KMC WAAHIDI USHINDI DHIDI YA AS KIGALI LEO
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Timu ya KMC inashuka dimbani leo kucheza mchezo wa Mkondo wa pili wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya As Kigali.
Mchezo huo utaanza majira ya saa 9 alasiri katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam .
Mchezo wa kwanza nchini Rwanda uliweza kumalizika kwa suluhu ya 0-0 ambapo KMC inahitaji ushindi wa aina yoyote ili iweze kuvuka hatua inayofuata.
Kocha Mkuu wa KMC Jackson Mayanja ameahidi ushindi kwa kuwa wachezaji wake wapo imara kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano dhidi ya AS Kigali utakaochezwa uwanja wa Taifa.
Mayanja amesema mchezo huo wa leo utakuwa wa wazi kwa pande zote na wachezaji wamejiandaa kwa ajili ya kupata matokeo chanya licha ya kutokuwa na washambuliaji halisi.
"Kuna baadhi ya majeruhi ambao wapo kwetu jambo linalotuumiza, Hatuna mshambuliaji kutokana na majeruhi ukimuangalia Salim Aiyee kwa sasa hayupo sawa ila tumejipanga kufanya vizuri kikubwa sapoti," amesema.
Kikosi cha KMC kitaongozwa na Golikipa mzoefu Juma Kaseja ambapo kwa pamoja wameendelea kujionea kuelekea mchezo wa kesho na wana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi na wamewaomba watanzania wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia mchezo huo.
Kwa upande wa As Kigali wao watakuwa na mchezaji wa zamani wa Klabu ya Yanga na Simba Haruna Niyonzima ambaye kwa sasa anacheza kwenye timu hiyo.
No comments: