa Spika; Wizara pia itaweka mkazo na umuhimu katika upatikanaji wa teknolojia, kuongeza miundombinu ya uzalishaji (Industrial shades) ili kuwawezesha wajasiriamali kupata mahali pa kufanyia uzalishaji, na kuweza kuhudumiwa kirahisi na taasisi mbalimbali zikiwemo za udhibiti wa ubora wa bidhaa, taasisi za fedha na mafunzo muafaka. Juhudi za kuimarisha jasiriamali nchini zitaenda sambamba na kuimarisha SIDO ili imudu kutoa huduma bora na zenye kuleta tija katika uzalishaji wa bidhaa, huduma na ufanyaji biashara.
-
Kuvilinda Viwanda na Biashara za Nchini
Mheshimiwa Spika; uchumi himilivu unaotabirika na shindani unatokana na jitihada za kuujenga, kuuendeleza na kuulinda. Kujilinda isitafsiriwe kuwa ndiyo kujitenga kiuchumi na nchi nyingine, na wala siyo dhambi, kwani hata nchi zilizoendelea kiuchumi duniani mbinu mbalimbali zinaendelea kutumika kwa njia tofauti. Hivyo, sera, sheria na mikakati ya kisekta itaendelea kuhakikisha kuwa kunakuwepo ushindani wa haki ili kulinda viwanda na biashara nchini. Aidha, tutaendelea kulinda haki za msingi za walaji kwa kuweka utaratibu wa kisheria utakaotaka wawekezaji, wenye viwanda na wafanyabiashara katika mazao, bidhaa na huduma kutotumia nguvu ya soko isivyotakiwa na kusababisha kuwakandamiza wanyonge.
Mheshimiwa Spika; ili kuongeza nguvu za utafutaji wa fursa za masoko ya nje, Wizara inafanya uchambuzi wa kina wa kuona umuhimu wa kuhuisha na kurejesha Waambata wa Biashara (Trade Attachee) katika ofisi za Balozi zetu zilizo nje ya nchi, ili kuweka mfumo wa kufanya tathmini na utafiti wa mahitaji ya soko la bidhaa zinazozalishwa nchini. Tathmini na tafiti hizo zitatoa picha ya mahitaji ya soko la nje na kuwezesha wazalishaji wa bidhaa za ndani kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko la nje.
Mheshimiwa Spika; utoaji huduma bora kwa wananchi kwa kiwango kinachoridhisha ni lengo kuu la mabadiliko ya kiutendaji ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayapa kipaumbele. Hivyo, mwelekeo wetu ni kuhakikisha kuwa taasisi za kisekta zinajielekeza katika kutoa huduma kwa kiwango kinachokidhi matarajio ya wananchi. Wizara yangu na taasisi zake zitaongeza ubunifu katika utendaji kazi kwa tija na kutoa huduma kwa weledi ili kuchochea ufanisi katika Sekta ya Viwanda na Biashara na hatimaye kuongeza Pato la Taifa.
-
Uimarishaji wa Taasisi za Udhibiti na Maendeleo ya Teknolojia na Uwekezaji Nchini
Mheshimiwa Spika; katika kuendeleza uchumi wa viwanda, Serikali inaimarisha taasisi zake ili ziweze kukidhi na kuhimili mahitaji ya maendeleo na ujenzi wa viwanda nchini. Wizara inajizatiti kuimarisha Taasisi za Utafiti na Maendeleo ya Teknolojia yaani TIRDO, TEMDO na CAMARTEC kwa kufanya tathmnini ya kitaalam, kupitia upya na kwa kina majukumu na miundo ya kisheria ya taasisi hizo. Lengo ni kuzifanyia maboresho mahsusi yatakayozingatia ushauri wa kitaalam na itakapoonekana inafaa, zitafanyiwa maamuzi ya kimuundo ikiwemo kuziunganisha ili ziweze kuwa na tija na ufanisi katika kuleta mwendelezo wa mafanikio ya taasisi hizo na pia kuongeza nguvu katika kuendeleza viwanda nchini.
Mheshimiwa Spika; Serikali pia kwa kuzingatia tathmini ya kitaalam, itajielekeza katika kuimarisha taasisi za uwekezaji nchini hususan EPZA na NDC ili ziwe mihimili na nguzo za uwekezaji katika viwanda ambavyo ni muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa lakini wakati mwingine sekta binafsi haiko tayari kuwekeza. Msukumo ukiwa ni kuunda taasisi / mamlaka mpya itakayobeba jukumu la kujenga viwanda mama, viwanda vya kimkakati.
-
Kutunga Sheria (Business Facilitation Act) kutekeleza Mpango Kazi - BLUEPRINT
Mheshimiwa Spika; ujenzi wa mazingira bora na endelevu ya biashara ni kichocheo kikubwa na muhimu katika kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Hivyo, Serikali kupitia Wizara yangu imejipanga kuhakikisha kuwa inaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini. Maboresho hayo yatavutia wawekezaji wa ndani na nje katika viwanda na biashara na hivyo kuwezesha kutumia fursa mbalimbali za ndani na nje ya nchi kadri zinavyojitokeza. Misingi ya maboresho ya mazingira ya kibiashara yanategemewa kuwekewa nguvu ya kisheria na utaratibu wenye ushirikishaji mpana zaidi wa wadau.
-
Muunganisho wa Kiutendaji Kati ya Wizara na Mamlaka za Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa utendaji kazi wenye tija katika ngazi za Makatibu Tawala Mkoa (RAS) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs), Kada za Maafisa Biashara zitapewa msukumo wa kipekee, ili kuhakikisha inahuishwa na kufanya kazi zake kitaaluma. Aidha, Wizara imeanza mazungumzo na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuandaa Mkataba wa Makubaliano (Memorandum of Undestanding) wa kuweka mifumo na mazingira bora ya kufanya kazi pamoja na kwa kushirikiana.
-
Utungaji wa Sheria ya Kujilinda Dhidi ya Athari za Biashara (Trade Remedies Act, 2020)
Mheshimiwa Spika; Wizara inaendelea na taratibu za kutunga Sheria ya Kujilinda Dhidi ya Athari za Kibiashara ya mwaka 2020 (Trade Remedies Act, 2020) ambayo inalenga kulinda biashara na viwanda vya ndani. Ulinzi huo unalenga kuzuia uingizwaji wa bidhaa kwa wingi (import surge); bidhaa kuuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na bei ya bidhaa kama hizo kwenye nchi zinakotoka (dumping); na bidhaa nyingine kupewa ruzuku (subsidies) na nchi zao au taasisi nyingine na hivyo kuathiri bidhaa ambazo zinazalishwa ndani ya nchi bila kupata ruzuku. Mapendekezo ya kutunga Sheria hiyo yamekwishawasilishwa Serikalini kwa ajili ya maamuzi.
-
Utekelezaji wa Mikakati Mbalimbali ya Uendelezaji Viwanda Nchini
Mheshimiwa Spika; Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Ngozi wa mwaka 2016-2020 umejikita katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa Zao la Ngozi. Katika kutekeleza mkakati huo, Serikali imetoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi na vifaa vinavyotumika kutengenezea viatu na bidhaa za ngozi vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi. Lengo likiwa ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa viwanda vya ngozi na kuvutia uwekezaji. Fursa hiyo imetumiwa na Kiwanda cha Karanga Leather Industries ambacho hivi karibuni kimeingiza mashine na vifuasi (accessories). Vilevile, Kiwanda cha ACE leather Morogoro kimetumia fursa hiyo kuingiza mashine na vifuasi ili kusindika ngozi hadi hatua ya mwisho. Mkakati huo pia umehamasisha taasisi za umma na shule kununua bidhaa za ngozi hususan viatu kutoka viwanda vya ndani kulingana na upatikanaji. Kwa sasa maandalizi ya kuhuisha Mkakati huo yanaendelea.
-
Kuimarisha Sekta Binafsi
Mheshimiwa Spika; mtazamo wa Sera za Taifa zinatambua nafasi ya sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi. Kujenga sekta binafsi hasa wajasiriamali wadogo kwa kuwawekea mazingira wezeshi na rafiki kupitia upatikanaji wa mitaji, teknolojia rahisi na rafiki, masoko ya uhakika na huduma muhimu zinazolenga kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji ni suala lisilohitaji mjadala. Hivyo, katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara, mtazamo wa kisera utalenga kukuza na kutengeneza uwekezaji kuanzia ngazi ya ujasiriamali mdogo hadi kuwa matajiri wazalendo wa baadaye. Msukumo utawekwa katika kuweka sera zinazotabirika, kujenga mazingira yanayotabirika na kutoa fursa ya masoko.
-
Nguvukazi Kukidhi Mahitaji ya Viwanda
Mheshimiwa Spika; suala la kuwa na rasilimali watu ya kutosha yenye sifa, uwezo na inayotumika vizuri ni muhimu katika kujenga uchumi endelevu wa viwanda. Wizara imejipanga kuendeleza kimkakati rasilimaliwatu iliyonayo kwa kuwa na mpango mpana wa kuwaendeleza na kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara ili kuongeza ujuzi na weledi katika kutekeleza majukumu yao. Hii itawezesha kuboresha huduma zitolewazo na kukidhi matarajio ya wadau na umma wa ujumla. Tutajielekeza zaidi katika maeneo ya kuboresha huduma (service delivery) kwa njia mbalimbali, kuimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za kisekta (Regulatory role) na kuishirikisha sekta binafsi na wadau wengine kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi. Ili kuwa na rasilimaliwatu yenye afya, Wizara itahakikisha kuwa watumishi wanapata elimu ya afya na huduma za kinga dhidi ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
-
Kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji
Mheshimiwa Spika; kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya msingi na wezeshi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na ufanyaji biashara ni suala la msingi. Uendelezaji wa miundombinu hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi utapewa msukumo zaidi ili kuleta tija na mvuto kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Wizara itashirikiana na Balozi za Tanzania pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji kuja na mkakati wa kuvutia wawekezji kutumia sehemu ambazo zimefidiwa chini ya EPZA. Pia, imezindua miradi ya ujenzi wa miundombinu hiyo katika mikoa yote nchini ambapo kwa Mkoa wa Dodoma tumeanza na ujenzi wa Kongano la Viwanda Kizota (Kizota Industrial Cluster).
-
Uendelezaji wa Miradi ya Kimkakati na ya Kielelezo
Mheshimiwa Spika; katika kuendeleza Miradi ya Kimakati, Wizara, TIRDO, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), na African Minerals and Geosciences Centre (AMGC) ilifanya uhakiki wa awali wa wingi na aina za madini yaliyopo kwenye miamba ya Liganga. Matokeo ya awali yalibainisha kuwa kuna tofauti ya wingi na aina za madini ikilinganishwa na ilivyobainishwa katika taarifa ya mwekezaji. Utafiti wa kina unaendelea kufanyika kwa nia ya kubainisha hali halisi ya rasilimali zilizopo. Aidha, NDC kwa kushirikisha na uongozi wa Wilaya ya Ludewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekamilisha kazi ya uthaminishaji mali ndani ya eneo la mradi ili kufidia wananchi watakaopisha Mradi unganishi wa Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Spika; TIRDO inaendelea kufanya “Techno Economic Study” katika Mradi wa Magadi Soda Engaruka. Lengo la utafiti huo ni kubainisha kiasi cha mahitaji ya magadi nchini, thamani ya uwekezaji utakaofanyika na faida za mradi huo kwa ujumla. Makadirio ya awali ya rasilimali magadi (brine) yameonesha uwepo wa kiasi cha mita za ujazo Bilioni 4.68. Aidha, ilibanika kuwa rasilimali hiyo inajiongeza kwa kiasi cha mita za ujazo wa Milioni 1.9 kwa mwaka. Uhakiki wa rasilimali hiyo unaendelea sambamba na ukamilishaji wa upembuzi yakinifu wa mradi na athari ya mradi katika mazingira na jamii. Utafiti huo unategemewa kukamilika mwisho mwa mwezi Aprili, 2020.
-
Vipaumbele kwa Bajeti ya Mwaka 2020/2021
Mheshimiwa Spika; vipaumbele vya bajeti na malengo ya sekta ya viwanda na biashara ya mwaka 2020/2021 vimeelezewa kwa kina ukurasa 138 hadi 181 ya hotuba ya bajeti.
-
MAKADIRIO YA MAKUSANYO NA MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/2021
-
Makusanyo ya Serikali
-
Mheshimiwa Spika; Katika mwaka 2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya Shilingi 15,000,000 kutokana na uuzaji wa nyaraka za zabuni na makusanyo mengine. Kati ya fedha hizo, Shilingi 9,000,000 zitakusanywa katika Fungu 44 na Shilingi 6,000,000 zitakusanywa katika Fungu 60.
-
Maombi ya Fedha
Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka 2020/2021, Wizara ya Viwanda na Biashara inaomba kutengewa jumla ya Shilingi 81,366,902,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 51,679,016,000 ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi 29,687,886,000 ni za Matumizi ya Maendeleo. Aidha, katika Bajeti hiyo, Shilingi 57,414,395,000 ni za Fungu 44 na Shilingi 23,952,507,000 ni za Fungu 60.
-
SHUKRANI
Mheshimiwa Spika; ujenzi wa uchumi wa viwanda ni shirikishi na jumuishi, hivyo huhitaji ushiriki wa wadau mbalimbali. Kwa kutambua umuhimu huo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati washirika wetu wa maendeleo, zikiwemo nchi rafiki. Vilevile, nashukuru taasisi zote, sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali (CBOs & FBOs) kwa kuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa uchumi wetu. Kama nchi, tunaendelea kutegemea ushirikiano wenye tija katika kufikia malengo endelevu ya jamii nzima ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika; Naomba nihitimishe kwa kuwashukuru tena Watanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na hivyo kuwa kichocheo cha kukua kwa sekta nyingine za uchumi. Ni dhahiri kuwa Taifa kwa kipindi hiki kinahitaji kuendeleza ari hiyo katika kupambana na majanga mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa mafua makali wa KORONA. Kwa pamoja tuungane kujikinga na kulindana ili Taifa libaki salama na likiwa na nguvukazi ya kutegemewa.
-
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika; Wizara ninayoisimamia imeazimia kuendeleza maamuzi makini na yenye mashiko ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda wenye mafanikio ambayo yanajitafsiri katika ubora wa maisha ya kila mwananchi na Taifa kwa ujumla. Hivyo, Sera, Sheria na Mikakati iliyopo itaendelea kuboreshwa ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuchochea mbinu za utekelezaji ili kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi. Ni dhahiri kuwa jitihada hizo pamoja na utekelezaji wa Blueprint utatutoa hapa tulipo na kutupaisha katika maendeleo na kufikia lengo la uchumi wa kati ifikapo 2025 kama ilivyoazimiwa na Dira ya Taifa ya 2025. Inawezekana, endapo kila mmoja wetu atachukua nafasi yake na kujituma ipasavyo.
-
MAOMBI RASMI YA FEDHA
Mheshimiwa Spika; Naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe makadirio ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 15,000,000 na matumizi ya jumla ya Shilingi 81,366,902,000 kwa mwaka 2020/2021.
-
MWISHO
Mheshimiwa Spika; Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara yenye anuani ifuatayo: www.mit.go.tz.
Mheshimiwa Spika; Naomba kutoa hoja.
No comments: