POLISI AKATWA MKONO AKIWA DORIA YA KUDHIBITI CORONA INDIA


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

POLISI mmoja nchini India amekatwa mkono kwa upanga na maafisa wengine sita kujeruhiwa vibaya mara baada ya kushambuliwa wakati wa kutekeleza zuio la watu kutoka nje (Lockdown) ikiwa ni sehemu ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona (Covid -19) huko Punjab kaskazini mapema leo asubuhi, Shirika la kimataifa la utangazaji la CNN limeripoti.

Imeelezwa kuwa sehemu ya mkono (kiwiko) wa kushoto wa Harjit Singh, mkurugenzi msaidizi wa Polisi wa Punjab ulijeruhiwa vibaya na baadaye ilirudishiwa kwa kufanyiwa upasuaji uliodumu takribani masaa nane.

Shambulio hilo lilitokea wakati gari lililokuwa limebeba watu saba  waliosadikika kuwa ni wanakikundi cha wapiganaji wachache wa Sikh kinachojulikana kama Nihangs waliosimama katika uwanja wa biashara nje ya soko la mboga wilayani Patiala na polisi walipowauliza wanaume hao hati halali za kusafiri, mmoja wao akatoa upanga kumkata mkono Singh.

Aidha maafisa wa polisi wameonesha silaha zenye ncha kali zilizopatikana huko Patiala, India, Aprili 12.

Maafisa wengine waliojeruhiwa, mmoja akiwa na majeraha ya upanga mgongoni walipelekwa katika Taasisi ya Uzamili ya Mafunzo ya Utabibu na Utafiti huko Chandigarh.

Kiongozi wa Serikali nchini humo  Amarinder Singh kupitia ukurasa wake wa Twitter amechapisha taarifa inavyoeleza namna upasuaji wa kurudisha sehemu ya mkono (kiwiko) ulivyochukua  takribani masaa manane na amewashukuru  madaktari na wafanyakazi kwa msaada na kumtakia Harjeet Singh ahueni ya haraka.

Aidha  imeelezwa kuwa hatua kali  zitachukuliwa kwa yeyote ambaye atakiuka taratibu na muda uliopangwa.

Kufuatia operesheni ya saa moja katika gurdwara ya eneo hilo (hekalu la Sikh) polisi waliwakamata watu hao saba waliotuhumiwa na  uchunguzi zaidi unaendelea.

 Kwa mara ya kwanza  India imefunga reli zake katika miaka 167 na sasa treni zimegeuzwa kuwa hospitali.

India kwa sasa iko chini ya kizuizi cha kitaifa hadi Aprili 30 huku Punjab likiwa jimbo lililoripoti jumla ya kesi 151 zilizothibitishwa za virusi vya  Corona, wagonjwa waliopona 5 pamoja na vifo 11.

No comments: