WIZARA YA AFYA YAPOKEA MSAADA KUTOKA TAASISI YA MILELE ZANZIBAR FOUNDATION

Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 13/04/2020.

NAIBU Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amewataka wananchi na Taasisi za kiraia kushirikiane na Serikali katika mapambano dhidi ya maradhi ya Corona.

Amesema mashirikiano ya pamoja kati ya wananchi na viongozi na kufuata maekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya yatasaidia kushinda vita dhidi ya maradhi hayo.  

Naibu Waziri wa Afya alitoa kauli hiyo baada ya kupokea msaada wa vifaa vya kujikinga na maradhi ya Corona kutoka Taasisi ya Milele Foundation Zanzibar kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano hayo.

"Wananchi tukijidhatiti kushirikiana na Serikali kupiga vita janga hili la Corona kama tulivyoshirikiana wakati wa maradhi ya kipindupindu na tukashinda," alisisitiza Naibu Waziri wa Afya.

Harusi Said Suleiman alitoa shukrani kwa Jumuiya ya Milele Foundation Zanzibar kwa kuunga mkono Serikali kupitia Wizara ya Afya na amesema vifaa hivyo  vitasambazwa katika sehemu zenye mahitaji ikiwemo vituo vya afya mijini na vijijini.

Amezitaka Jumuiya na Taasisi nyengine zikiwemo za kiraia kuiga mfano ulioonyeshwa na Milele Foundation katika kuhakikisha janga la Corona linaondoka nchini.

Mkuu wa Miradi wa Milele Foundation Zanzibar Khadija Mohamed Sharif amesema msaada wa vifàa vya kujikinga na maambukizi ya Corona ni hatua ya awali na wataendelea kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu na Jumuiya ya gari za Daladala kutoa elimu kwa madereva na abiria juu ya maradhi hayo.

Ameitaka jamii kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima pamoja na kukosha mikono kwa maji ya kutitirika mara kwa mara.

Nae Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Shirika la Msalaba Mwekundu Mwatima Kombo Said, amesema wataendelea kutoa elimu  kwa jamii kwa njia mbali mbali pamoja na kugawa vipeperushi  vyenye muongozo wa kujiepusha na maambukizi ya maradhi ya corona mjini na vijijini.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya gari za Daladala Zanzibar Said Abdalla Suleiman amewataka abiria kabla ya kuingia ndani ya gari kuhakikisha kuna nafasi ya kukaa kwani ipo sheria ya abiria anaezidi ndani ya gari kupelekwa mahakamani kama wanavyopelekwa madereva na makonda .

“Abiria usipande gari kama hakuna nafasi ya kukaa, sheria za kupelekwa mahakamani kwa abiria aliekosa nafasi ya kukaa zipo na ingefaa zitumike hasa kipindi hichi cha mapambano dhidi ya Corona,“alishauri Mwenyekiti huyo .

Vifaa vilivyotolewa na Milele Foundation Zanzibar ni pamoja na vifaa vya kupima joto la mwili, ndoo, sabuni za kukoshea mikono, tishu, glavzi, Sanitizer na mafuta ya gari lita 1,500 kwa ajili ya kufuatilia wagonjwa wa Corona vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 32.
 :Mwenyekiti wa Jumuiya ya Daladala Zanzibar Saidi Abdalla Sleiman akizungumzia  kuhusu uingiaji wa abiria kwenye gari  katika kujiikinga  na maradhi ya Corona huko Wizara ya afya  Zanzibar.
 Mjumbe wa Halmashauri kuu wa shirika la Msalaba Mwekundu Zanzibar Mwatima Kombo Said akieleza mikakati yao ya kutoa elimu kuhusiana na mapambano dhidi ya  Corona huko Wizara ya afya Mnazi mmoja Zanzibar.
 Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleman akipokea msaada wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Corona kutoka Taasisi ya Milele  Foundation Zanzibar hafla iliyofanyika katika Wizara ya Afya Mnazi mmoja  Zanzibar.PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO
Mkuu wa Miradi wa Taasisi ya  Zanzibar  Milele Foundation Khadija Mohammed Bakar akitoa maelekezo  juu ya matumizi ya chanja maalum ya kunawa mikono wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kujikinga na Corona katika Wizara ya Afya Zanzibar .

No comments: