JUNI 15, 2020 MWISHO USAJILI MIRADI YA UCHENJUAJI DHAHABU KWA AJILI YA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA NA UKAGUZI WA MAZINGIRA
JUNI 15, 2020 MWISHO USAJILI WA MIRADI YA UCHENJUAJI DHAHABU (LEACHING AND ELUTION PLANTS) KWA AJILI YA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA (ENVIRONMENTAL IMPACT ASSESSMENT) NA UKAGUZI WA MAZINGIRA (ENVIRONMENTAL AUDIT)
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linawatangazia wawekezaji wote wanaojihusisha na shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu (“vat leaching na elusion plants”) kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, Kifungu cha 81 na Kanuni za Tathmini ya Athari kwa Mazingira ya Mwaka 2005, zilizofanyiwa marekebisho Mwaka 2018 Miradi yote inatakiwa kuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au Cheti cha Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit).
Kifungu Na 7 cha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 kinasisitiza umuhimu wa kulinda, kutunza na kusimamia uhifadhi wa mazingira. Aidha, uwekezaji wowote unatakiwa kukidhi matakwa ya kisheria hususan katika suala zima la Tathmini ya Athari za Mazingira. Tathmini ya athari za mazingira ni takwa la kisheria na nguzo muhimu inayosaidia kuhakikisha athari za mazingira kwenye shughuli za maendeleo zinapatiwa ufumbuzi mapema (Precautionary Principle).
Kutokuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit) kwa miradi hiyo ni kosa kisheria na utachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufungiwa shughuli zako. Kwa hiyo, Baraza linawakumbusha wenye miradi yote ya jinsi hiyo kuwa, lazima miradi iliyotajwa kwenye Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit) na kupata cheti cha Mazingira. Kutofanya hivyo ni kutenda kosa kwa mujibu wa kifungu Na. 81 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004.
Tamko hili linafuatia athari kadha za kimazingira zilizobainishwa ambazo zinazosababishwa na uchenjuaji wa madini ambazo zimepelekea vifo vya mifugo na kuathirika kwa afya za wakazi kwenye maeneo yanayozunguka shughuli hizo. Hivi karibani matukio ya vifo vya mifugo na kuathirika kwa afya za wakazi kwenye maeneo hayo vimeongezeka mbali ya uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji, mmomonyoko wa ardhi na uchafuzi wa hewa za sumu kuwepo karibu na maeneo ya makazi.
Kama huna cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit), Baraza linakutaka kusajili mradi wako ndani ya siku thelethini (30) kwenye ofisi za Baraza Makao Makuu, Mtaa wa Migombani Mikocheni Dar es Salaam. Au, unaweza kusajili katika Ofisi za Kanda zilizopo Mikoa ya Arusha, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Mtwara na Mwanza ili kupata cheti hicho. Baraza linawataka kufanya hivyo mara moja na kutakuwapo na ukaguzi wa kina kutathmini utekelezaji wa agizo hili, kuazia tarehe 15 June, 2020.
Orodha ya Wataalamu elekezi kwa ajili ya usajili wa miradi hiyo pamoja na tathmini ya athari za mazingira na kaguzi za mazingira inapatikana katika Tovuti ya Baraza (www.nemc.or.tz). Aidha, Orodha hiyo itatolewa kwa mara nyingine kwenye magazeti yatolewayo kila siku, pamoja na namba zao za simu.
Wataalamu elekezi kwa shughuli hii ni wale tu waliokidhi matakwa ya sheria baada ya kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya kuhuisha daftari (register) la orodha ya wataalamu elekezi waliosajiliwa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Tathmini ya Uhakiki wa Athari za Mazingira.
Wataalam elekezi vilevile mnakumbushwa kuwa Gharama mnazotoza kwa ajili ya kazi za tathmini za athari kwa mazingira na kaguzi za mazingira ziwiane na uhalisi wa shughuli husika. Ili kuweza kuwasaidia wawekezaji hao, Bei ya kazi ya tathimini iwe gharama ziwe na mchanganuo wa gharama halisi ya kuaganya kazi kwa maana ya mahitaji ya lazima kwa ajili ya tathmini na kaguzi na itofautishwe bayana na ada ya mtaalam husika (professional fee).
Kwa maelezo zaidi piga namba: 0737796252 dawati la malalamiko na msaada
Imetolewa na :Mha. Dkt. Samuel Gwamaka Mafwenga
Mkurugenzi Mkuu,
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
No comments: