WALIOCHAPISHA TANGAZO LINALOSEMA 'JANET MAGUFULI SACCOS' WAFIKISHWA KORTINI WAKIKABILIWA NA KESI YA UHUJUMU UCHUMI
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MWANAMKE Masse Uledi (43) ambaye ni Mkazi wa Kitunda Magore na mfanyabiashara Nkinda Shekalage (34), anayeishi Tegeta wazo wamewamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando ambayo ni kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon imeeleza katika shtaka la kwanza kuwa kati ya Januari 20 na Machi 31 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam na katika maeneo mengine ya ndani ya Tanzania washtakiwa hao kupitia mtandao wa Facebook walichapisha taarifa za uongo.
Imedaiwa walichapisha ujumbe unaosema JANET MAGUFULI saccos "mpya mpya isome tafadhali mkopo yote ni online tuu! na utapata ndani ya hakika 45 tu, mikopo huanzia kutolewa kuanzia laki tatu hadi milioni ishirini kufuata utaratibu huu ili kupata mkopo ..... tuna namba za kitambulisho champ cha mpiga kura au NIDA na majina yako matatu kupitia namba 0685012921 kisha. Piga namba hiyo ili upatiwe namba ya mhasibu ili kuweka akiwa hatimae kupata mkopo...", ambapo walifanya hivyo huku wakijua kuwa si kweli na walikuwa na lengo la kuipotosha jamii.
Katika shtaka la pili imedaiwa, siku na mahali hapo washtakiwa hao kwa njia ya udanganyifu walijipatia Sh. 15,068 650 kupitia muamala wa simu iliyosajiliwa kwa jina la Adam Mamba huku akijua kuwa si kweli.
Aidha, katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha imedaiwa washtakiwa hao walijipatia kiasi hicho cha fedha huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi wanayoshtakiwa nayo haina dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 30 mwaka huu na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.
Watuhumiwa wa tukio hilo wakiwa Mahakamani
No comments: